Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Justin Lazaro Nyamoga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Primary Question
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza:- Je, lini fidia kwa wananchi wa Kijiji cha Liugai Kata ya Luilo zitalipwa ili wapishe Mradi wa Umeme?
Supplementary Question 1
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Awali nianze kwa kuipongeza na kuishukuru sana Serikali kwa kutoa kiasi cha shilingi bilioni sita kwa ajili ya kurekebisha miundombinu ya umeme uliokuwa wa Madobe. Ahsante sana wananchi wa Ludewa wanaishukuru sana Serikali.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo niombe sasa niiulize Serikali. Swali la kwanza; Serikali itufahamishe wananchi wa Ludewa tunavyo viwanda vitatu ambavyo vinakusudiwa kujengwa kuanzia hivi sasa, lakini kituo cha kupoozea umeme kinatoka Madaba ambako ni mbali na hii inasababisha umeme kukatikakatika sana. Je, nini mpango wa Serikali kuweka bajeti kwa sababu tunaenda Bunge la Bajeti kwa ajili ya kutengeneza kituo cha kupooza umeme Ludewa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Ludewa ikihitajika kurekebishwa nguzo moja wanategemea gari kutoka mkoani. Sasa nini mpango wa Serikali kupeleka gari la kubebea nguzo Ludewa ili changamoto za wananchi ziweze kutatuliwa kwa wakati? Ahsante sana.
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joseph Zacharious Kamonga Mbunge wa Ludewa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza juu ya umeme wa uhakika katika Wilaya ya Ludewa na vile ambavyo amesema kwamba kuna viwanda vinaenda kujengwa. Nitoe taarifa mbele ya Bunge lako kwamba Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba sio Ludewa peke yake bali kila wilaya katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapata substation yake na tayari kuna mradi wa gridi imara ambapo tunamalizia hatua ya kwanza. Tutakapokwenda hatua ya pili kuna wilaya nazo zitapata substation hizo na katika hatua ya tatu Ludewa na yenyewe ipo itapata substation yake ili kuweza kuwa na umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Spika, nitakaa pia na Mheshimiwa Mbunge ili kuona viwanda hivi vinaenda kuwekwa wapi kuona maeneo ambapo vinakwenda kuweka walau kwa hatua za mwanzo tuweze kuweka transfoma ili kuwa na umeme ambao ni wa uhakika kwa ajili ya wawekezaji hao wa Ludewa wakati tunaendelea na Mradi wa gridi imara kuhakikisha umeme unapatikana.
Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili la gari la nguzo. Ni majuzi tu Shirika letu la TANESCO, Tanzania limenunua magari ya nguzo zaidi ya 270 na hivi ninavyozungumza magari haya yameshapokelewa 200 na yameanza kusambazwa katika wilaya mbalimbali hapa nchini kwetu na nitaangalia Wilaya ya Ludewa na yenyewe iweze kupata gari lake kwa haraka ili nguzo ziweze kuwafikia wananchi kwa haraka.
Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved