Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
| Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
|---|---|---|---|---|---|---|
| 2025-2030 | Session 3 | Sitting 16 | Industries and Trade | Wizara ya Viwanda na Biashara | 185 | 2026-04-24 |
Name
Mgore Miraji Kigera
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Musoma Mjini
Primary Question
MHE. MGORE M. KIGERA aliuliza:-
Je, nini kauli ya Serikali juu ya kufufua viwanda vilivyotelekezwa muda mrefu ili kuleta ajira kwa Watu wa Musoma?
Name
Denis Lazaro Londo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mikumi
Answer
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara ninaomba nijibu swali namba 185 kutoka kwa Mheshimiwa Mgore Miraji Kigera, Mbunge wa Musoma Mjini:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mara ni moja ya mikoa ya kipaumbele katika suala zima la ufufuaji wa viwanda na ujenzi wa viwanda vipya. Katika mkoa huo, hasa Wilaya ya Musoma Mjini, kuna viwanda viwili ambavyo vilikuwa vinamilikiwa na Serikali ambavyo havifanyi kazi. Viwanda hivyo ni MUTEX na Kiwanda cha Musoma Dairy.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha kwamba viwanda hivi vinarudi katika uzalishaji, Serikali inaendelea kuangalia namna bora ya kufanya, ambapo baada ya tathmini ya kina ama mazungumzo, imekubalika kwamba kiwanda cha MUTEX kirejeshwe kwa mwekezaji wa awali kwa mkataba na masharti mapya. Majadiliano hayo yamefanyika na mkataba uliowasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye pia amefanya maboresho na kurejesha kwa Msajili wa Hazina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maboresho hayo yanaenda sambamba na tathmini ya kina kufanyiwa kazi, na ikikamilika, mwekezaji atakabidhiwa kiwanda ili mkataba mpya uanze kazi na shughuli za uzalishaji ziendelee. Aidha, Kiwanda cha Musoma Dairy, aliyekuwa mwekezaji wa awali ametuma maombi Serikalini akiomba arejeshewe kiwanda hicho ili aweze kuendeleza uzalishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa maombi hayo yanafanyiwa tathmini ya kina na mazungumzo yanaendelea ili yakikamilika tuangalie namna ya kufufuliwa kwa shughuli za Kiwanda hicho cha Musoma Dairy.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved