Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ESTER A. BULAYA aliuliza:- Je, lini Mradi wa TACTIC Awamu ya Tatu utaanza kutekelezwa katika Jimbo la Bunda Mjini?

Supplementary Question 1

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, huu mradi unasubiriwa kwa hamu kubwa sana. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; mbali na kilometa ambazo amezitaja, ingawa wenyewe wanajua 25, kulikuwa kuna ahadi ya ujenzi wa kilometa 10 za lami kwenye Mitaa ya Bunda Mjini tangu Awamu ya Serikali ya Nne. Ni lini ahadi hii itatekelezwa ukizingatia Halmashauri ya Mji wa Bunda ina kilometa moja tu ya lami na ni ya zamani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; mbali na kwamba, kwenye Mradi wa TACTIC kuna ujenzi wa masoko, lakini ninajua Serikali wana mpango wa kusaidia halmashauri ambazo bado hazijaimarika kimapato, kuwasaidia ujenzi wa masoko ya kimkakati. Kwenye Kata ya Nyasura kuna Soko la Kimkakati la Manjebe ambalo litasaidia halmashauri yetu kupata mapato. Ni lini sasa wataisaidia Halmashauri ya Mji wa Bunda ili kujenga Soko la Manjebe na Wananchi wa Bunda Mjini waweze kuinuka kiuchumi? Ninakushukuru. (Makofi)

Name

Kwagilwa Reuben Nhamanilo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Handeni Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tangu Awamu ya Nne ya Tano na sasa Awamu ya Sita imeendelea na uendelezaji wa miundombinu, hasa hasa ujenzi wa barabara za lami, ikiwemo ndani ya Mji wa Bunda. Mpaka sasa tuna kilometa za lami zipatazo 2.27 na tunaendelea na ujenzi wa barabara hizo ikiwemo Barabara ya Ikizu kwenda Maduka Saba ambayo, Mheshimiwa Mbunge anaifahamu vizuri, kwa sasa ujenzi umefikia zaidi ya 60%. Ninamwahidi Mheshimiwa Mbunge tutaendelea na ujenzi wa barabara zote ambazo zimetajwa kwa kadiri ambavyo tutakuwa tunatenga kwenye bajeti na kwa kadri ambavyo mpango wetu unatuelekeza, ikiwa ni pamoja na mpango uliowasilishwa hapa mbele ya Bunge lako leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, kuhusu masoko ya kimkakati na hususani Soko la Mwanjabe. Ninamwelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Bunda TC waandae andiko la kimkakati litakalokidhi vigezo, litapokelewa kwenye Wizara yetu ya Mipango na kupelekwa Wizara ya Fedha, kwa ajili ya kupatiwa fedha kwa ujenzi. (Makofi)

Name

Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Primary Question

MHE. ESTER A. BULAYA aliuliza:- Je, lini Mradi wa TACTIC Awamu ya Tatu utaanza kutekelezwa katika Jimbo la Bunda Mjini?

Supplementary Question 2

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Mji wa Vwawa ni moja ya miji ambayo iko kwenye hii Miradi ya TACTIC Awamu ya Tatu. Je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza mradi huo katika Mji wa Vwawa? Ahsante sana.

Name

Kwagilwa Reuben Nhamanilo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Handeni Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Mji wa Vwawa ni miongoni mwa miji 18 ambayo tunakwenda kutekeleza huu Mradi wa TACTIC. Kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi, tunakwenda kuanza utekelezaji wa mradi huu mara baada ya shughuli hizi za usanifu kukamilika. (Makofi)

Name

Esther Nicholas Matiko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tarime Mjini

Primary Question

MHE. ESTER A. BULAYA aliuliza:- Je, lini Mradi wa TACTIC Awamu ya Tatu utaanza kutekelezwa katika Jimbo la Bunda Mjini?

Supplementary Question 3

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Tarime una Miradi mitatu ya TACTIC, ambayo ni Stendi ya Kimange, barabara za lami ikiwepo Barabara kutoka Lebu – Kebaga mpaka Biyambu, ambayo ni barabara muhimu sana kwa uchumi wa Tarime pamoja na Mradi wa Dampo. Ninataka kujua ni lini sasa miradi hii itaanza na kukamilika kwa manufaa mapana ya wananchi wa Tarime Mji? Ahsante sana. (Makofi)

Name

Kwagilwa Reuben Nhamanilo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Handeni Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Tarime ni miongoni mwa miji inayokua kwa haraka. Nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna anavyoupambania huu Mji wa Tarime; tupo katika mpango wetu wa kutekeleza huu Mradi wa TACTIC Awamu ya Tatu na ngazi ya usanifu wa dhana, pamoja na usanifu wa awali tuko mwishoni kuukamilisha. Tutakwenda kutangaza zabuni, kuanza ujenzi mara moja. (Makofi)