Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Azza Hilal Hamad

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. AZZA H. HAMAD aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuunganisha Barabara ya lami ya Kahama – Njiapanda ya Lohumbo, Mji Mdogo wa Didia?

Supplementary Question 1

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Ninamshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri kwa wananchi wangu wa Jimbo la Itwangi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kuwa, Barabara ya kipande hiki kidogo cha Njiapanda ya Lohumbo kwenda center kubwa ya Didia ni barabara muhimu sana kwa wananchi wa Jimbo la Itwangi na kwa halmashauri kwa ujumla, ukizingatia Mji Mdogo wa Didia unakuwa kwa kasi kwa biashara ya mchele na biashara nyingine, lakini Serikali imewekeza fedha nyingi kwa ujenzi wa reli ya mwendokasi na kujenga station katika Mji huu Mdogo wa Didia. Je, Serikali ipo tayari sasa kufanya usanifu huu haraka iwezekanavyo, ili kuupa hadhi Mji Mdogo wa Didia na kuipa hadhi Station ya Reli ya SGR? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari sasa kuongozana na mimi kwenda kuona hali halisi ya Mji wa Didia jinsi ulivyo, unavyokuwa kwa kasi na unavyoingizia halmashauri mapato na kuona changamoto kubwa iliyopo katika barabara hii? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Mheshimiwa Azza Hillal Hamad, amekuwa akifuatilia mara kadhaa kuhusiana na ujenzi wa barabara zake, ikiwemo barabara hii muhimu ya kilometa 4.5. Kwa hakika wananchi wa Itwangi wamempata Mbunge anayefanya kazi kubwa sana kwa ajili yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Jimbo la Itwangi kwamba, Serikali inatambua sana umuhimu wa barabara hii kwa sababu, pale kuna Kituo cha SGR, lakini pia, kuna huduma nyingi za kiuchumi na kijamii ambazo zinaongezeka kila siku. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, timu yetu ya wataalam ipo hatua za mwisho za kukamilisha tathmini. Ninatumia nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, kumwelekeza Meneja wa TARURA Mkoa wa Shinyanga, pamoja na Meneja wa TARURA wa Wilaya, wahakikishe wanasimamia ukamilishaji wa tathmini haraka iwezekanavyo na kuwasilisha Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, kwa ajili ya kutafuta fedha ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa awamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, nipo tayari kuambatana na Mheshimiwa Mbunge kwenda kufanya ziara katika Jimbo la Itwangi tuweze kuona barabara zetu na tuone namna nzuri ya kuboresha miundombinu hiyo. Ahsante sana.

Name

Jafari Wambura Chege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Primary Question

MHE. AZZA H. HAMAD aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuunganisha Barabara ya lami ya Kahama – Njiapanda ya Lohumbo, Mji Mdogo wa Didia?

Supplementary Question 2

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kuniona. Barabara inayotuunganisha kati ya Shirati – Minigo na Kata ya Nyamtinga Rung’enye imeharibika kwa muda mrefu na haipitiki kwa sasa. Ninataka kujua Serikali ina mpango gani juu ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha changarawe, pamoja na makalavati yanayozunguka barabarani?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia Mbunge wa Rorya, Mheshimiwa Wambura Chege kwamba, Serikali hivi sasa inafanya tathmini ya barabara zote zilizokatika kufuatia mafuriko na mvua nyingi. Tutatoa kipaumbele kwenye barabara hiyo katika Jimbo la Rorya, kwanza, kupata taarifa za tathmini na mahitaji ya gharama mapema. Pili, kutenga fedha, kwa ajili ya matengenezo, ili barabara iweze kupitika wakati tunaendelea kupanga mipango ya muda wa kati na muda mrefu, kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami kwa kadiri itakavyoonekana inafaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge ninamhakikishia kwamba, suala hilo tumelichukua, tunalifanyia kazi. Meneja wa TARURA wa Mkoa wa Mara na Wilaya ya Rorya wakamilishe tathmini ya barabara hiyo mapema iwezekanavyo na kuiwasilisha Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI kwa sababu, tupo hatua za mwisho za ku-comply yale mahitaji ya kupeleka fedha, kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizo. Ahsante sana.