Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA K.n.y. MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Mpalanga – Bahi?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri. Hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza. Katika Kata za Bahi, ujenzi kama ulivyosema unaendelea kufanyika kwenye vituo vya afya, lakini kuna wataalam wachache wa afya. Je, ni lini wataalam wa afya watapelekwa kwenye Kata hizo za Bahi ambapo sana ni manesi na madaktari?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili. Kuna vituo vya afya vikongwe katika Manispaa ya Morogoro ambavyo ni Sabasaba pamoja na Mafiga. Ni lini vitapata kujengewa chumba cha upasuaji ili kupunguza tatizo linalotokea kwenye Hospitali ya Mkoa pamoja na kuwapatia akinamama huduma ambao wanapata matatizo ya kujifungua kawaida? Ahsante.

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inafanya uwekezaji mkubwa sana kuendelea kuimarisha sekta hii muhimu kabisa ya afya msingi. Mheshimiwa Mbunge amehoji kuhusiana na uhitaji wa watumishi wa afya katika hii Wilaya ya Bahi kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inafanya jitihada ya kuajiri watumishi wa kada ya afya na kuwapanga katika maeneo tofuti tofauti katika vituo hivi vya kutolea huduma ya afya msingi ili waweze kutoa huduma hiyo bora zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea na jitihada hizo za kuajiri. Tayari vibali vya ajira ya watumishi hawa vinatoka kila mwaka wa fedha na watumishi hawa watapangwa katika vituo hivi alivyovitaja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la piIi la Mheshimiwa Dkt. Christine Ishengoma, ninaomba nimtaarifu kwamba, Serikali inaendelea pia kuboresha miundombinu kwa maana ya ujenzi wa hospitali, kukarabati hospitali kongwe, kujenga vituo vya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya vituo vya afya 367 vimejengwa kwenye Serikali hii ya Awamu ya Sita, zaidi ya zahanati 980 zimejengwa, na hospitali za Halmashauri 129. Kwa hiyo, unaona kabisa dhamira ya dhati ya Serikali ya kuendelea kuimarisha miundombinu katika vituo vyetu hivi vya kutolea huduma ya afya msingi katika vituo hivi alivyovitaja katika Eneo la Sabasaba na hili lingine alilolitaja Mheshimiwa Mbunge, Serikali itahakikisha inafika kwa ajili ya kujenga chumba cha upasuaji ili kiweze kuwanufaisha wananchi, waweze kupata huduma bora zaidi na hasa hizi za upasuaji. (Makofi)

Name

Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Primary Question

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA K.n.y. MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Mpalanga – Bahi?

Supplementary Question 2

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kilindi kwenye Kata ya Kiberashi ina vijiji saba, lakini ni vijiji vitatu vyenye zahanati, hawana kituo cha afya. Je, ni lini mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba tunapata kituo cha afya au kwa maana hospitali kubwa ambayo inaweza kuhudumia eneo hilo?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inahakikisha kwamba kila Halmashauri inajengewa Hospitali ya Halmashauri. Mpaka wakati huu, katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, HospitaIi za Halmashauri 129 tayari zimeshajengwa, na Serikali inaendelea kuhakikisha kila Halmashauri inapata hospitali.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia inaendelea kujenga vituo vya afya vya kimkakati katika kata za kimkakati. Fedha zinapelekwa kwa ajili ya kujenga vituo hivi vya afya. Hata katika huu mwaka wa Bajeti, tulipitisha hapa Bungeni nyongeza ya bajeti shilingi bilioni 53 kwa ajili ya kujenga vituo vya afya vya kimkakati katika kila jimbo katika majimbo 214.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge, hata kwenye Jimbo lake italetwa shilingi milioni 250 kwa ajili ya kuhakikisha kinajengwa kituo cha afya cha kimkakati. Serikali inaendelea pia na jitihada za ujenzi wa zahanati katika maeneo yote ambayo yana uhitaji na yanakidhi sifa ya kujengewa zahanati hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Serikali ya Awamu ya Sita pekee, tayari zaidi ya zahanati 980 zimejengwa. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, hata Kilindi tutaendelea kuleta fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba zahanati zinajengwa, vituo vya afya vinajengwa na huduma za afya msingi zinaimarishwa kwa ajili ya wananchi wake. (Makofi)