Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Primary Question
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza: - Je, lini Kanuni za CSR kwenye migodi zitabadilika ili miradi ya maendeleo isimamiwe na halmashauri kwa mtindo wa Local Fund badala ya mwekezaji?
Supplementary Question 1
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Halmashauri ikiendesha utaratibu wa manunuzi, darasa ambalo tunajenga kwa shilingi milioni 25 mkandarasi akiwekwa na mgodi unatumia shilingi milioni 32, nyumba single ya shilingi milioni 50 mkandarasi anaweka kwa shilingi milioni 85, nyumba pacha ambayo tungetumia shilingi milioni 70 kwa halmashauri, mkandarasi ni shilingi milioni 125. Bweni la shilingi milioni 130 wanapiga mpaka shilingi milioni 230.
Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza; ni kwa nini fedha ile isibaki kwenye mgodi, lakini mchakato wa manunuzi ufanywe na halmashauri ili kuokoa fedha hizo na tupate miradi mingi zaidi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kanuni hizi zimetoa provision ambayo inaonesha kwamba kuna team ya wataalam ya kuibua miradi. Mbunge hayupo mle ndani kwenye hiyo team, wala Mwenyekiti wa Halmashauri, wameshachakata, wamepanga miradi yao, wanaleta kwenye Kamati ya Fedha au Baraza la Madiwani unakuta hata Mbunge hayupo, unatakiwa uende kuunga mkono kitu ambacho hukijui. Je, kwa nini, katika mchakato wa kuibua miradi ile Mwenyekiti wa Halmashauri au Mbunge asiwekwe ili waanze pamoja kupanga miradi ya maendeleo ya halmashauri husika? Ahsante.
Name
Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Longido
Answer
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, suala la manunuzi kutokana na fedha za CSR limebainishwa vizuri sana kwenye kanuni hizi ambazo tumezitunga mwaka 2023.
Mheshimiwa Spika, mchakato wa kuibua miradi unaanzia kwenye ngazi ya kijiji, inaenda ngazi ya kata inaenda kwenye halmashauri na Mbunge pia ni Mjumbe katika Halmashauri ya Wilaya yake au Jimbo lake. Kwa hiyo, miradi inapokuwa imeibuliwa, inapokwenda kwenye ngazi ya kutenga fedha na utekelezaji, Kamati ya Wataalam hukaa ambayo Mwenyekiti wake ni Mkurugenzi wa Halmashauri na Katibu wake Afisa Mipango, kuna mwakilishi wa Tume ya Madini na kuna wawakilishi wawili wa mwenye mgodi.
Mheshimiwa Spika, ule mchakato wa manunuzi hufanyika kwa uwazi kabisa na anachoongelea Mbunge ni zamani kabla hatujawa na kanuni. Sasa hivi miradi yote japokuwa mwenye kutoa fedha ndiye anayesimamia akishirikiana na ile Kamati ya Wataalam, lakini Mbunge ameachwa pembeni ili awe sehemu ya check and balances, kufuatilia kama wajibu wake ulivyo kuona kwamba fedha ile imeenda kutekeleza miradi iliyokusudiwa kwa usahihi.
Mheshimiwa Spika, Mbunge anapoongelea suala la fedha hii kwa nini manunuzi yasifanyike moja kwa moja na halmashauri ni suala ambalo limefungwa kikanuni, lakini kuhusu uibuaji wa miradi ni suala ambalo linaanzia kwenye jamii, kwa hiyo hakuna kinachofanyika na mwekezaji bila ushirikishwaji wa jamii, ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved