Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Kiza Hussein Mayeye

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. KIZA H. MAYEYE aliuliza:- Je, wananchi wa Kigoma watanufaikaje na Mkataba baina ya Mamlaka ya Bandari Tanzania na Kampuni ya Zijin ya China kuendesha Bandari ya Kigoma?

Supplementary Question 1

MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, uendeshaji wa Bandari ya Kigoma unakwenda sambamba na uwekezaji wa meli, hasa meli za mizigo ambazo zingeweza kwenda Congo DRC katika mgodi mkubwa sana wa madini ya lithiamu, pale Manono katika Jimbo la Tanganyika. Sasa ni miaka mitatu Serikali imesaini mkataba wa ujenzi wa meli ya mizigo, hakuna ambacho kinaendelea. Serikali haioni inawakosea watu wa Kigoma kwa kuwakosesha fursa na mapato? Ni lini mradi huu utakamilika ili tuweze kupata meli hizo za mizigo?

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Mheshimiwa Kiza Mayeye kwa namna anavyoungana na Wabunge wote wa Chama cha Mapinduzi katika mkoa huo, na Tanzania kwa ujumla, katika kufuatilia kwa karibu miradi ya kimkakati katika Ziwa Tanganyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua umuhimu na umadhubuti wa Ziwa Tanganyika kwa uchumi wa nchi yetu na kwa uchumi wa wananchi wa Kigoma. Ndiyo maana kwa mara ya kwanza tunaona uwekezaji mkubwa unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niseme kwa ufupi kidogo. sote tunakubaliana katika maji yote ambayo yapo duniani, Ziwa Tanganyika linakuwa namba mbili likiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 32,900 na takribani upana wa karibu kilomita 50. Hata hivyo, ziwa hili ndiyo la pili duniani kwa kuwa na kina kirefu zaidi kwa maziwa yenye maji masafi; pia, kama nchi tuna karibu 41% ya ziwa lote, na wengine wanabaki na sehemu inayobaki. Hivyo, inaturahisishia kupeleka bidhaa au vitu mbalimbali kwenye nchi ya Congo, Burundi pamoja na Zambia na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hivi ninavyozungumza mpaka kufika mwaka 2020 Ziwa Tanganyika, meli karibu zote zitakuwa zimelala. Nini Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya? La kwanza kabisa, amesaini mikataba ya uboreshaji wa bandari, uboreshaji wa meli. Meli ya kwanza ni MV Liemba ambayo Mheshimiwa Mbunge mwenyewe mara kadhaa alizungumza hapa na tumekwenda wote kuitembelea, ipo karibu 64%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, MV Sangara, hii ni meli kwa ajili ya kubeba mafuta, tayari imeshaanza kufanya kazi. Tatu ni MV Mwongozo, hii tumeshasaini mkataba, tunachosubiri kwa sasa hivi ni kulipwa fedha ili kazi ianze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyozungumza kuhusu meli ya mizigo, inayobeba tani 3,500, Serikali imeshasaini mkataba, na nimhakikishie, inakamilisha taratibu za ndani za kulipa fedha. Fedha zikipatikana, atalipwa mkandarasi ili kuanza ujenzi kama ambavyo miradi mingine imeshaanza.