Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Stella Ikupa Alex

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. STELLA I. ALEX aliuliza: - Je, Serikali inachukua hatua zipi kwa Halmashauri ambazo hazitengi fedha za kununua mafuta ya Watu Wenye Ualbino?

Supplementary Question 1

MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niishukuru na kuipongeza sana Serikali kwa majibu haya mazuri. Uhalisia wa site ni tofauti na fedha ambazo zimeelezwa kwenye jibu la msingi kwamba, zinatengwa. Nini Kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba, mafuta haya yanapatikana kwenye halmashauri na Manispaa zetu, sambamba/sawasawa na fedha zinazotengwa?

Name

Dr. Jafar Rajab Seif

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busanda

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya shilingi milioni 182 zimetengwa kwa wanufaika 14,695 waliopatiwa mafuta ya lotion na pia, utambuzi unaendelea kufanyika katika maeneo yote. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Stella, kwenye maeneo ambayo bado utambuzi haujafanyika, tuendelee kuwatambua. Ni maelekezo ya Serikali kwa Wakurugenzi wetu kuendelea kuwatambua wahitaji wa mafuta haya.

Name

Nyamizi Simon Mhoja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. STELLA I. ALEX aliuliza: - Je, Serikali inachukua hatua zipi kwa Halmashauri ambazo hazitengi fedha za kununua mafuta ya Watu Wenye Ualbino?

Supplementary Question 2

MHE. NYAMIZI S. MHOJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa kwa kuwa, ni mara yangu ya kwanza kuongea katika Bunge hili, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali cha kuwepo mahali hapa, Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, namshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuniteua kuwa Mbunge, Viti Maalum, kundi la Wenye Ulemavu. Bila kuwasahau wapigakura wangu wote nchi nzima, ninawashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la nyongeza ni kwamba, Wizara ina mpango gani wa kuajiri Madaktari wa Afya ya Ngozi, maalum kwa ajili ya watu wenye ualbino kwenye hospitali zote za halmashauri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwepo wa hawa watu kwenye halmashauri utasaidia kupanga bajeti ambayo wao watakuwa na idadi kamili ya mafuta na hata kufanyiwa check-up, siyo tu lotion; check-up kwa ajili ya watu wenye ualbino kwenye halmashauri zote, ahsante.

Name

Dr. Jafar Rajab Seif

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busanda

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Sita, kipindi cha kwanza na kipindi cha pili, tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kundi hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiukweli tayari tumewaelekeza madaktari wote wa halmashauri ambako kuna uhitaji mkubwa wa wenye changamoto ya ngozi. Hivyo, pamoja na wataalamu wale 5,000 ambao tumewaajiri mwezi Januari, wamo ambao wanahusika na kufanya utambuzi wa changamoto hizi za ngozi, pamoja na kutoa ushauri katika matibabu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nderiananga.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA WENYE ULEMAVU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA) Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante ninakushukuru, pamoja na majibu mazuri ya Serikali yaliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri, ninaomba niongeze jambo kwenye eneo la mafuta kwa watu wenye ualbino.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua uhitaji wa mafuta ya ualbino kwa watu wenye ualbino nchi nzima, lakini ninamhakikishia dada yangu, Mheshimiwa Stella kwamba, Serikali kupitia ofisi ya Waziri Mkuu, chini ya Waziri wetu, Mheshimiwa Wiliam Lukuvi, tunao Mfuko wa Watu Wenye Ulemavu Tanzania ambao kwa sasa tayari tumetenga fedha. Kupitia kwenye mfuko, tuta-push fedha hiyo ndani ya wiki mbili, tangu sasa, ili iende KCMC ika-produce mafuta mengi zaidi yaweze kusambazwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa pili kupitia wenzetu Wizara ya Elimu, tunasambaza mafuta haya kwa wanafunzi. Tunanunua, kama eneo la vifaasaidizi, moja kwa moja yanawafikia shuleni. Kwa hiyo, nawatoa wasiwasi wenzangu wenye ualbino.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema na hili la pili kidogo. Tuna hospitali ambazo ni teule, kama hospitali za kanda. Kwa mfano, kule Mwanza Bugando yanafanyika matibabu hayo ya kufanya screening tangu mwanzo, watoto wanapokuwa wadogo, kwa ajili ya kutambua level yao ya aina ya ngozi, mafuta na kila kitu ambacho wanatakiwa wapate.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna KCMC, tuna Ocean Road na tunaendelea kuhakikisha huduma hizi zinaendelea kusambaa hadi chini. Kwa hiyo, nawahakikishia watu wenye ualbino wasiwe na mashaka, tuko vizuri. Serikali ya Awamu ya Sita ya Mama Samia ya Kazi na Utu Tunasonga Mbele, tutaendelea kupeleka huduma kwao, ahsante.