Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Twaha Said Mwakioja

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkinga

Primary Question

MHE. TWAHA S. MWAKIOJA aliuliza: - Je, lini Serikali itafanya utafiti wa vyanzo vya uhakika vya maji Tarafa ya Maramba, Wilaya ya Mkinga ili kutatua changamoto ya maji kwa wananchi?

Supplementary Question 1

MHE. TWAHA S. MWAKIOJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali japo kwa maoni yangu nayaona bado ni majibu mepesi. Hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mkinga na hususan tarafa ya Maramba imekuwa na miradi ambayo haijakamilika na ilipaswa kukamilika tangu mwaka 2023 na wakandarasi wameshaondoka maeneo ya mradi na sababu kuu ni kwamba wakandarasi hawa hawajalipwa; Kata ya Gombero mkandarasi ameondoka na anadai shilingi bilioni 1.2, Kata ya Mhinduro, mkandarasi ameondoka na anadai shilingi milioni 368, Kata ya Mapatano mkandarasi ameondoka na anadai shilingi milioni 196, Mradi wa Mkinga - Horohoro mkandarasi anadai zaidi ya shilingi bilioni 1.7.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, pamoja na fedha nyingi tunazopewa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, miradi hii imechelewa zaidi ya miaka minne wananchi hawapati maji. Je, sasa ni lini Serikali ituambie kwa uhakika kabisa wakandarasi hawa watalipwa ili wakandarasi warudi na wananchi waweze kupata maji safi na salama waliyoahidiwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; tarafa hii ya Maramba ina hali ngumu sana ya upatikanaji wa maji na hususan wakati wa kiangazi. Naomba Serikali ituambie, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuambatana nami mara tu baada ya Bunge hili la bajeti ili tutembee kata kwa kata tujionee hali halisi na ikiwezekana tupate vyanzo vya uhakika na ikibidi tarafa hii ya Maramba tuweze kuiunganisha na mtandao wa Gridi ya Maji ya Taifa? Ahsante. (Makofi)

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Twaha Said Mwakioja, Mbunge wa Mkinga kwa kazi nzuri, kubwa anayoifanya na kwa ufuatiliaji na kwa kata hii ya Maramba natambua kwamba Mheshimiwa Mbunge aliongea kwenye bajeti yetu ya maji, lakini pia amekuwa na mawasiliano ya karibu sana na Mheshimiwa Waziri wa Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na swali lake la kuhusu miradi iliyoko katika kata tatu; mradi wa kwanza ambao umesema upo Gombero ni kweli, lakini Mradi wa Mapatano pamoja na Mhinduro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Gombero umeshafikia 100% maana yake umeshakamilika, mkandarasi natambua anadai kiasi cha shilingi bilioni 1.2. Mradi wa Mapatano kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema upo katika hatua ya 35% ya utekelezaji na Mradi wa Mhinduro upo 46%. Tunatambua tulikuwa tunafanya uhakiki wa zile hati zake za madai ili tulipe fedha inayoendana na kazi ambayo kule imefanyika kwa sababu tumebaini kuna maeneo mengine hati zinazoletwa haziiendani na hali halisi ya kazi iliyofanyika site, hizi ni fedha za Watanzania za walipakodi wa Tanzania lazima tuzisimamie ili ziweze kutoa matokeo halisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nakuhakikishia kazi ya uhakiki tumeshaimaliza, sasa tunasubiri kuwalipa wakandarasi ili waweze kurudi site kwa upande wa Mapatano pamoja na Mhindiro waweze kufanya kazi nzuri.
Mheshimiwa Mweyekiti, lakini pia upande wa Mkinga Horohoro Mheshimiwa Rais amewekeza zaidi shilingi bilioni 35 katika mradi huu na mradi huu upo hatua nzuri kabisa sisi tunachokifanya hatupeleki fedha kwa kasi tunayotaka sisi, tunapeleka fedha baada ya hati ya madai kuja mezani.

Kwa hiyo, sisi tutahakikisha kwamba tunaongeza msukumo pale ambapo hati imeshafika mezani lazima mkandarasi alipwe na kuhakikisha kwamba mradi uweze kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hali ya upatikanaji wa maji Mheshimiwa Mbunge hata wewe unafahamu, hivi sasa ni zaidi ya 72.9% natambua changamoto ya kwenda kufanya utafiti. Mheshimiwa Waziri ulimuomba kwenda katika jimbo lako, nataka nikupe taarifa nzuri ni kwamba Mheshimiwa Waziri pamoja na wataalam wa Wizara pamoja na wewe, yupo tayari kuambatana nawe kwenda katika jimbo lako ili kwenda kufanya kazi hiyo, lakini lengo kubwa ni nini, lengo kubwa la kwenda Mkinga la kwanza ni kwenda kufanya tathmini ya vyanzo vya maji vilivyopo na la pili kwenda kubaini vyanzo vipya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, kama ambavyo umeomba kuangalia uwezekano wa Tarafa ya Maramba inaunganishwa kwenye Gridi ya Taifa ya Maji. Katika hili hatutosubiri Mheshimiwa Waziri aende, ninawaelekeza bonde waanze kufanya hii kazi kabla ya Mheshimiwa Waziri hajaenda ili anapofika wampatie taarifa ya tathmini ambayo watakuwa wameshaifanya na wewe Mheshimiwa Mbunge ukiwepo ili sasa tuanze kuchukua hatua ya kufanya feasibility study, baada ya hapo tupate fedha na baada ya hapo tuanze kutekeleza mradi bila kuwa na cha...

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu sauti yako ni sauti ya wananchi wa Mkinga na sisi kama Serikali tutaendelea kushirikiana na wewe ili kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji ndani ya Jimbo la Mkinga, ahsante sana.

Name

Ramadhani Hamza Singano

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bumbuli

Primary Question

MHE. TWAHA S. MWAKIOJA aliuliza: - Je, lini Serikali itafanya utafiti wa vyanzo vya uhakika vya maji Tarafa ya Maramba, Wilaya ya Mkinga ili kutatua changamoto ya maji kwa wananchi?

Supplementary Question 2

MHE. RAMADHANI H. SINGANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, Wilaya Lushoto miongoni ya wilaya ambazo maeneo machache yana changamoto ya maji juu ya ardhi ikiwemo Kata ya Milingano maeneo ya Kwebamba na Kishimai, lakini Kata ya Mbwei na Malibwi kwa Tarafa ya Mlola. Je, Serikali ina mpango gani madhubuti wa kimkakati na wa kiutafiti kuhakikisha kwamba maeneo hayo yanafanyiwa utafiti na kuwapatia suluhu ya changamoto ya maji?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Engineer Ramadhani Singano, Mbunge wa Bumbuli, lakini kwa kumbukumbu yangu napata kujua kwamba kata hizi ambazo ameziongelea ziko katika Jimbo la Profesa Shemdoe ambazo ziko upande wa Lushoto, lakini kwa Kata ya Mbwei mwaka 2022 tulipata fedha za UVIKO kiasi cha shilingi milioni 430 mradi huu ulitekelezwa na unafanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaendelea kuboresha kuna kuna chanzo cha mto fulani kitu kama Kiloleli, Kilole kitu kama hicho tunaendelea kufanya tafiti ili kubaini kama tuna uwezo wa kutumia chanzo hicho ili tupeleke maji tena kwenye Kata ya Mbwei lengo ni kuhakikisha kwamba tunaendelea kuboresha zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ramadhani Singano ni mtaalamu wa masuala haya ya maji (water resources) tunatambua kwamba namna gani anatamani tuendelee kuhakikisha kwamba tunawatumia wataalam wa Wizara ya Maji kubaini vyanzo vipya ili tuhakikisha kwamba tunaendelea kuboresha huduma ya maji safi na salama. Tunaendelea kupokea maoni na ushauri ili tuendelee kuboresha upatikanaji wa huduma maji safi na salama kwa wananchi, ahsante sana.

Name

Abdallah Jafari Chaurembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbagala

Primary Question

MHE. TWAHA S. MWAKIOJA aliuliza: - Je, lini Serikali itafanya utafiti wa vyanzo vya uhakika vya maji Tarafa ya Maramba, Wilaya ya Mkinga ili kutatua changamoto ya maji kwa wananchi?

Supplementary Question 3

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Kilungule ina changamoto ya upatikanaji wa maji safi ya kunywa na matamu. Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa maji kutoka Mashine ya Maji Mtoni kupeleka Kata hiyo ya Kilungule?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chaurembo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Dar es Salaam ni eneo ambalo tunasema kwamba ni eneo la kiuchumi na ni muhimu sana kuhakikisha kwamba huduma ya maji inakuwa sehemu ya kichocheo cha uchumi wa Jiji la Dar es Salaam, lakini nikizingatia kwamba chanzo tayari tunacho, kinachohitajika tu ni kuongeza mtandao kufika katika kata ambayo Mheshimiwa Mbunge amesema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalipokea na nimwelekeze kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji Chief Executive Officer wa DAWASA atume wataalamu wake, wakafanye tathmini na kujiridhisha kwamba tunaweza tukachukua hatua ipi ili kuhakikisha kwamba wananchi wa kata ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja basi wapate huduma ya maji safi na salama baada ya kuwa tumetengeneza mtandao wa kuwafikia wananchi hao, ahsante sana.