Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mgore Miraji Kigera

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Primary Question

MHE. MGORE M. KIGERA aliuliza:- Je, nini kauli ya Serikali juu ya kufufua viwanda vilivyotelekezwa muda mrefu ili kuleta ajira kwa Watu wa Musoma?

Supplementary Question 1

MHE. MGORE M. KIGERA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Musoma Mjini, kama ambavyo dhamira ya Serikali ni kukuza sekta ya viwanda kutoka 4.8% mpaka asilimia tisa ifikapo 2030, je, Serikali inatoa commitment gani kwa wananchi wa Musoma Mjini kwamba mwekezaji huyo atakapokabidhiwa kiwanda hicho, ataenda kufanya uzalishaji haraka iwezekanavyo ili wananchi hao waweze kupata ajira?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wawekezaji wengi wamekuwa wakipata viwanda hivyo na kuvitumia kama collateral, na dhamira ya dhati ya kuwekeza viwanda hivyo inakuwa haipo, na Serikali inashindwa kutatua changamoto za ajira pamoja na uchumi kwa wananchi kwa maeneo yaliyo mengi hasa ya Musoma Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, mwekezaji wa Kiwanda cha Musoma Dairy, tangu aliponyang'anywa kiwanda hicho na Serikali mwaka 2018, leo ni miaka tisa, katika kiwanda hicho kumefanyika wizi na ubadhirifu mkubwa sana, na kusema kumrudishia kiwanda hicho ili aweze kufanya investment ni kwamba tunadanganyana kwa sababu kiwanda hicho kwanza kina mkopo ambao mwekezaji alikopa TIB Bank na PTA Bank…

MWENYEKITI: Swali Mheshimiwa.

MHE. MGORE M. KIGERA: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali haioni ni muhimu kushirikiana na mwekezaji huyo kutafuta strategic investor ambaye atakuwa na mtaji mkubwa wa kuwekeza katika kiwanda hicho?

Name

Denis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mgore Miraji Kigera kwa jitihada kubwa ambazo anazifanya kuunga mkono sera ya ukuzaji wa viwanda katika nchi yetu na ongezeko la thamani ya mazao hasa katika Mkoa wa Mara hususan katika Wilaya ya Musoma Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ameomba commitment ya Serikali kuhusiana na suala zima la uzalishaji pale ambapo mwekezaji huyu mpya atakapokabidhiwa kiwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilikichukua kiwanda hiki kwa sababu ya kusuasua na kusimama kwa shughuli za uzalishaji. Mazungumzo ambayo tumeyafanya ni kuingia mkataba mpya wenye masharti mapya, ambayo yanamwelekeza mwekezaji huyu kuwa committed na hasa kwa upande wake pale ambapo hatatimiza makubaliano na Serikali, ambayo ni kuanza kwa uzalishaji pale ambapo atakabidhiwa kiwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninampa faraja Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali iko makini. Masharti ya mkataba huu mpya yanaenda kumlazimisha muwekezaji huyu kuanza shughuli za uzalishaji wa kiwanda hiki mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la Musoma Dairy, Serikali haina taarifa ya wizi na ubadhirifu, lakini kama upo, hatuwezi kushirikiana na wezi na wabadhirifu katika kujadiliana namna bora ya kufufua kiwanda hiki. Sheria zipo na tathmini inaendelea kujua athari ambazo zimesababishwa na uwekezaji katika kiwanda hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili liko kwa Msajili wa Hazina. Wizara ya Viwanda na Biashara inafuatilia kwa karibu kuona ni namna gani shughuli za kiwanda hiki cha maziwa zinarudi, ili kuongeza thamani ya mazao pale katika Mji wa Musoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.