Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Janeth Elias Mahawanga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza:- Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha wanawake wajasiriamali wanashiriki moja kwa moja kwenye utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050?

Supplementary Question 1

MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa majibu mzuri ya Serikali, lakini nilikuwa na maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; ni kwa namna gani elimu na mafunzo yanayotolewa kwa wanawake wajasiriamali yanakidhi mahitaji ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Serikali inahakikishaje majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi yanakuwa siyo miradi ya muda mfupi, lakini yanakuwa endelevu ili kukidhi na kufikia malengo ya Dira ya Taifa 2050? (Makofi)

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Janeth Mahawanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipende kumpongeza sana Mheshimiwa Janeth amekuwa mstari wa mbele sana kuhakikisha vikundi na majukwaa mbalimbali yanaweza kufanya kazi kwa usahihi. Kwa Mkoa wake wa Dar es Salaam amekuwa akifanya mara nyingi na amenishirikisha hata hapo nyuma kwa kweli anafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namna gani elimu na mafunzo yanatolewa na Serikali kuendana na uhitaji wa Dira 2050, hakika sisi kama Wizara tunapaswa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais ametupa nguzo ya kuona kwamba tunahakikisha kwenye Dira ya Taifa, ile nguzo ya kwanza, uwezeshaji wa wanawake na wanaume kiuchumi tunaisimamia vizuri. Katika hili tunafanya mafunzo mbalimbali na tunashirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI kuona kwamba mafunzo haya yanakamilika. Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI inaingia kwa sababu Waheshimiwa ma-DC na ma-RC ndiyo walezi wa haya majukwaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kule elimu inapatikana kupitia Maafisa Maendeleo ya jamii wetu katika halmashauri. Vilevile, tayari tuna jukwaa ambalo la kidijiti. Mheshimiwa Waziri Dorothy Gwajima anaendesha mikutano mitandaoni na wiki iliyopita tayari tumeweza kuzindua Sekretarieti ya Taifa ya majukwaa haya. Lengo ni kuona kwamba tunashirikiana sasa na hawa Sekretarieti kuona elimu sahihi inaendelea kuwafikia wengi na kuhakikisha mahitaji ya dira yanaweza kutimia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inachukuliaje majukwaa haya katika uendelevu wake. Sisi kama Wizara tumejipanga kikamilifu kuandaa mwongozo ambao unaelezea namna ya uundwaji wa haya majukwaa, lakini vilevile uendeshaji wake. Majukwaa haya yanajengwa na vikundi na vikundi hivi viko pale halmashauri. Maafisa maendeleo ndiyo wetu wa jamii wanavisimamia kuhakikisha vinaweza kuendana na mwongozo uliopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, uendelevu unakuwepo wa uhakika kwa sababu taratibu na namna ambavyo tumeweka katika mwongozo inavibeba hivi vikundi na inakuwa na manufaa zaidi kwa sababu, kwenye kikundi wanakutana wanawake wenye elimu mbalimbali: mwingine ni mzuri katika kuongea; mwingine ni mzuri katika kutafuta masoko; na mwingine ni mzuri katika kuona uboreshaji wa bidhaa aliyonayo. Kwa hiyo, pale kwenye vikundi kwa umoja wao, wanakwenda kuona kwamba sasa wanasogezana mbele na uendelevu unakuwa wa uhakika. Ahsante.