Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Neema Peter Majule

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Mfumo madhubuti wa kupima matokeo ya mikopo 10% ya Halmashauri ili kubaini changamoto na mafanikio?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ya kwamba tathmini ilifanyika na bado kuna maboresho yamefanyika, lakini bado kumekuwa na malalamiko makubwa kwa wanawake wa Dodoma Vijijini kwamba mikopo hii haiwafikii na pia kumekuwa na mchakato mrefu sana wa upatikanaji wa mikopo hiyo. Je, ni lini Serikali itakuwa na njia mbadala kwa ajili ya wanawake wa vijijini kupata mikopo sawa na wanawake wa mijini ambao wapo karibu na hizo fursa?

Mheshimiwa Spika, lingine pia kumekuwa na huo mchakato mrefu...

SPIKA: Mheshimiwa hujauliza maswali mawili?

MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Spika, hili ni swali la pili la nyongeza.

SPIKA: Sawa, endelea.

MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Spika, kumekuwa na mchakato mrefu wa upatikanaji wa huduma hii ya mikopo, kwamba, wanawake wengine wamekata tamaa kabla hawajafikia kupata mikopo. Swali, je, ni lini Serikali itakuja sasa na one stop centre ambapo mwanamke huyu akienda atakuta na atapata pale pale katiba, cheti, tax clearance, service levy na huo mkopo ili kunusuru wanawake kukata tamaa ku-process mkopo huu?

Name

Kwagilwa Reuben Nhamanilo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Handeni Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Spika, ninaomba niyajibu maswali yote mawili kwa pamoja kwa sababu yanaingiliana.

Mheshimiwa Spika, wote tutakumbuka kwamba mara baada ya kuanzisha utoaji wa mikopo awamu mpya, kwa maana ya baada ya kuachana na utaratibu wa zamani, Serikali ilizigawa halmashauri zetu katika makundi mawili. Kundi la kwanza likiwa na halmashauri 174 na kundi la pili, ikiwemo Dodoma, likiwa na halmashauri 10. Halmashauri 174 tumeendelea kutoa mikopo kupitia utaratibu ulioboreshwa, lakini halmashauri hizi 10 pia tulisema tutoe mikopo kupitia benki ili tuweze kuona kama tutafanikiwa, kama ambavyo Mheshimiwa Rais alikuwa ametamani ifanyike, hatimaye tuweze kufanya utaratibu wote utumike kwa nchi nzima.
Mheshimiwa Spika, sasa katika mikoa 10, maeneo 10 ambayo tulipanga kufanya kupitia benki ni pamoja na Jiji la Dar es Salaam, kwa maana ya Mkoa mzima wa Dar es Salaam, Dodoma, Songea Manispaa, Newala, Bumbuli, Siha, Mbulu pamoja na Itilima na Nkasi; huku kote tumeendelea kutoa kupitia utaratibu wa benki.

Mheshimiwa Spika, wiki mbili zilizopita tumekaa na benki hizi tatu ambazo tulikuwa tumezipa kazi hii; Benki za CRDB, NMB na Uchumi Commercial Bank; kwa ajili ya kufanya tathmini na kuona maeneo ambayo yamekuwa kikwazo kwa watu wetu.

Mheshimiwa Spika, msisitizo wetu na namna ambayo tumekubaliana na maelekezo ambayo tumepeana ni kwamba, mabenki ni sharti yazingatie kwamba wananchi ambao tunataka wakopeshwe mikopo hii, ni wananchi ambao hawawezi kukidhi masharti ya kibenki. Ndiyo maana tumesaini MoU ya kuhakikisha kuwa wanapewa kwa mazingira hayo hayo waliyonayo. Mheshimiwa Rais anataka watu wote wapate mikopo, hata wasiokopesheka kwenye benki. Kwa hiyo nisisitize tena kwamba tutayasimamia haya ili kuhakikisha hakuna ucheleweshwaji wa utoaji wa mikopo.

Mheshimiwa Spika, jana tumejibu swali hapa na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI amelitolea maelezo marefu na ya kina, kwamba Maafisa Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na TAMISEMI wamewezeshwa. Kwanza pikipiki zaidi ya 98 ili waweze kuwafikia wananchi wetu kwenye vikundi vyao mahali walipo; na pia Serikali kupitia TAMISEMI tumekuwa tukitenga fedha kwenye OC zetu. Kila tunapopeleka OC tunapeleka na fungu kwa ajili ya Mafisa Maendeleo ya Jamii kuweza kuwafikia watu wetu. Niwaelekeze mikoa yote kupitia ma-RAS wetu wahakikishe kuwa hapawi na usumbufu wote kwa wananchi kupatiwa mikopo hii.

Name

Bakari Bakari Shingo

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Ukonga

Primary Question

MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Mfumo madhubuti wa kupima matokeo ya mikopo 10% ya Halmashauri ili kubaini changamoto na mafanikio?

Supplementary Question 2

MHE. BAKARI B. SHINGO: Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi hii na nina swali dogo la nyongeza. Katika Jimbo langu la Ukonga, hasa Halmashauri yetu Jiji la Dar es Salaam moja ya mambo yaliyopelekea halmashauri ikahamisha utaratibu wa kukopesha moja kwa moja ni baadhi ya watumishi wa halmashauri na baadhi ya Madiwani walisemwa kwamba wamekuwa wakitumia mlango wa nyuma kujikopesha, lakini pia kuwepo na vikundi ambavyo sasa vimekopeshwa zaidi ya mamilioni na vimetajwa kuwa havionekani.

Mheshimiwa Spika, swali langu ni kuwa; je, kwa ajili ya kulinda maslahi mapana ya Taifa na kodi zetu, ni kwa nini Serikali isiweke utaratibu wa kuyataja hadharani hayo makundi ama hivyo vikundi vilivyokopa ambavyo sasa havionekani, sambamba na baadhi ya watumishi wa halmashauri ambao siyo waaminifu waolijingiza katika mtego huu ambao leo unapelekea halmashauri zetu kuhamisha Mfuko huo kupeleka kwenye benki, benki ambazo zinasababisha tushindwe kupata mikopo?

Name

Riziki Silas Shemdoe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lushoto

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ambayo Naibu wangu ameyatoa, kama alivyosema, tulikuwa na kikao na benki hizi. Kilichotokea ni kwamba, kweli kwenye majiji kuna fedha nyingi ambazo hazijakopeshwa uki-compare na kwenye halmashauri za wilaya na miji. Shida iliyopo, kutokana na maelezo waliyotupa benki; la kwanza, ni kweli kwamba walikuwa na masharti magumu, lakini kwa sasa sharti linalotakiwa kwa mtu kwa kikundi kukopa ni wale wanakikundi kuwa na NIDA.
Mheshimiwa Spika, nini kimesababisha sasa majiji yawe na fedha nyingi; wamesema, ni kwa sababu wale wanaounda vikundi walioko Dar es Salaam kwa mfano wanakutana kimjini mjini, kwa hiyo hawawezi na inakuwa ngumu sana kupata kikundi kimoja cha watu ambao wanaweza kukopeshwa kwa wakati huo. Hii ni kwa sababu, huyu ametoka Segerea, mwingine ametoka Ubungo, mwingine tena ametoka Kawe na wanakutana Kariakoo kwenye biashara. Wakiwa pale kila mtu hajui huyo mwenzake ametokea wapi.

Mheshimiwa Spika, proposal ya benki ni kwamba, ikiwezekana tuwape mikopo individuals kama tunavyofanya kwa walemavu; lakini tuwe na condition moja kwamba huyu individual tunayempa mkopo atuhakikishie kwamba kwanza ana biashara, ana leseni ya biashara; lakini pili, ataweza ku-employ angalau watu watatu kwenye ile biashara kutokana na mkopo tunaowapa.

Mheshimiwa Spika, kama hii itafanyika, kitu cha kwanza zile bilioni zilizolala kule benki zitatoka. Kitu cha pili, tutaona kwamba tume-create ajira kwa vijana ambao ni moja ya vitu ambavyo tunaviangalia sana kwenye fedha hii. Kwa hiyo Bunge lako hili ninaomba lielewe kwamba, tutakwenda kuona namna ya kubadilisha ule mwongozo na kukubali kwamba tuwe na pilot ya majiji ya kutoa mikopo kwa individuals ambao watatuhakikishia kwamba wata-create ajira kwenye maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, nimeomba nisimame nitoe ufafanuzi huu na kushukuru sana.