Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mattar Ali Salum

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shaurimoyo

Primary Question

MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza:- Je, Serikali haioni haja ya kuongeza wigo wa fedha za mazingira ili kusaidia juhudi za Zanzibar kukabiliana na athari hizo?

Supplementary Question 1

MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini kwanza nichukue fursa ya kumpongeza sana Mheshimiwa Engineer Masauni kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa. Hili ni jambo jema kwa nchi yetu na ni fursa kwa nchi yetu, lakini Mheshimiwa Waziri Serikali yetu itafaidika vipi na fursa za kifedha katika taasisi hiyo? Ahsante sana. (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Mattar Ali Salumu, Mbunge wa Shaurimoyo kwa kuwa mdau mzuri wa mazingira na kwa kuwasemea wananchi wa Jimbo la Shaurimoyo Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, ninaomba nimhakikishie Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinao mkakati mahususi wa kuongeza fedha za mazingira kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunahifadhi na kutunza mazingira yetu kwa sababu tunafahamu mazingira ni uhai na hivi sasa katika Mpango wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025/2050 suala la mazingira limepewa nguzo mahususi na Serikali ya Zanzibar pamoja na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tutaendelea kuhakikisha kwamba tunaongeza vyanzo na kutunza mazingira. Ahsante sana.

Name

Zacharia Paulo Issaay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Primary Question

MHE. MATTAR ALI SALUM aliuliza:- Je, Serikali haioni haja ya kuongeza wigo wa fedha za mazingira ili kusaidia juhudi za Zanzibar kukabiliana na athari hizo?

Supplementary Question 2

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru. Kwa kuwa ni miaka mitatu sasa taarifa ya Wizara ya Mazingira na Wizara zingine mtambuka kuhusu Maziwa ya Babati, Basutu, Tlawi kule Mbulu na Mkoa wa Manyara kwa ujumla haijarudishwa na kazi haijafanyika; je, ni lini Waziri atakwenda Mbulu kutembelea hayo Maziwa? (Makofi)

Name

Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa nafasi hii. Ninaomba kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ya maswali yote mawili ya Waheshimiwa Wabunge. Vilevile, nimshukuru Mheshimiwa Mattar na Mheshimiwa Spika wewe pia, pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunipongeza jana na leo kwa kuweza kuchaguliwa kwenye nafasi ya Makamu wa Rais wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa.

Mheshimiwa Spika, ninaomba niongezee sasa kujibu maswali ya Waheshimiwa Wabunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza ni dhahiri kabisa nafasi hii ambayo tumeipata inachangiwa na kazi kubwa na mafanikio makubwa na heshima kubwa ambayo Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan na nchi yetu iliyojenga katika Jumuiya ya Kimataifa ndiyo ikawezesha kuweza kupata heshima hii ya kuweza kupata nafasi hiyo.

Mheshimiwa Spika, kupitia nafasi hiyo tunaweza kunufaika katika masuala mengi; moja ni kuhakikisha kwamba tunapenyeza vipaumbele vyetu kama Taifa katika kukabiliana na changamoto za mazingira ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, upotevu wa Bioanuwai, masuala mengine mbalimbali yanayohusu ikiwemo nishati safi na kadhalika. Hiyo pia itatusaidia kuweza kunufaika na fedha mbalimbali (fursa za kifedha) kupitia Mifuko ya Mazingira kwenye Jumuiya ya Kimataifa.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge wa Mbulu aliuliza swali la Ziwa Babati. Ninataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba yeye pamoja na Mheshimiwa Mbunge wa Babati Mjini tulizungumza nao kuhusiana na jambo hilo. Hivi sasa ninavyozungumza leo kuna timu ya wataalam imekwenda kule Babati kufanya tathmini ili kuhakikisha kwamba tunafanya nini kwa kupata hatua za dharura za kuweza kukabiliana na tatizo hilo.

Mheshimiwa Spika, wakati huo huo, Serikali ina mkakati wa muda mrefu ikiwemo kununua mitambo ya kukabiliana na changamoto ya magugu maji katika maeneo yote yaliyoathirika na magugu maji katika nchi yetu. Kwa hiyo, hatua za kwanza za dharura tayari tumeanza nazo leo, lakini baada ya muda siyo mrefu tayari tutapata fedha kupitia Serikali Kuu (kupitia Hazina) ili tuweze kupata mitambo ya kukabiliana na tatizo hilo.

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana.