Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Revocatus Chipando Clayton

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Mjini

Primary Question

MHE. CLAYTON R. CHIPANDO aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza mtandao wa Barabara za lami Kigoma Mjini kwa kuongeza bajeti?

Supplementary Question 1

MHE. CLAYTON R. CHIPANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI, nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza. Moja litakuwa swali, na lingine litakuwa ombi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Bwawa la Katubuka linazidi kuwaletea madhara makubwa sana wananchi wa Kata ya Katubuka na tayari kulikuwa na mkandarasi pale anaendelea na kazi ya kutoa maji yale kwa kutengeneza mtaro mkubwa ambao ulikuwa unayapeleka maji Ziwa Tanganyika. Sasa hivi ameondoa vifaa katika eneo la site. Serikali ina mpango gani wa kumlipa yule mkandarasi ili aweze kumaliza kazi ya kuyaondoa yale maji na kuwaacha wananchi katika makazi yao wakiwa na amani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi la pili, nilikuwa ninaiomba Serikali, sisi Wabunge pamoja na kufanya maendeleo, lakini tunafanya siasa pia. Tulikuwa tunaomba, pale ambapo wanaleta fedha ya ujenzi wa barabara, basi wataalamu wetu waambiwe waje washauriane na sisi, ni barabara gani ambazo zikienda kujengwa zitatusaidia, na pia ndiyo kilio cha wananchi wetu katika Majimbo yetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani ukiwa uko huku Bungeni unaambiwa tu greda liko mtaani linafanya kazi, unaweza kukuta hiyo barabara inayojengwa ni barabara ambayo kwenye ahadi zako kwa wananchi wako haina umuhimu kama kuna barabara nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kwa ruhusa yako naomba nimtajie barabara tano ambazo hata nikifa leo ninaomba zijengwe katika Jimbo la Kigoma Mjini. Barabara ya kutokea Uwanja la Lake Tanganyika kupita Bezebazeba Sokoni – Rusimbi, Kata ya Majengo pamoja na Kata ya Machinjioni. Barabara ya kutokea Kata ya Mwanga Kaskazini inaitwa Barabara ya Serengeti inayounganisha Kata ya Mwanga Kaskazini na Kata ya Gungu; Barabara ambayo inaunganisha Kata ya Buhanda na Kata ya Businde; Barabara ambayo inaanzia Shini – Vamia – Bega; Barabara ambayo inaanzia Madukani…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Clayton ahsante. Ameshakuelewa kwa sababu hilo ni ombi, siyo swali. Kwa hiyo, Mheshimiwa Naibu Waziri ameshakuelewa, tunashukuru…

MHE. CLAYTON R. CHIPANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naomba sana Mheshimiwa Waziri abaki na hizi barabara kichwani hata nikifa leo hayo ndiyo maombi ya wananchi wa Kigoma Mjini. (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, niaomba kwanza nikubaliane na Mheshimiwa Clayton Revocatus Chipando, Mbunge wa Kigoma Mjini kwamba Bwawa la Katubuka ambalo limekuwa likisababisha mafuriko ya mara kwa mara kwa wananchi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Serikali inatambua kwamba kuna changamoto hiyo na ndiyo maana ilishapeleka mkandarasi pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumeshafanya addendum kwenye mkataba kuhakikisha kwamba mkandarasi analiingiza suala la ujenzi wa mfereji mkubwa wa kutoa maji kwenye maeneo hayo yanayosababishwa na mafuriko ya Bwawa la Katubuka kupeleka Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tuko hatua za mwisho za kufanya malipo kwa mkandarasi ili arejee, aendelee na ujenzi na hatimaye kuondoa kero hiyo ya mafuriko ya mara kwa mara kwa wananchi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, ni kweli kwamba kuna fedha za ujenzi wa barabara ambazo zimeendelea kupelekwa kwenye Majimbo yote kote nchini likiwemo Jimbo la Kigoma Mjini. Hivi karibuni Jimbo la Kigoma Mjini limepelekewa jumla ya shilingi milioni 898 kwa ajili ya kujenga lami ya Baptists mita 800, lakini shilingi milioni 450 kwa ajili ya kujenga Barabara ya Zuru kiwango cha zege mita 420 na bajeti ya Kigoma Mjini imeongezeka kwa mwaka 2025/2026 kutoka bilioni 3.2 za mwaka uliopita mpaka shilingi bilioni 5.33.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inathamini uboreshaji wa miundombinu ya barabara katika Mji wa Kigoma, lakini nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI kuwaelekeza Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kwamba ni maelekezo ya Serikali kwamba fedha zozote zinapoingia katika Majimbo yetu, lazima Waheshimiwa Wabunge wapewe taarifa rasmi ya mapokezi ya fedha hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango ya utekelezaji iwe barabara au miundombinu mingine yoyote, lazima Waheshimiwa Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi katika Majimbo hayo washirikishwe ili tuwe na uelewa wa pamoja na maamuzi ya pamoja ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili limetolewa maelekezo mara kadhaa. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge kwamba tutafuatilia kwa karibu na tutachukua hatua kwa Wakurugenzi na Watendaji ambao hawatatekeleza maelekezo haya ya Serikali. (Makofi)

Name

Mecktridis Fratern Mdaku

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Malinyi

Primary Question

MHE. CLAYTON R. CHIPANDO aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza mtandao wa Barabara za lami Kigoma Mjini kwa kuongeza bajeti?

Supplementary Question 2

MHE. MECKTRIDIS F. MDAKU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Jimbo la Malinyi lina mtandao wa mita chache za lami. Je, ni lini sasa Serikali ina mpango wa kuongeza kupitia programu ya kuboresha Halmashauri za Wilaya au Makao Makuu ya Wilaya kwa kiwango cha lami? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mheshimiwa Mbunge wa Malinyi, Mheshimiwa Mecktridis amelifuatilia suala la Barabara za Malinyi mara kwa mara. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tu kwamba tunaendelea kutenga fedha kwa awamu kwa ajili ya kujenga barabara kwa kiwango cha changarawe na pale inapowezekana kuendelea kujenga barabara kiwango cha lami na tutahakikisha kadri fedha zinapopatikana tunatoa kipaumbele cha juu kabisa kwa ajili ya Mji wa Malinyi.