Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2025-2030 Session 3 Sitting 18 Regional Administration and Local Government Authorities Ofisi ya Waziri Mkuu-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) 205 2026-04-28

Name

Devotha Daniel Mburarugaba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DEVOTHA D. MBURARUGABA aliuliza:-

Je, Serikali ipo tayari kutenga dirisha maalumu la mikopo kwa sekta za kipaumbele za kilimo cha kahawa, ufugaji na biashara ndogo ndogo – Kagera?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Daniel Mburarugaba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wa Mkoa wa Kagera unategemea sana sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na biashara ndogo ndogo. Serikali imekuwa ikitoa mikopo mbalimbali ili kuwawezesha wananchi wake. Mikopo hiyo ni pamoja na mikopo ya 10% inayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri; mikopo ya kuwezesha shughuli za ufugaji wa mifugo na samaki kwa kutumia vizimba inayotolewa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi; mikopo kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (Building a Better Tomorow – BBT) na Mfuko wa Pembejeo inayoratibiwa na Wizara ya Kilimo. Aidha, ipo mikopo inayotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii kwa wajasiliamali wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Serikali imeanzisha Benki ya Maendelo ya Kilimo na Ushirika ambayo imepewa jukumu mahsusi la kutoa mikopo kwa ajili ya kuwezesha sekta za kipaumbele za kilimo ikiwemo kilimo cha kahawa, ufugaji na biashara ndogo ndogo. Mwaka 2024/2025 Serikali imetoa mikopo ya shilingi milioni 742.67 kwa makundi mbalimbali ya Mkoa wa Kagera kupitia mikopo ya 10%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kwa sasa Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetoa matangazo ya kutoa mikopo ya shilingi bilioni 200 ambazo ni ahadi ya Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwezesha wananchi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi zikiwemo kilimo, ufugaji wa mifugo na samaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutoa elimu na hamasa kwa jamii na makundi husika ili kunufaika na fursa za mikopo mbalimbali.