Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Saashisha Elinikyo Mafuwe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Primary Question
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza: - Je, kuna mpango gani wa kudhibiti watoa elimu ya afya na aina ya ulaji mitandaoni bila kuwa na taaluma inayotambulika jambo linalowachanganya wananchi?
Supplementary Question 1
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa kuwa tuko hivi kutokana na aina ya ulaji wetu; na kwa kuwa tunakula kutokana na aina ya elimu tunayopewa; na kwa kuwa Serikali imekubali kwamba tatizo hili la utoaji wa elimu iliyochanganyikana na mambo mengi isiyothibitika lipo; na kwa kuwa Serikali imekubali kwamba sheria ipo hai inayodhibiti mambo haya; na kwa kuwa Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali langu maswali ya papo kwa papo alitoa maagizo kwa Serikali sheria hii izingatiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni mpango gani thabiti wa Serikali na ni lini Serikali itaanza kutekeleza sheria hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili Serikali imesomesha Maafisa Lishe na wataalamu wengine wanaohusika na lishe, lakini Serikali imeajiri Maafisa Lishe ngazi zote na wapo kwenye maeneo yetu.
Je, ni lini sasa Serikali itawatumia maafisa lishe kutoa elimu hii pamoja na kuunda Baraza la Lishe Tanzania ili waweze kushauriana na elimu hii iwe centralized kwa watu ambao wana taaluma ya kutoa elimu ya lishe kuliko ilivyo sasa hivi kila mtu ni mwalimu wa lishe?
Name
Dr. Florence George Samizi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Saashisha kwa kazi nzuri anayofanya ya kufuatilia lishe za Watanzania ambazo lishe ni kigezo muhimu katika kukuza uchumi wa nchi hii, lakini nimshukuru pia Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye amelijibu swali hili tarehe 7 Mei na akalitolea ufafanuzi mzuri sana na sina sababu ya kurejea ufafanuzi ule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na alituelekeza tufanye tathmini ya suala hili linavyoendelea. Tathmini ambayo itatusaidia kwanza, kuwatambua hao wato wa elimu wanaotoa elimu bila kuwa na vibali. Pili, kuweka kanuni na taratibu ambazo zitawafanya waweze kufuatilia kupata vibali; tatu, tuweze kuwa na Kamati ambayo itafuatilia kwa ukaribu zaidi maudhui ya hayo na mengine mengi yatakayotufanya tuweze kufanya reinforcement ya hiyo sheria ambayo kiukweli haijafanyiwa reinforcement.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimhakishie Mheshimiwa Mbunge tayari wataalamu wako kazini wanaendelea kufanyia kazi tathmini hizo na pindi zitakapoisha basi tutaanza utekelezaji wa sheria hii kiukamilifu ili tuweze kuendana na hali ya sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ukweli ndio mwanalishe wa kwanza ambaye ameajiri Maafisa Lishe nchi nzima. Kila halmashauri ina zaidi ya Maafisa Lishe wawili mpaka watatu. Tunao zaidi ya Maafisa Lishe 600 nchi nzima ambao wanafanya elimu hii ya lishe lakini wanatumia taratibu za kizamani. Wanatumia redio rasmi, wanatumia mitandao rasmi, ambayo dunia sasa haiko huko kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaomba nitoe rai, niwaelekeze Maafisa Lishe wote sasa tubadilike, twende na dunia inavyoenda, tuwafuate hao wananchi waliko. Wanataka huko kwenye Instagram kwenye Facebook ndiko waliko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia sasa waendane na hali ya sasa. Watoe elimu ambayo inavutia walaji ili wale wananchi waweze kusikiliza hicho wanachokifundisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa watumie influencers kwa sababu sisi Wizara ya Afya tunayo page ya elimu kwa jamii lakini ina followers wachache. Kwa hiyo, niwaombe kwamba tutumie influencers ili watu waweze kufikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mwisho kabisa niwaombe Watanzania, nchi yetu inao wataalamu wa lishe ambao wamekidhi vigezo ambao wanatoa elimu, basi tuwasikilize kule kwenye jamii zetu tunazo redio za local content ambazo Maafisa Lishe wanazitumia. Tufuate huko tuwasikilize lakini na Watanzania basi tusikilize elimu ya wataalamu ambao wameaminiwa na Serikali kulingana na mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved