Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Timida Mpoki Fyandomo
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. TIMIDA M. FYANDOMO K.n.y. MHE. JOHN J. NCHIMBI aliuliza: - Je, lini Serikali itatoa mikopo nafuu ya Boti za Uvuvi za Fiber kwa Wavuvi wa Wilaya ya Nyasa?
Supplementary Question 1
MHE. TIMIDA M. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya Mheshimiwa John John Nchimbi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na taarifa nyingi kuwa vizimba vya samaki havijengeki Ziwa Nyasa. Swali la kwanza; je, Serikali ipo tayari kupeleka watafiti kwa ajili ya kuchunguza namna ya kufanya ili vizimba hivyo viweze kujengeka?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, Serikali ipo tayari kuwajengea uwezo vijana wa Wilaya ya Kyela wa kuwahusisha katika minyororo ya thamani ya uvuvi ili kupunguza ukosefu wa ajira kwa vijana katika eneo hilo, lakini pia kuwapa mikopo ya asilimia fulani ya kuweza kupata boti za fibre?
Name
Ng'wasi Damas Kamani
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Timida Fyandomo kwa sababu tangu ameingia Bungeni hapa amekuwa akijitahidi sana kuhakikisha kuwa hoja za vijana zinasikika na sisi Serikali tunazipokea na kuzifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza linahusiana na utafiti juu ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ziwa Nyasa. Ninaomba nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba ufugaji wa vizimba kwetu sisi Wizara lengo letu ni kuhakikisha kwamba unafanyika katika maziwa yote makuu nchini, lakini na maziwa madogo. Kwa hiyo kwa yale maziwa ambayo bado tunayafanyia tafiti au bado tupo katika taratibu za kuyafanyia tafiti tunaendelea kuhakikisha tunatenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha pia huko tunaweka ufugaji wa samaki kwa vizimba ikiwemo Ziwa Nyasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimtoe wasiwasi, tayari tumeanza utaratibu wa kuhakikisha tunafanya tafiti za kutosha ili kuona namna gani tunaweza tukauanzisha ufugaji huu katika Ziwa letu Nyasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la pili, amezungumzia suala la boti za fibre kwa vijana wa Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya. Ziwa Nyasa linanufaisha mikoa mikuu mitatu ya Ruvuma, Mbeya na Njombe. Ni kweli kwamba tunahitaji kuendelea kuwawezesha vijana wetu katika wilaya zetu zote za Mbeya na hasa zinazozunguka ziwa hili ili waweze kuingia katika sekta yetu ya uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026, Wizara imetenga shilingi bilioni 9.5 kwa ajili ya kuwawezesha wavuvi kwa kutoa boti hizi za kisasa. Tumetenga bajeti hii kwa ajili ya kununua boti 100 za kisasa na boti 76 shikizi. Nimtoe wasiwasi, kwamba katika wale wananchi 2,100 ambao tumelenga kuwanufaisha kwa fedha hii basi vijana wa Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya nao watanufaika. Ninakushukuru sana.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved