Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. John Danielson Pallangyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arumeru-Mashariki

Primary Question

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO K.n.y. MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza: - Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Maziwa Kijiji cha Likiushin Mnadani - Arumeru Magharibi?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali na kwa kweli nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jinsi ambavyo inaendelea kuboresha maisha ya Watanzania. Nina maswali mawili. Je, ni lini Kiwanda kitatengenezwa hapo ili kazi ya uchakataji na kuongeza thamani ya maziwa itekelezwe?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kule Meru wananchi wameanzisha taasisi yao inaitwa UWAWAME (Umoja wa Wakulima na Wafugaji Meru) kwa lengo la kuunganisha nguvu ili wajenge viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo na mifugo. Je, ni upi mkakati wa Serikali wa kuunga mkono juhudi za wananchi hawa ili wafanikishe ndoto yao kulingana na azma ya Serikali pia ya kutaka kufanya kilimo cha biashara na ufugaji wa biashara? Ahsante sana. (Makofi)

Name

Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI K.n.y. WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru, naendelea kupokea pongezi kwa niaba ya Serikali na kwa niaba ya Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi kubwa inayofanyika. Naendelea kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Pallangyo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kuhusu kiwanda au viwanda vya kuchakata maziwa. Ni kwamba, Serikali imezidi kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji kuja kuwekeza katika viwanda vya kuongeza thamani kwenye mazao ya mifugo na mazao mengine ya shambani.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali, tukizingatia hii dira ambayo ni mpya tunayokwenda kuizindua ya mwaka 2050, tumehakikisha tumeweka mazingira mazuri kwa maana ya kupeleka miundombinu ya maji, umeme na barabara kwenye maeneo mbalimbali nchini, ili kuvutia wawekezaji waweze kuwekeza kila eneo kutokana na mazao wanayozalisha katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mazao ya kutoka shamba na mazao ya mifugo, ikiwemo uchakataji wa maziwa, ni moja ya mkakati madhubuti ambao Serikali imekwenda kuuweka. Tunakwenda kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji kuja kuwekeza katika bidhaa zinazozalishwa na mifugo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kwamba, Serikali imezidi kutoa mikopo kwa wafanyabiashara, especially, akinamama, walemavu, vijana na watu wengine wote ili kwenda kuwekeza. Ili waweze kupata mikopo ya 10% inayotokana na halmashauri tunawashauri, hawa wakulima waungane kuomba ili waweze kuwekeza kwa ajili ya kuchakata maziwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile juzi Mheshimiwa Rais alipokuwa Mkoani Simiyu, amezindua chanjo ya mifugo pamoja na kutoa ruzuku kwenye mifugo kwa ajili ya kuwafanya wawekezaji au wanaowekeza kwenye mifugo waweze kupata mikopo mbalimbali ili kupata tija katika kuwekeza katika masuala yote ya ufugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi.