Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mattar Ali Salum
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shaurimoyo
Primary Question
MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza: - Je, kwa nini Shirika la Ndege la Tanzania lisianzishe safari za ndege za moja kwa moja toka Zanzibar mpaka Dodoma?
Supplementary Question 1
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri ambayo ameyatoa; lakini nina maswali mawili ya nyongeza, la kwanza; ninaomba Mheshimiwa Waziri alieleze Bunge na Watanzania kuhusu mafanikio ya ATCL tangu Serikali ianze kuwekeza fedha.
Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni upi mpango wa ATCL kushika soko la kimataifa likawa kama mashirika mengine makubwa ya duniani?
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, sisi kama Wabunge na Watanzania tuna mengi ya kujivunia kwa ATCL. Tumshukuru Mheshimiwa Rais wetu kwa kuamua rasmi kuliboresha shirika letu la ndege la Tanzania. Katika miaka hii mitatu au minne ambayo Mheshimiwa Rais ameamua kuwekeza tumeona mabadiliko mengi. Kwanza, idadi ya ndege imeongezeka. Mwaka 2016 tulikuwa na ndege moja, ilipofika mwaka 2021 tukawa na ndege tisa. Mheshimiwa Rais ameongeza ndege ziko 16 ikiwemo na ndege kubwa ya mizigo; na hivyo imepelekea mzigo unaosafirishwa kuongezeka kutoka tani 1,290 hadi tani 6,900, haijawahi kutokea. Hata idadi ya abiria imeongezeka mara dufu kutoka abiria 537,000 sasa wako abiria 1,100,000.
Mheshimiwa Spika, hata mtandao wa ndege umeongezeka, hapo awali tulikuwa tunakwenda vituo vichache na leo ninapozungumza Air Tanzania inakwenda vituo takriban ukanda wote wa kusini; inakwenda takriban mikoa yote Tanzania ambapo viwanja imekamilika. vilevile Inakwenda kwenye maeneo ya kimataifa kama Guangzhou, Mumbai na Dubai; hayo yote ni mafanikio. Fedha za kigeni zimeongezeka zaidi kutoka takriban fedha iliyokuwepo mwanzoni dola milioni 43 hadi 157. Kwa hiyo, tunayo kila sababu na sifa ya kujivunia maboresho makubwa ya shirika letu la Air Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, ametaka kufahamu, kwamba je, ni mipango gani ambayo shirika inayo ya kuhakikisha kwamba linakuwa competitive na kushindana na mashirika makubwa duniani. Kwanza kabisa ni kuongeza idadi ya ndege. Ukimsikiliza Mheshimiwa Rais alipokuwa anahutubia Bunge na mara kwa mara akizungumzia sekta hii ya uchukuzi, anataka kuongeza ndege. Ukisoma Dira 2050 na Ilani ya CCM kwa umoja wake ifikapo 2030 zitaongezeka zaidi ya ndege nane hadi 10 ukilinganisha na zilizopo sasa hivi. Pili, pamoja na kuongeza ndege ambazo pia tunakwenda kuongeza vituo vya kimataifa, sasa hivi tuna vituo vitatu kama nilivyosema, ATCL ina mpango wa kuongeza vituo vingine saba na kwenda juu ili iende Ulaya, Asia na maeneo mengine ya dunia hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tatu, ATCL iliyojipanga kufanya majukumu yake kibiashara inakwenda kukodi ndege. Mashirika mengi duniani pamoja na kumiliki inakodi ndege zingine ili kuweza kushika soko la kimataifa; na sisi tunatengeneza balance sheets zetu vizuri ili tuongeze ndege nyingi zaidi, twende duniani kote tuweze ku-compete kama mashirika kwa mengine yalivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama hiyo haitoshi, tulikuwa na changamoto ya wataalam, sasa hivi tunamiliki ndege 16 lakini changamoto kubwa ni marubani. Tuna upungufu wa marubani 61 pamoja na wahandisi, (professional engineers). Ni nini tunakifanya kama shirika? Kwanza ni kuhakikisha tunajenga Chuo Kikuu cha Anga pale KIA ambacho kitajengwa hapo baadaye. Pili, kuboresha chuo chetu cha NIT. Mheshimiwa Rais ametoa fedha nyingi ili marubani wapate vifaa na utaalam wa kutosha. Kama hiyo haitoshi, tunatoa rai kwa Watanzania kupeleka vijana wetu kwenda kusoma kwenye kada ya urubani pamoja na uhandisi wa ndege kwa sababu huko hawatoshi, tunahitaji wengi waende huko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama hiyo haitoshi ni kuimarisha diplomasia yetu. Kama ambavyo Wabunge wanafahamu, Mabalozi wetu katika dunia hii wanafanya kazi nzuri sana na ninatumia nafasi hii kuwapongeza sana kwa sababu ndio ambao wametupatia masoko. Hivi ninavyozungumza mwezi huu tunakusudia kuongeza kituo kingine Accra, Ghana. Hii ni kazi nzuri ya wanadiplomasia wetu wanayoifanya huko duniani. Kwa hiyo, kote huko tutakwenda kufika na hii yote inafanywa na wenzetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama haitoshi, tunakamilisha uwanja wa Msalato. Uwanja huu ni wa kimataifa, maana yake unapoongeza viwanja vya kimataifa shirika lako la ndani linapata nguvu na uwezo wa kuongeza scope ya kutoka hapa na kwenda kwenye maeneo mengine. Kwa hiyo, mipango ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya anga hususan kuboresha shirika letu la ATCL ni mikubwa, tumwombee Rais wetu afya njema ili maono yake yaweze kutimia. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved