Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Latifa Khamis Juwakali
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza: - Je, Serikali imejipangaje katika kutafuta fursa za kuwawezesha vijana?
Supplementary Question 1
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri utaungana na mimi, huwezi kumtaja kijana bila kuigusa Wizara ya Kazi, Ajira na Mahusiano. Nilikuwa nataka kufahamu, Wizara ya Vijana mna ushirikiano gani wa karibu na Wizara hiyo ambayo nimeitaja katika kuzitafuta, kuzitangaza na kuzilinda ajira zote za nje ya nchi na pia kuwasimamia vijana wote ambao wanapata ajira nje ya nchi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Mheshimiwa Waziri wewe unafahamu kwamba ajira na fursa nyingi hazipo tu katika Wizara ya Vijana, zipo pia katika Wizara nyingine za kisekta.
Je, Wizara au Serikali kupitia Wizara ya Vijana haioni haja sasa kuanzisha Youth Desk Officers katika kila Wizara ili kuona namna gani Wizara ya Vijana inazisimamia fursa zote zinazotoka katika wizara za kisekta? Nakushukuru sana. (Makofi
Name
Joel Arthur Nanauka
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtwara Mjini
Answer
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba nimpongeze Mheshimiwa Latifa kwa kuwa mstari wa mbele kila wakati kufuatilia masuala yanayohusu vijana na kuongeza tija katika utekelezaji wake, kuhakikisha fursa zinapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyoeleza, Serikali inafanya kazi kwa muunganiko na sisi kama Wizara ya Maendeleo ya Vijana, tunafanya kazi kwa karibu sana na Wizara ya Kazi, Ajira pamoja na Mahusiano. Ahadi ya Chama Cha Mapinduzi ni kutoa ajira takribani 8,000,000 katika miaka mitano ijayo. Katika hilo, ilielekeza waziwazi kwamba inalenga pia kutafuta ajira nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Wizara ya Kazi, Ajira na Mahusiano, mikataba mbalimbali imekuwa ikiingiwa kati ya Serikali na nchi mbalimbali. Mpaka sasa kuna vijana 7,593 ambao wameenda katika mataifa mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuchukua nafasi hii nitoe wito kwamba tumekuwa na changamoto ya vijana kadhaa ambao wamekuwa wakielezea changamoto kuhusiana na mchakato huu. Serikali inaingia mikataba hii kupitia Balozi zetu na Serikali ndiyo custodian wa mikataba ya ajira kupitia mawakala wa ajira binafsi ambao wamesajiliwa na Serikali. Mwezi Februari mwaka huu zaidi ya mawakala 148 walifanya kikao na Serikali, katika kuhakikisha kwamba vijana wanatumia utaratibu unaofaa, wakitembelea tovuti ya Serikali wataona mawakala hao ambao wameidhinishwa na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hayo ni kwamba vijana huwa wanapewa taarifa kwa maana ya kupewa mafunzo, wanapopata nafasi ya kwenda nje ya nchi ili kuepusha changamoto ambazo wanakutana nazo. Serikali itaendelea kufanya hivyo ili kuhakikisha fursa nyingi zinaendelea kupatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili Mheshimiwa Latifa, ni kwamba Serikali ina Maafisa Maendeleo ya Vijana wanaopatikana katika halmashauri mbalimbali. Mara tu baada ya kuundwa kwa Wizara hii, mwezi Desemba tulifanya kikao cha pamoja cha uratibu na Maafisa Maendeleo ya Vijana wote wanaopatikana katika halmashauri zetu, nia ikiwa ni pamoja na kuongeza ufanisi katika mfumo. Nimepokea wazo ulilolitoa kuhusiana na Youth Desk, na nikuahidi kwamba Serikali italifanyia kazi ili kuhakikisha taarifa zinawafikia vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Name
Eng. Johnston Johansen Mutasingwa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Primary Question
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza: - Je, Serikali imejipangaje katika kutafuta fursa za kuwawezesha vijana?
Supplementary Question 2
MHE. ENG. JOHNSTON J. MUTASINGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, tuna vijana wengi sana wamejiajiri hasa upande wa garage. Kwa mfano pale Jimbo la Bukoba Mjini, tuna vijana zaidi ya 250 wako kwenye garage ya Mnyonge, lakini wako barabarani.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuweza kuwatengea maeneo maalumU ya kufanyia shughuli zao hizo za garage ili waweze kwanza kuwa na uhakika wa shughuli zao, lakini waweze kuwa na sifa za kupata mikopo ya Serikali? Ahsante
Name
Joel Arthur Nanauka
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtwara Mjini
Answer
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa swali la Mheshimiwa Mutasingwa na bahati nzuri nilishafanya ziara katika jimbo lake na nilipita katika maeneo ya garage na tulikuwa naye pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuhakikisha kwamba vijana hawa kwanza tunawarasimisha ili kupata urahisi wa wao kupata fursa ambazo Serikali inazitengeneza. Mpaka sasa kupitia programu ya urasimishaji ambayo inafanyika kupitia VETA, mwaka huu pekee yake malengo ni kurasimisha vijana 14,400. Ninaamini vijana mojawapo watakaopata fursa hii ni vijana wanaopatikana katika jimbo lako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kupitia TAMISEMI kumekuwa na utaratibu wa kupanga maeneo rasmi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanapata maeneo ambayo hawatabugudhiwa. Nimhakikishie, Serikali itaendelea kuratibu zoezi hilo na vijana wataendelea kupata nafasi na fursa za kufanya kazi katika maeneo ambayo ni rasmi. Ahsante sana.
Name
Josephine Joseph Kapoma
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza: - Je, Serikali imejipangaje katika kutafuta fursa za kuwawezesha vijana?
Supplementary Question 3
MHE. JOSEPHINE J. KAPOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, vijana wengi wamekuwa wanapata hizi fursa za mikopo na Serikali imejitahidi sana kufungua hizi fursa, lakini tumekuwa na shida kubwa sana kwa vijana kwa sababu wengi hawana nidhamu ya fedha (finance mistress), lakini sasa Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha Vyama vya Ushirika vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) ili waweze kujengewa uwezo wa kuwa na nidhamu ya fedha? Ahsante.
Name
Joel Arthur Nanauka
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtwara Mjini
Answer
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, Serikali imeendelea kujitathmini kila wakati kuona namna ambavyo mikopo inayotolewa hasa kwenye kundi la vijana inakuwa na ufanisi. Kama alivyoeleza Mheshimiwa Kapoma, ni kwamba kumekuwa na changamoto kubwa sana hasa katika urejeshaji, kwa mfano tukiangalia Mfuko wa Maendeleo wa Vijana, zaidi ya shilingi bilioni 3.9 zimeshindwa kurejeshwa. Tumefanya tathmini kuangalia changamoto ni nini, ikiwepo pia na asilimia nne zinazotolewa kupitia halmashauri zetu. Moja ya changamoto tuliyoiona, ni elimu ya kifedha na ndiyo maana kupitia awamu hii ya mikopo tuliyoitoa, tumeingia utaratibu wa makubaliano rasmi na taasisi ya kifedha hasa CRDB, ambayo kabla kijana hajapata mkopo, huwa anapata fursa ya kupewa mafunzo maalum yanayohusiana na usimamizi wa kifedha, nidhamu pamoja na biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafunzo haya yanakuwa endelevu pia, ili kuhakikisha kwamba wanaendelea kupata elimu hiyo kwa namna endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea wazo lako na ushauri wako juu ya kuwa na SACCOS za vijana, na kama ambavyo Serikali imeendelea kuwezesha kwenye vikundi, tutaendelea kuifanyia kazi ili kuhakikisha kwamba vijana wanafikiwa kwa wingi. Ahsante sana.
Name
Asia Abdulkarim Halamga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza: - Je, Serikali imejipangaje katika kutafuta fursa za kuwawezesha vijana?
Supplementary Question 4
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wa Wilaya ya Hanang, wameniagiza na kunituma, wanakuhitaji, Mheshimiwa Waziri, je, ni lini utakuja kukutana na vijana wa Wilaya ya Hanang?
Name
Joel Arthur Nanauka
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtwara Mjini
Answer
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa swali la Mheshimiwa Asia na nimpongeze pia kwa kuendelea kufuatilia masuala yanayohusu vijana hasa katika Jimbo lake la Hanang.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wizara, tunao utaratibu na ratiba ya kutembelea vijana katika maeneo mbalimbali kama ambavyo tumefanya tayari katika maeneo kadhaa ya nchi yetu. Nimhakikishie Mheshimiwa Asia, tutakapokuwa tunaweka ratiba kwa mara nyingine tena, basi tutafika pia katika Jimbo la Hanang kuweza kuwafikia na kuweza kusikia changamoto zao, lakini pia kuwaletea fursa ambazo zinapatikana. Nashukuru sana. (Makofi)
Name
Rashid Abdallah Shangazi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Primary Question
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza: - Je, Serikali imejipangaje katika kutafuta fursa za kuwawezesha vijana?
Supplementary Question 5
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, tatizo la vijana sio mitaji na ajira pekee, lakini yako matatizo makubwa sana ya kisera kwenye sekta mbalimbali yanayowafanya vijana wasikue kwa haraka. Ni upi mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba sera zote katika kila sekta zinapitiwa ili kuruhusu ukuaji wa wa mitaji na uwezo wa wa kiuchumi kwa vijana?
Name
Joel Arthur Nanauka
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtwara Mjini
Answer
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MAENDELEO YA VIJANA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na nashukuru kwa swali la Mheshimiwa Shangazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba changamoto za vijana ni zaidi ya mitaji na ndiyo maana kwa mujibu wa Sera yetu ya Maendeleo ya Vijana Toleo la mwaka 2024, limeainisha maeneo 13 ambayo tunayalenga na mitaji ni sehemu mojawapo tu ndogo. Nimhakikishie Mheshimiwa Shangazi kwamba tumeendelea kufanya marejeo na mapitio ya sera ambazo zitatusaidia pia kuelekea katika sheria. Moja ya mafanikio ya sera ya mwaka 2007 ilikuwa ni kutungwa kwa sheria ya asilimia nne katika halmashauri zetu, lakini pia 30% ya manunuzi kwa ajili ya makundi maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tutaendelea kufanya hivyo kama Serikali na kuhakikisha kwamba kila eneo ambalo vijana wanaweza wakapata fursa tunaendelea kuleta marekebisho hayo ya kisera zaidi. Nashukuru sana.