Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Hawa Subira Mwaifunga
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga zahanati Kijiji cha Zugumlole itakayohudumia Vitongoji vya Kaung’ando, Ibasa “A” na “B”, Mkombozi, Ulinda na Ndevelwa?
Supplementary Question 1
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali, Kata ya Ndevelwa ina wananchi zaidi ya 11,000 kwa mujibu wa sensa, kijiji hiki mpaka kufika kwenye Zahanati ya Ndevelwa ni zaidi ya kilometa 25 kama majibu ya msingi yalivyoeleza. Kumekuwa na changamoto kubwa sana na hususani kwa akina mama wajawazito wanapokwenda kujifungua, barabara ni mbovu lakini pia kufika kwenye zahanati ni shughuli.
Je, Serikali haioni sasa umefika wakati wa kuharakisha ujenzi wa zahanati hii ili wananchi wa Kijiji za Zugumlole, Shaurimoyo na Inala waweze kupata huduma za afya kwenye eneo la karibu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, je, Serikali haioni sasa umefika wakati wa kupandisha hadhi Zahanati ya Ndevelwa ambayo inahudumia zaidi ya vijiji sita ili iweze kuwa kituo cha afya?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza, nimpongeze sana dada yangu Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini kwa namna ambavyo anafanya kazi kubwa ya kuwasemea na kufuatilia maendeleo ya Wananchi wa Tabora Mjini na sisi tukuhakikishie kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI tutaendelea kukupa ushirikiano kuhakikisha wananchi wa Tabora wananufaika na matunda ya Serikali yao sikivu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba umbali kutoka Zahanati ya Zugumlole mpaka kituo cha afya na hospitali ya halmashauri ni mkubwa na ndio maana Serikali tumeona umuhimu wa kuanza ujenzi wa zahanati katika Kijiji cha Zugumlole, na tayari Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya na Serikali ya Wilaya ilifika na kuongea na wananchi na kuwahamasisha wananchi ili waanze kwa utaratibu wetu wa mpango wa maendeleo ya afya msingi, waandae eneo la ujenzi wa zahanati, waanze hatua za awali za ujenzi wa boma na Serikali yetu itaweka mpango wa fedha kwa ajili ya kwenda kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo.
Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali itashirikiana na wananchi na Serikali za Mkoa wa Tabora na Halmashauri ya Tabora kuhakikisha Zahanati ya Zugumlole inajengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni kweli tumekuwa na kata ambazo zina idadi kubwa ya wananchi kama ambavyo Kata hii ya Ndevelwa ina idadi kubwa ya wananchi, lakini umbali mkubwa kwenda hospitali ya halmashauri. Tayari tumeshaweka utaratibu kwamba zahanati ambazo zina sifa ya kupandishwa hadhi kuwa vituo vya afya, Mkurugenzi wa Halmashauri alete maombi rasmi Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, tutatuma wataalam, watafanya tathmini na ikiwa vigezo vitaafikiwa tutahakikisha kwamba tunaweka utaratibu wa kujenga kituo cha afya. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Mbunge na nitumie nafasi hii kumsisitiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora kufuata utaratibu huo ili Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI iendelee na hatua zinazofuata.
Name
Mariam Nassoro Kisangi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Temeke
Primary Question
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga zahanati Kijiji cha Zugumlole itakayohudumia Vitongoji vya Kaung’ando, Ibasa “A” na “B”, Mkombozi, Ulinda na Ndevelwa?
Supplementary Question 2
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mitaa ya Temeke iliyoko katika Kata ya Temeke, Jimbo la Temeke haina kabisa zahanati wala kituo cha afya na hawawezi kutibiwa kwa urahisi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Je, Serikali haioni haja ya kujenga zahanati katika Kata ya Temeke?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, Serikali iliweka mpango wa ujenzi wa zahanati katika vijiji na mitaa, lakini pia katika kata za kimkakati ujenzi wa vituo vya afya.
Ninaomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mariam Kisangi kwamba Serikali inaendelea na utaratibu wa kuainisha maeneo ya kimkakati kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya, lakini pia mitaa ile yenye sifa kwa ajili ya ujenzi wa zahanati na tutahakikisha kwenye mipango yetu tunaweka kipaumbele Jimbo la Temeke kupata huduma ya zahanati na vituo vya afya.
Name
Sikudhani Yasini Chikambo
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga zahanati Kijiji cha Zugumlole itakayohudumia Vitongoji vya Kaung’ando, Ibasa “A” na “B”, Mkombozi, Ulinda na Ndevelwa?
Supplementary Question 3
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, tunafahamu kwamba viko vijiji mpaka leo havina zahanati, lakini kuna vijiji vingine wananchi wameamua kukusanya nguvu na kuanza ujenzi kikiwemo Kijiji cha Sisi kwa Sisi na tayari wamejenga boma wamefikia hatua ya lenta.
Ni nini kauli ya Serikali katika kuhakikisha nguvu za wananchi haziendi bure na wanapata zahanati kwenye kile kijiji? Ahsante.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita mwaka wa fedha 2021/2022 mpaka sasa Serikali imepeleka zaidi ya shilingi 40,000,000,000 katika halmashauri zetu na katika vijiji vyetu kwa ajili ya ujenzi wa maboma ya zahanati na hasa kumalizia maboma ambayo wananchi wameanza ujenzi kwa nguvu zao na kufikia hatua za lenta. Serikali ilikuwa inatoa shilingi 50,000,000 kila boma na maboma zaidi ya 3,500 yamekamilishwa.
Kwa hiyo, ninaomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaendelea na utaratibu wake kila mwaka wa bajeti tunaendelea kutenga fedha, kuhakikisha kwamba tunakamilisha maboma ya zahanati yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi yakiwemo maboma katika Wilaya ya Tunduru.
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Primary Question
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga zahanati Kijiji cha Zugumlole itakayohudumia Vitongoji vya Kaung’ando, Ibasa “A” na “B”, Mkombozi, Ulinda na Ndevelwa?
Supplementary Question 4
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, kituo cha afya kwa maana ya majengo Bumera, Kwihancha, Magoma, Genkuru vimekamilika pamoja na Mtana. Ni lini sasa huduma itaanza kutolewa katika maeneo hayo? Ahsante.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tulifanya ziara mara kadhaa na Mheshimiwa Waitara katika Jimbo la Tarime Vijijini na tulikwenda moja ya vituo vya afya kikiwepo cha Magoma pamoja na Kwihancha, na tuliona kazi kubwa iliyofanywa na Serikali kupeleka fedha kuhakikisha majengo yanakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tulianza na awamu ya kwanza ya ujenzi wa miundombinu, tumekwenda awamu ya pili ya kununua vifaa tiba na ninafahamu Tarime Vijijini na vituo hivyo vimepokea vifaa tiba na tumekwenda awamu ya tatu ya kuajiri watumishi kwa ajili ya kutoa huduma. Nikuhakikishie majengo yote yaliyojengwa yatapewa vifaa tiba stahiki na watumishi wataendelea kuongezwa ili kuhakikisha kwamba vituo hivyo vinatoa huduma stahiki. (Makofi)
Name
Moshi Selemani Kakoso
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tanganyika
Primary Question
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga zahanati Kijiji cha Zugumlole itakayohudumia Vitongoji vya Kaung’ando, Ibasa “A” na “B”, Mkombozi, Ulinda na Ndevelwa?
Supplementary Question 5
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Kijiji cha Kamsanga ni kijiji ambacho kimejenga zahanati kwa kutumia nguvu za wananchi, zahanati nzuri na ya kisasa na ina zaidi ya watu 25,000. Ni lini zahanati hii mnaipandisha hadhi ili kiwe kituo cha afya?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yote ambayo yana zahanati, lakini idadi kubwa ya wananchi zaidi ya 15,000 sera yetu ya afya inaelekeza kuwa na vituo vya afya. Kwa hiyo, eneo hilo la Zahanati ya Kamsanga ambayo ina idadi ya wananchi zaidi ya 25,000 ina sifa ya kuwa na kituo cha afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wetu ni kwamba halmashauri wanaainisha kama eneo hilo lina ukubwa unaotosheleza kujenga kituo cha afya, lakini pili wanapeleka maombi yao Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI ili tathmini ifanyike na iweze kuingizwa kwenye mpango kwa ajili ya ujenzi.
Kwa hiyo, ninaomba nikuhakikishie Mheshimiwa Kakoso, sisi tutawasiliana na Halmashauri ya Tanganyika ili tuweze kuweka utaratibu wa kupata taarifa kwa ajili ya kufanya tathmini na kuweka kwenye mipango yetu kwa ajili ya kupandisha hadhi zahanati hiyo kuwa kituo cha afya.
Name
Anne Kilango Malecela
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Same Mashariki
Primary Question
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga zahanati Kijiji cha Zugumlole itakayohudumia Vitongoji vya Kaung’ando, Ibasa “A” na “B”, Mkombozi, Ulinda na Ndevelwa?
Supplementary Question 6
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kata ya Kalemawe ni kata ambayo iko pembezoni sana na imesimama yenyewe sehemu za ziwani. Wakati wa kampeni kata hii tuliiahidi na iliahidiwa kwamba itajengewa kituo cha afya na Mkurugenzi wa Wilaya ya Same akalisimamia hili. Je, Serikali mnasemaje kuhusu ujenzi wa kituo cha afya kwenye Kata ya Kalemawe?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ni dhamira ya Serikali kusogeza huduma za afya karibu na wananchi na hususani vituo vya afya ili kupata huduma za dharura za upasuaji kwa akina mama wajawazito, lakini na wananchi wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili suala la muhimu ni kufanya tathmini ya vigezo, kwanza idadi ya wananchi katika kata husika, lakini pili ni umbali wa kutoka kituo cha jirani zaidi na kinachotoa huduma za upasuaji, lakini tatu upatikanaji wa eneo linalotosheleza mahitaji ya kituo cha afya.
Kwa hiyo, ninaomba nikuhakikishie Mheshimiwa mama yangu Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, kwamba tutafanya tathmini na nitumia nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same kuwasilisha taarifa hiyo na kuchanganua ikiwa vigezo vinafikiwa ili Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI tuone namna ya kuanza kutenga bajeti ili tuanze ujenzi wa kituo hicho ikiwa vigezo vitafikiwa.
Name
Agnesta Lambert Kaiza
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga zahanati Kijiji cha Zugumlole itakayohudumia Vitongoji vya Kaung’ando, Ibasa “A” na “B”, Mkombozi, Ulinda na Ndevelwa?
Supplementary Question 7
MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Minazi Mirefu iliyoko ndani ya Jimbo la Segerea yenye wakazi 31,000 haina zahanati wala haina kituo cha afya, lakini eneo la kujenga kituo cha afya lipo. Mheshimiwa Naibu Waziri ningeomba kufahamu, nini kauli ya Serikali kwa ajili ya wakazi wa Minazi Mirefu kwa ajili ya wao kupata kituo cha afya? Ahsante.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa vituo vya afya kwa mujibu wa mwongozo wa mpango wa maendeleo ya afya msingi ni kuendana na kata za kimkakati, na kwa aina ya setup ya Dar es Salaam yako maeneo ambayo yana idadi kubwa sana ya wananchi, lakini yako jirani na hospitali au vituo vya afya vingine na wanapata huduma katika maeneo hayo, lakini kuna maeneo mengine kata ziko mbali na zinahitaji ujenzi wa vituo vya afya.
Kwa hiyo, ninaomba nikuhakikishie Mheshimiwa Agnesta Lambert, Kata hiyo ya Minazi Mirefu tutaifanyia tathmini na kuona kama iko mbali zaidi na vituo vya afya vya jirani tuweze kufanya mipango kwa ajili ya ujenzi.