Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Margaret Simwanza Sitta

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Urambo

Primary Question

MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga uzio wa Uwanja wa Ndege Urambo ili kuutunza vema Uwanja huo na kuwa salama?

Supplementary Question 1

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo yametupa matumaini sisi Wananchi wa Urambo. Ninaomba niulize maswali mawili kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninatanguliza ombi maalum, Mheshimiwa Naibu Waziri alipokuwa akijibu ameeleza wazi kabisa kwamba, Serikali inatambua kwamba ule uwanja ni muhimu na ni wa kihistoria na kwamba tayari wameshauweka katika mpango wa maendeleo, tunaishukuru sana Serikali kwa kutambua hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sasa kwa niaba ya wananchi wa Urambo ujenzi wa uzio wa Uwanja wa Ndege wa Urambo uwekwe katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2026/2027.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa uwanja wa ndege wa Urambo upo kati kati ya mji na kwa msingi huo unachangia mwonekano wa mji. Je, Serikali ipo tayari kuweka utaratibu maalum wa usafi wa uwanja na ulinzi?

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Margaret Sitta kwa maswali yake mawili ya nyongeza ambayo kimsingi hoja yake ya kwanza ni ombi. Ninapenda kupokea kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi kwamba ombi lake limepokelewa, tutalichakata. Na kwa kuwa tumelipa msukumo mkubwa ninaamini tutakuwa kwenye hatua nzuri ya kwenda kulifanyia kazi kama ambavyo tumesema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu jambo lake la pili, amesisitiza kuhusiana na mwonekano wa uwanja. Huu ni uwanja wa kihistoria kama nilivyosema na mama yetu Mama Sitta ni mmoja kati ya watu ambao wanapigania sana uwanja wa Urambo pamoja na uwanja wa Tabora na maendeleo ya jimbo lake kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe, tumeshaweka utaratibu hivi ninavyozungumza, pengine nitumie nafasi hii kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wetu wa Uchukuzi kuwaelekeza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania kuweka mkakati maalum wa kuhakikisha kwamba tunapata watoa huduma watakaoweza kuimarisha ulinzi na usalama na usafi katika eneo hili ili hoja ambayo anaipigania mara kwa mara iweze hatimaye kufuatiliwa.