Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Tarimba Gulam Abbas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kinondoni
Primary Question
MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza: - Je, kuna mpango gani wa kuondoa mgongano wa Vikao vya Bunge na Halmashauri za Majiji, Manispaa na Miji ili Wabunge washiriki?
Supplementary Question 1
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini naomba niseme yafuatayo; kwamba najua halmashauri zinafanya kazi nzuri, Madiwani wanafanya kazi nzuri na hatuna sababu ya kupata mashaka ya kazi zao wanazozifanya, isipokuwa ushiriki wa Wabunge ni muhimu kwa sababu utaongeza, nitumie neno la kiingereza value katika majadiliano ya vikao vile. (Makofi)
Sasa kutokana na ukweli kwamba, hizi juhudi, Mheshimiwa Naibu Waziri anazosisema kwamba Serikali imekuwa ikiagiza, ukweli hazitekelezwi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ushauri wangu, sio ushauri, ni swali je, Serikali iko tayari kupeleka barua, kwa sababu Serikali inaendeshwa kwa barua. Barua mahususi zikieleza kwamba ama vikao vifanyike weekend ili Wabunge waweze kwenda au wakubaliane na ratiba za Mbunge bila kuathiri shughuli za halmashauri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nichukue nafasi hii nimpongeze sana Mheshimiwa Abbas Tarimba, Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, amekuwa msemaji mahiri sana wa wananchi wa Jimbo la Kinondoni, lakini si mara yake ya kwanza kutoa hoja hii ambayo ameuliza leo kuhusiana na Waheshimiwa Wabunge kupata fursa ya kushiriki Vikao vya Mabaraza ya Madiwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hoja hii imekuwa ni hoja ya miaka mingi ya Waheshimiwa Wabunge. Serikali inatambua umuhimu wa mchango wa Waheshimiwa Wabunge kushiriki kwenye Mabaraza ya Madiwani na Kamati za Kudumu za Halmashauri katika halmashauri zetu. Serikali ilishatoa maelekezo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini, kwamba kwanza wawasiliane na Waheshimiwa Wabunge ili kukubaliana tarehe za vikao na Waheshimiwa Wabunge wapate fursa ya kushiriki kwenye vikao hivyo na kutoa maoni yao, lakini pia kusimamia shughuli za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba ziko baadhi ya halmashauri ambazo hazijazingatia maelekezo ya Serikali na kuendelea na vikao hivyo wakati Waheshimiwa Wabunge wakiwa kwenye majukumu mengine ya kibunge.
Naomba nitumie nafasi hii kwanza, niwaelekeze kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, Wakurugenzi wote wa Halmashauri zetu kote nchini, wahakikishe wanafuata na kusimamia maelekezo ya Serikali kwamba kabla ya kupanga tarehe ya Vikao vya Baraza au Kamati za Madiwani, ni lazima wawasiliane na Wabunge husika, wakubaliane na ikiwezekana Waheshimiwa Wabunge washiriki kwenye vikao hivyo. Vivyo hivyo katika Mabaraza ya Madiwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nitoe angalizo kidogo, kwamba mara nyingine vikao vyetu vya Bunge vinakuwa virefu, kwa mfano Bunge hili la kuanzia Machi mpaka Juni, lakini kwa mujibu wa kanuni na miongozo pia, kuna vikao ambavyo vinatakiwa vifanyike kwenye ngazi za halmashauri kipindi hiki. Kwa hiyo, mara nyingine kuna changamoto za mwingiliano wa majukumu. Kwa mara hizo chache tunaweza tukakubaliana, tukafanya weekend au tukaruhusu wenzetu wakaendelea na vikao kwa niaba yetu na tukaenda kupata mrejesho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge tunalitambua suala hili na tuko tayari kuandika barua, maelekezo rasmi kwa Wakurugenzi ili waweze kusimamia utaratibu huu na Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, tutafuatilia utekelezaji wa maelekezo haya. (Makofi)
Name
Isack Joseph Copriano
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Monduli
Primary Question
MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza: - Je, kuna mpango gani wa kuondoa mgongano wa Vikao vya Bunge na Halmashauri za Majiji, Manispaa na Miji ili Wabunge washiriki?
Supplementary Question 2
MHE. ISACK J. COPRIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili limekuwa likijirudiarudia mara zote na kauli ya Serikali ni hiyo, tunatoa maelekezo kwa wakurugenzi, kwa wakurugenzi. Sasa ni vyema, kama jambo haliwezekani, ni afadhali Mheshimiwa Waziri akatuambia jambo hili haliwezekani ili tusiwe tunauliza jambo mara kwa mara tunaonekana...
Kwa hiyo swali langu ni, je, kwa nini sasa Serikali isiwe na maelekezo mahususi, kama alivyotoa kauli Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na haitekelezwi. Sasa nini kauli ya Serikali juu ya jambo hili? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Monduli, kaka yangu Kadogoo kwamba kwanza Serikali ilitoa maelekezo na si kwamba hayajatekelezeka. Baadhi ya halmashauri zimetekeleza na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakiwasiliana na halmashauri zao na kupanga vikao, na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakishiriki vikao hivyo. Kwa hiyo, maelekezo yaliyotolewa na Serikali yameendelea kutekelezwa, lakini ufanisi wa utekelezaji wake bado unahitaji kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kauli ya Serikali ni kwamba tutaendelea kusimamia maelekezo ya Serikali na kuhakikisha kwamba Waheshimiwa Wabunge wanashirikishwa, ili waweze kushiriki kwenye vikao hivyo vya Kamati na Mabaraza ya Madiwani, lakini kama ambavyo nilitoa angalizo, viko vipindi ambavyo Waheshimiwa Wabunge wana ratiba ambazo zimebana, lakini kwa mujibu wa kanuni na miongozo ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa, vikao vya Kamati ya Fedha ambavyo vinafanyika kila mwezi, lazima vifanyike ndani ya mwezi. Kila mwezi Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango, kila mwezi lazima vifanyike, mara nyingine Waheshimiwa Wabunge wanakuwa na majukumu mengi.
Kwa hiyo, lazima twende kwa ku-balance mazingira haya, kwamba kuna vikao vingine tunaweza tusishiriki, lakini vikao vilivyo vingi tutashiriki. Sisi tutafuatilia halmashauri kuzingatia utaratibu na mwongozo huo. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved