Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
| Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
|---|---|---|---|---|---|---|
| 2025-2030 | Session 3 | Sitting 18 | Works and Transport | Wizara ya Uchukuzi | 216 | 2026-04-28 |
Name
Kiza Hussein Mayeye
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. KIZA H. MAYEYE aliuliza:-
Je, wananchi wa Kigoma watanufaikaje na Mkataba baina ya Mamlaka ya Bandari Tanzania na Kampuni ya Zijin ya China kuendesha Bandari ya Kigoma?
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa Mnyaa, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Kiza Hussein Mayeye, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TPA inaendelea na mpango wa maboresho ya Bandari ya Kigoma ili kunufaika na fursa za Tanzania kuwa lango la biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati hususan Mashariki mwa nchi ya DRC kwani, Bandari ya Kigoma ni kiungo muhimu katika Ushoroba wa Kati kuelekea Bandari ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutimiza azma hiyo, Serikali kupitia TPA waliingia makubaliano na Kampuni ya Zijin International Mining PTE Limited ambaye kwa Tanzania anatambulika kama Gold Marine Tanzania Limited ili kuboresha Bandari ya Kigoma na gati la “Malindi Wharf” katika Bandari ya Dar es Salaam. Mawanda ya makubaliano baina ya TPA na Mwekezaji yanajumuisha usanifu na kugharamia maboresho ya miundombinu, usimikaji wa mifumo ya kisasa, ununuzi wa vitendea kazi na uendeshaji. Aidha, TPA ataendelea kutoa huduma kwa meli na huduma nyingine zilizoainishwa kwenye makubaliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla, wananchi wa Kigoma na nchi watanufaika kwa namna mbalimbali ikiwemo kuongeza mtaji wa uwekezaji nchini; kupitia uwekezaji huo, kutaongeza ufanisi wa utoaji wa huduma katika bandari hiyo, na hivyo kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi katika Mkoa huo na Ziwa Tanganyika kwa ujumla; kupatikana kwa mapato yatokanayo na ada ya uendeshaji na upangishaji; kujenga uwezo wa Watanzania kuwa na ujuzi stahiki; kuongeza ajira kwa Watanzania; kuongeza upatikanaji wa shehena mpya hususan kutoka Mashariki mwa DRC; ushiriki wa kampuni za ndani; na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine za uchumi, kama vile kilimo, uvuvi na viwanda.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved