Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Subira Khamis Mgalu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SUBIRA K. MGALU K.n.y. MHE. HAMOUD A. JUMAA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kupandisha hadhi Mji Mdogo wa Mlandizi kuwa Mji kamili?
Supplementary Question 1
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza ninaishukuru sana Serikali kwa majibu mazuri ya kuleta matumaini.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kwa kuwa, hii Halmashauri ya Kibaha kwa vigezo imekuwa na vigezo vingi ikiwemo idadi kubwa ya watu imefika 123,000, ikiwemo Serikali kujenga Mji wa Viwanda, maono ya Rais, Kibaha Vijijini, Mji wa Kwala. Je, Serikali ipo tayari yenyewe kuona namna gani ya kuenzi maono ya Mheshimiwa Rais kutokana na Mji wa Kwala na kuupandisha hadhi Halmashauri ya Kibaha Vijijini kuwa Mji? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Serikali yetu imeitangaza Halmashauri ya Bagamoyo kuwa Halmashauri ya Mji na tunashukuru sana hatua mbalimbali zimekamilika na tangazo la Serikali limetoka. Je, ni lini sasa Serikali itaanza mchakato wa kuhakikisha hadhi ya Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo kutoka kwenye Vitongoji kwenda kwenye Mitaa na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utafanyika. Ahsante sana. (Makofi)
Name
Kwagilwa Reuben Nhamanilo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Handeni Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Spika, sheria yetu pamoja na Mwongozo wa Uanzishwaji wa Mamlaka za Kiutawala wa Mwaka 2014 umeweka vigezo vingi lakini vigezo vikubwa ni vitatu.
Mheshimiwa Spika, kigezo cha kwanza ni kigezo cha uwezo wa kujiendesha kwa kutumia mapato ya ndani, hapa tumeweka uwiano Halmashauri Mama inapotenganishwa na kuanzisha Halmashauri mpya ya Mji, ile Halmashauri mpya ya Mji inatakiwa iwe na uwezo wa kujiendesha kwa mapato ya ndani kwa 30% na ile Halmashauri mama inayobaki inatakiwa iwe na uwezo wa kujiendesha kwa kutumia mapato ya ndani kwa 20% na hivyo kufanya hitajio la kujitegemea kwa 50%.
Mheshimiwa Spika, kigezo cha pili ambacho ni kikubwa na kimewekwa ni kigezo cha idadi ya watu na hii ni kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi, lipo hitajio kwamba Halmashauri mpya inayoanzishwa kwa maana ya Halmashauri ya Mji iwe na idadi ya watu wasiopungua 150,000 na ile inayobaki kwa maana ya Halmashauri mama inatakiwa iwe na watu 250,000.
Mheshimiwa Spika, lipo hitajio la tatu ambalo ni la muhimu zaidi katika yale mengi yaliyopo, ni angalau kwenye ile Halmashauri ya Mji tunayoanzisha iwe na watu 30% wanaojishughulisha na shughuli ambazo siyo za kilimo. Kwa hiyo, nirudie tena kuwaelekeza Halmashauri ya Kibaha wapitie vigezo hivi, wapitie sheria zetu na kama wanakidhi vigezo hivi waendelee na mchakato huo nasi TAMISEMI tutakuwa tunasubiria kwa ajili ya kutekeleza wajibu wetu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Bagamoyo ni kweli tumeitangaza kwa maana ya kuwa gazetted Bagamoyo kuwa Halmashauri na sisi ndani ya Serikali mchakato haujasimama kama ambavyo tumeendelea tumetangaza, sasa tunaendelea na mambo ya kibajeti na mipango ya nchi yetu ili tuweze kuendelea kwenye hatua iliyobaki. (Makofi)
Name
Ado Shaibu Ado
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Tunduru Kaskazini
Primary Question
MHE. SUBIRA K. MGALU K.n.y. MHE. HAMOUD A. JUMAA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kupandisha hadhi Mji Mdogo wa Mlandizi kuwa Mji kamili?
Supplementary Question 2
MHE. ADO S. ADO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona ili niulize swali dogo la nyongeza. Mbunge wa Tunduru Kusini Mhandisi Fadhili Chilombe, ninafahamu kwamba ameleta hoja na kufuatilia mara nyingi Wizara ya TAMISEMI juu ya haja ya kuigawanya Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kupata Halmashauri mbili na mchakato wetu ulifika mpaka RCC, tuna watu zaidi 400,000 na tuna kilometa za mraba 18,000.
Mheshimiwa Spika, tunataka kauli ya TAMISEMI ili Watanzania wanaoishi Tunduru wapate kauli ya Serikali ndani ya Bunge. (Makofi)
Name
Kwagilwa Reuben Nhamanilo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Handeni Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kujibu kwenye jibu la msingi, uanzishwaji wa mamlaka za kiutawala ikiwemo hili analoliongelea Mheshimiwa Mbunge, Ado Shaibu, Mwenyekiti wetu wa Kamati ya LAAC unazingatia Sheria ile ya Uanzishwaji ya Mamlaka za Wilaya, Sura Na. 287 pamoja na Sheria ya Uanzishwaji wa Mamlaka za Miji, Sura 288.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimetoa maelekezo na ushauri kwa Halmashauri ya Kibaha, vivyo hivyo wananchi wa Tunduru wafuate utaratibu huo na TAMISEMI kazi yetu ni moja tu kufanya tathmini na mapitio kama vigezo vimezingatiwa. (Makofi)
Name
Patali Shida Patali
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbeya Vijijini
Primary Question
MHE. SUBIRA K. MGALU K.n.y. MHE. HAMOUD A. JUMAA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kupandisha hadhi Mji Mdogo wa Mlandizi kuwa Mji kamili?
Supplementary Question 3
MHE. PATALI S. PATALI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii nami nipate kuuliza swali la nyongeza kutoka kwenye swali la msingi Na. 138. Je, ni lini Serikali itaupandisha hadhi Mji Mdogo wa Mbalizi kuwa Mamlaka ya Mji kamili, ikizingatiwa mji huu umekidhi vigezo vyote ikiwepo idadi ya watu, uwezo wa kujiendesha wenyewe? Pia mji huu umeomba kupandishwa hadhi muda mrefu sana?
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kwa niaba ya Wanambeya Vijijini nipate majibu ya Serikali. Ahsante sana. (Makofi)
Name
Kwagilwa Reuben Nhamanilo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Handeni Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Spika, ninawaelekeza uongozi wa Mkoa, husika wakamilishe michakato yote ambayo imeainishwa kisheria, ikiwa ni pamoja na kuanza mijadala kwenye ngazi ya Mitaa na Kata, Wilaya kwenye vikao vya RCC, vikao vya DCC. Watakapokamilisha wawasilishe TAMISEMI kama utaratibu unavyotaka, TAMISEMI tutatuma timu na tutafanya mapitio ya vigezo hivyo na kama vigezo vitakidhi, mamlaka itachukua hatua zinazofuata. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved