Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Issa Ally Mchungahela
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lulindi
Primary Question
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA aliuliza:- Je, nini hatma ya Mradi wa TASAF nchini?
Supplementary Question 1
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri, lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Serikali iliahidi kutumia taarifa za TASAF katika utekelezaji wa awali wa bima ya afya kwa wote kwa maana ya pilot study. Je, ni nini kimefanyika mpaka hivi sasa?
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na tabia ya kuwaondoa watu kwenye utaratibu wa TASAF kwa kisingizio cha kuhitimu kwa maana ya ku-graduate ilihali bado wangali maskini wa kutupwa. Je, Serikali haioni sababu ya kuiondoa dhana hii ya uhitimu ili kuwaondolea adha maskini hawa? (Makofi)
Name
Regina Ndege Qwaray
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi 2022 imetambulika kaya zaidi ya 3,900,000 ambao wako katika kaya maskini. Katika kaya hizo, kaya 931,000 zimetambulika na tayari zimewekwa katika kanzidata. Kwa sasa kaya 276,000 zinawekwa katika mpango wa awamu ya kwanza ya utekelezaji wa bima ya afya kwa wote wakati Serikali inaendelea kuchambua na kuendelea kutambua hizo kaya maskini ambazo tayari zinatakiwa ziingie katika utekelezaji wa bima ya afya kwa wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye swali lake la pili kuhusu walengwa kuhitimu, Serikali imeendelea kutoa ruzuku ya fedha kama chachu ya kuimarisha uchumi katika kaya maskini. Hata hivyo, katika utekelezaji wa mpango wa pili (PSSN2) Serikali imeendelea kusisitiza na kuwapa nguvu walengwa wa kaya maskini waweze kujitegemea kiuchumi. Hela zinavyotolewa ni kuwezesha zile kaya ziweze kusimama na kuweza kujitegemea kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo Serikali imeendelea kuwawezesha na kuwaunganisha katika fursa mbalimbali walengwa ambao wako katika mpango ili waweze kujitegemea kwa kuwaunganisha na fursa kama mikopo ya halmashauri lakini kuwapa elimu ya ujasiriamali, pamoja na kuwapa rasilimali za uzalishaji kwa ajili ya kwenda kujitegemea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kuhitimu Serikali imekuwa ikifanya tathmini ya kina ili kuona kama zile kaya zina uwezo sasa wa kusimama zenyewe na zimeimarika kiuchumi. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved