Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Nape Moses Nnauye
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtama
Primary Question
MHE. NAPE M. NNAUYE aliuliza:- Je, Serikali haioni haja ya kuanza upembuzi wa ujenzi wa reli ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Kusini kufuatia maandalizi ya Mradi wa LNG?
Supplementary Question 1
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu haya ya Serikali, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kama Serikali ilivyokiri, kwamba mradi huu ni wa muhimu, lakini ni wa muhimu kwa nchi yetu kuliko ilivyo wa muhimu kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki, ikiwemo kuongeza thamani na utekelezaji wa haraka wa Mradi wa LNG wa Lindi ambao ni mradi mkubwa kuliko yote katika historia ya nchi yetu. Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuuchukuwa mradi huu kutoka kwenye miradi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuufanya mradi wa Serikali yetu ili tuutekeleze utupe advantage kwa nchi za Afrika Mashariki?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, Serikali ipo tayari kushirikiana na wabia wanaotekeleza Mradi wa LNG wa Gesi wa Lindi katika kutafuta rasilimali za ujenzi wa reli hii kwa sababu nao ni wanufaika wakubwa wa kusafirisha mizigo na wananchi watakaokwenda kutekeleza mradi huu wa gesi?
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Nape Nnauye kwa swali lake la msingi na maswali ya nyongeza ambayo ameyaongezea. Ninakubaliana naye kwamba mradi huu ni muhimu kwa uchumi wa Taifa letu. Serikali ilipoamua kuuingiza kwenye Master Plan ya East Africa msingi wake ni nini? Ni kutaka uingizwe katika vipaumbele vya Kanda ya Afrika Mashariki; lakini mbili ni kutaka tushirikiane katika utafutaji wa pamoja wa rasilimali fedha kwa miradi yote iliyopo katika kanda hii; na tatu ni kutaka mradi huu usomane na miradi mingine inayotekelezwa katika jumuiya hii; kwa hiyo ndiyo hoja ya kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na kwamba ni muhimu na kwamba tuiingize kwenye kipaumbele chetu, hilo tumelipokea na tunakubali kwamba ni muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili ambapo kimsingi ni dhana ya PPP; kwamba je, Serikali haioni sasa ni muhimu kushirikiana na wawezekaji wanaofanya Mradi wa LNG. Pengine labda uniruhusu niseme kwa ufupi sana kuhusu concept ya PPP.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali zote duniani zinatambua na kuthamini mchango wa sekta binafsi katika kukuza uchumi wa mataifa yao; na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameendelea kuweka mazingira mazuri na rahisi ili wawekezaji, ama sekta binafsi iweze kunawiri na kustawi katika nchi yetu ili ishiriki katika kujenga uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, kwenye upande wa reli ukitazama miradi ambayo inatekelezwa, ukiangalia kuanzia kipindi cha uhuru mpaka miaka 2020 tulikuwa na reli ya mita gauge ambayo ni kama 2700 pamoja na TAZARA ambayo ni kilomita kama 975, ukijumlisha kwa pamoja ni kilomita 3,600. Mipango ya Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake ni nini? Ni kujenga reli ya SGR peke yake yenye urefu takriban 4,700. Tayari hivi ninavyozungumza miradi yenye urefu wa kilometa 2,100 imekwishaanza kutekelezwa; na ipo kwenye mpango wa kujenga reli ya kusini kilomita 1,000 kaskazini, kilometa 1,000 pamoja na reli ya mjini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukichukua miradi hii peke yake fedha inayohitajika kwa ujenzi ni matrilioni. Hapo ndipo unakubali kwamba ni lazima uzishirikishe sekta binafsi katika kujenga miundombinu hiyo. Ukishamaliza kuijenga bado utahitaji vitendea kazi, vichwa na mabehewa. Ndiyo maana kwa kutambua hilo sekta ya uchukuzi kama Serikali ilibadilisha Sheria Namba 10 ya Mwaka 2017 ili kuruhusu sekta binafsi kuingia katika ujenzi wa miundombinu ya reli.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, nimhakikishie Mheshimiwa Nape Nnauye pamoja na Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali inatambua umuhimu huo na kwa kweli inakaribisha wadau wote, wale wa LNG pamoja na wadau wengine waje tushirikiane kujenga uchumi. Hii ni kwa sababu tulipoanza kujaribisha tumeona faida yake. Kule TAZARA kama tunavyofahamu tuliporuhusu open access, yaani watu walete mabehewa na vichwa vyao, takriban nusu ya mzigo imeongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kule Bandarini vilevile tuliporuhusu sekta binafsi washiriki katika ujenzi wa nchi yetu tumeona meli zimeongezeka kutoka 4,200 zipo 4,800, mzigo umeongezeka kutoka tani milioni 17 zilizokuwepo mwaka 2020 leo zipo tani milioni 32. Kwa hiyo sekta binafsi ni muhimu sana na Serikali inawakaribisha katika kushiriki kwenye nchi yetu.
Name
Jonas William Mbunda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbinga Mjini
Primary Question
MHE. NAPE M. NNAUYE aliuliza:- Je, Serikali haioni haja ya kuanza upembuzi wa ujenzi wa reli ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Kusini kufuatia maandalizi ya Mradi wa LNG?
Supplementary Question 2
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay, lakini pia kuna usafirishaji mkubwa wa makaa ya mawe kutoka Nyasa na Mbinga kwenda Mtwara; lakini pia tunategemea Mradi mkubwa wa Liganga na Mchuchuma. Katika majibu ya msingi ya Naibu Waziri amesema kwamba upembuzi yakinifu wa kutekeleza Mradi wa Ujenzi wa SGR kutoka Mtwara kwenda Mbamba Bay umeanza kutekelezwa. Je, itachukua muda gani kukamilisha upembuzi yakinifu na mradi huo ukaanza kutekelezwa?
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninafahamu swali hili linagusa takriban Wabunge wote wa Kusini; na pengine wangesimama kutaka kuuliza reli ya kusini itaanza kutekelezwa lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nitoe maelezo kwa ufupi sana. Serikali inatambua umuhimu wa reli ya kusini, kwanza kama kiunganishi cha Bandari ya Mbamba Bay na Bandari ya Mtwara, kwa sababu hizi mbili zikiungana unarahisisha usafirishaji; na nini kimekifanyika?
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hatua za awali Serikali imekwishaanza kujenga Bandari ya Kisiwa Mgao pale Mtwara bandari ya pili ambayo itakuwa maalum kwa ajili ya kusafirisha dirty cargo; yaani cement, makaa ya mawe na kadhalika; zaidi ya bilioni 435 zimeelekezwa pale. Pia ujenzi wa bandari ya Mbamba Bay ambao utagharimu zaidi ya bilioni 70, ni hatua muhimu kuelekea kwenye jambo hilo. Tatu, fidia imelipwa kule Ludewa kwa wananchi waliopo kwenye maeneo ya Liganga na Mchuchuma, hiyo ni hatua pia. Nne sasa, tumekwishafanya usanifu. Kama nilivyosema, tunatafuta wawekezaji binafsi ambao tutashirikiana nao ili tuanze kujenga. Ninatoa rai tena kwa watu wote wa ndani na nje ya nchi ambao wapo tayari kushirikiana na Serikali, twendeni tukajenge reli hii ambayo ni muhimu sana kwa uchumi wa Taifa letu.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved