Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Lucy Edward Mwakyembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. LUCY E. MWAKYEMBE aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapa ajira vijana wanaojitolea?

Supplementary Question 1

MHE. LUCY E. MWAKYEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninamshukuru Naibu Waziri, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, ndugu yangu, Mheshimiwa Regina Ndege, kwa majibu mazuri ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sera ya Menejimenti na Ajira ya Mwaka 2008, Toleo Namba Mbili pamoja na Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura 298 na Mwongozo wa Kujitolea wa Mwaka 2025. Ninaomba nitoe ushauri, Mwongozo huo wa Mwaka 2025, basi ufike haraka katika Taasisi za Serikali, pamoja na Taasisi za Sekta Binafsi ili watumishi hawa wa kujitolea wanapopata huduma hii iwe katika uwiano katika taasisi tofauti. Ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)

Name

Regina Ndege Qwaray

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Lucy kwa namna anavyoendelea kuwasemea watumishi na vijana wa nchi hii. Ushauri wake tumeupokea. Hata hivyo, ninapenda kulihakikishia Bunge lako kwamba, utaratibu tuliouweka, kama Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ni kwamba, mwongozo tayari umetoka. Hatua iliyobaki ni kuhakikisha mwongozo huo unasambazwa na kufika kwenye taasisi zetu za umma na kwenye idara na Wizara mbalimbali, ili uanze kutumika, kwa ajili ya kuwapata vijana ambao wapo tayari kujitolea katika utumishi wa umma. (Makofi)

Name

Zacharia Paulo Issaay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Primary Question

MHE. LUCY E. MWAKYEMBE aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapa ajira vijana wanaojitolea?

Supplementary Question 2

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Kwa kuwa, idadi hii ya vijana wanaojitolea nchini ni kubwa sana. Je, Serikali haioni kuwa, kuna umuhimu mkubwa sasa wa kufanya takwimu na tafiti, kwa ajili ya idadi ya waliojitolea kwa miaka mitatu hadi sasa, ili Serikali ione namna pekee ya ...

MWENYEKITI: Mheshimiwa Zacharia, zungumza kwa ufanisi akuelewe. Naona Naibu Waziri anapata mashaka na swali lako.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, vijana wengi sasa hivi wanajitolea kwenye shule zetu na tunashindwa kuwaambia wasiendelee kujitolea kutokana na umuhimu wa nafasi walizoshika na masomo wanayofundisha. Serikali haioni kuwa, ni wakati muafaka sasa wa kuchukua takwimu sahihi ya vijana hawa waliyojitolea kwa miaka mitatu, ili iweze kutoa mwongozo sahihi wa namna ya hao vijana watakavyohudumiwa. (Makofi)

Name

Regina Ndege Qwaray

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay. Kama nilivyosema kwamba, utaratibu wa ajira sasa unaenda kwa njia ya ushindani kwa sababu, tumejiwekea sera ambayo inatuongoza namna ya kuwapata watumishi wanaoingia katika ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la nyongeza linaeleza namna ambavyo tunaweza kuwatazama kwa karibu wale vijana ambao wanajitolea kwenye shule zetu; tayari Ofisi ya Utumishi imeanza kuweka mkakati wa kuwafuatilia vijana hawa, ambao wanajitolea, lakini utaratibu upo palepale kwamba, watafuata mwongozo ule wa kujitolea wanapoingia kwenye ajira zile za kujitolea, hasa kwenye shule zetu. Kama nilivyosema, mwongozo huu utaelekezwa kwenye shule, utaelekezwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, kwenye taasisi, kwenye Idara na Wizara zote, ili utumike, kwa ajili ya kuwapata vijana wa kujitolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajira zile za kujitolea ni kuwaandaa vijana wetu waendeleze taaluma walizozipata vyuoni au shuleni, ili wanapokwenda kupambana katika ajira waweze kutumia vizuri ujuzi walioupata. Kwa sababu, wanapopata ile nafasi ya kujitolea inawapa uwanja mpana wa kuelewa field au kada zao, ili waweze kupambana katika ushindani wa ajira. Ahsante.

Name

Khadija Shaaban Taya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. LUCY E. MWAKYEMBE aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapa ajira vijana wanaojitolea?

Supplementary Question 3

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali. Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuajiri wanasaikolojia katika ofisi na idara zote za Serikali, ili kuongeza ufanisi kwa sababu, huenda kutokufanya kazi vizuri kunasababishwa na matatizo ya saikolojia? Ninashukuru.

Name

Regina Ndege Qwaray

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi niweze kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Taya, kama alivyouliza. Ni ukweli usiopingika katika ofisi zetu, katika taasisi zetu, watumishi wengi wanapata changamoto na wakati mwingine inasababisha hata wasifanye kazi vizuri. Ofisi yetu tayari imeona kuna tatizo hilo, tupo kwenye kuandaa mkakati kuhakikisha kwamba, tunapata wataalam ambao watakuwa katika hizo ofisi, ili kutoa huduma za ushauri nasaha au huduma zile za saikoloji, ili kuwasaidia watumishi wetu waweze kutoa huduma vizuri pindi wanapokutana na changamoto.

Name

Thomas Maganga Kampala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katavi

Primary Question

MHE. LUCY E. MWAKYEMBE aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapa ajira vijana wanaojitolea?

Supplementary Question 4

MHE. THOMAS K. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa, Wabunge wengi wanazo takwimu sahihi za watumishi na walimu wanaojitolea kwenye majimbo na halmashauri zetu. Je, Serikali haioni sasa ni wakati sahihi kushirikiana na Wabunge, ili kupata takwimu sahihi za watumishi na walimu wanaojitolea kwenye majimbo yetu? (Makofi)

Name

Regina Ndege Qwaray

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu ya watu wanaojitolea kwa sasa ofisi haijapata takwimu kamili kwa sababu, kwanza watu wamekuwa wakiingiza watumishi kwa namna ambayo, kama nilivyosema kwamba, watu wanapojitolea wakati mwingine wanaingizwa kwa upendeleo na wengine wanaingia kwa kujuana. Serikali imeendelea kupanga mkakati kuhakikisha tuna mwongozo na mfumo ambao utakwenda kufuatilia kwa karibu wale vijana ambao wamepata nafasi ya kujitolea baada ya kutumia mwongozo huu ambao tumeutoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, watumishi watakapoingia kupitia mwongozo huu, Serikali itapata urahisi wa kupata data kamili ya vijana wa kujitolea, lakini pia, mwongozo ule unaeleza masharti na vigezo ambavyo vitatumika, ili watu hawa waweze kujitolea. Kwa hiyo, ushauri wa Mheshimiwa Mbunge tunauchukua, ili kuendelea kupata data kamili kwa kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge.

Name

Edibily Kinyoma Kazala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Vijijini

Primary Question

MHE. LUCY E. MWAKYEMBE aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapa ajira vijana wanaojitolea?

Supplementary Question 5

MHE. EDIBILY K. KINYOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni kumekuwa na wimbi la vijana kufanya interview nyingi na kwenye aptitude test wanapata asilimia za juu mpaka 90%, lakini wanakuwa hawapo selected. Je, Serikali haioni ipo haja ya kuweka cutting point, ili kuepuka vijana kufanya interview 10 hadi 20 na hawapati kazi? Ahsante.

Name

Regina Ndege Qwaray

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wengi wanapokwenda kwenye mitihani ile ya awali, yaani aptitude test, kwanza tunapata waombaji wengi sana ambao ajira ikitangazwa wanajitokeza kuomba ajira hizi. Kwa hiyo, wanapokwenda kwenye usaili wanafanya mtihani wa written, kwenye ule mtihani wa written kunakuwa na alama ambazo zinamfanya yule msailiwa aweze kufikia zile alama na waliofikia zile alama wanachukuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hoja ya Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, wengi wanafaulu na kwa kuwa kiwango ambacho labda Serikali imepanga kwa muda huo ni watu 10,000 na wanaohitajika labda ni watu 5,000 kwa hiyo, cutting point ya alama zile zinazotakiwa lazima itapanda kulingana na wingi wa watu kufaulu kwenda kwenye mtihani wa written. Hii ni kwa sababu, tunazingatia Sheria ya ILO ambayo inatuelekeza kwamba, nafasi moja itashindaniwa na watu watatu.