Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Daniel Awack Tlemai
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Karatu
Primary Question
MHE. DANIEL A. TLEMAI aliuliza: - Je, lini Serikali itatimiza ahadi yake ya shilingi bilioni 4.5 kwa wananchi wa Mji wa Karatu ili waweze kupata huduma ya uhakika ya majisafi?
Supplementary Question 1
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa nafasi ya swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali madogo ya nyongeza. Kwa kuwa upatikanaji wa maji katika Mji wa Karatu ni 52%, na tunaishukuru Serikali imechimba visima vinne katika Mji wa Karatu na visima hivyo vinne ili vikamilike vinahitaji shilingi bilioni 2.7. Lini Serikali itatoa shilingi bilioni 2.7 ili wananchi wa Mji wa Karatu waweze kupata maji katika Mji wa Karatu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la nyongeza, kwa kuwa kuna Mto Endoro katikati ya Mji wa Karatu ambao unatiririsha maji kutoka Mlima Ngorongoro. Je, ni lini Serikali itaweka mpango wa kujenga bwawa ili kuongeza uhitaji wa maji katika Mji wa Karatu na ule mto ukawa sehemu ya chanzo cha kuongeza maji katika Mji wa Karatu? (Makofi)
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake muhimu ya nyongeza yanayogusa mahitaji ya moja kwa moja ya wananchi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali la kwanza, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 2.7 katika bajeti ya 2026/2027 ili kuhakikisha tunaenda kujenga miundombinu inayotokana na visima vile vitatu ambavyo vimeshachimbwa tayari na vina uwezo wa kutoa lita 200,000 kwa saa. Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, kwamba tayari Serikali imeshaanza kuchukua hatua katika hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la pili, katika Mji wa Karatu tunalo bwawa ambalo linatoa huduma ya majisafi kwa wananchi wa Karatu Mjini pale, lakini pia kulingana na jiografia ya Karatu, kuna kipindi cha masika maji huwa yanaporomoka kutoka kwenye Milima ya Ngorongoro kule na Hifadhi ya Ngorongoro na hatimaye kuchafua miundombinu na kuharibu bwawa lile ambalo linatoa huduma ya majisafi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ilitoa fedha kiasi cha shilingi milioni 600 kwenda kujenga mitaro ambayo itazuia maji yanayoshuka ili yasiende kwenye bwawa linalotumika kwa matumizi ya maji kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunao mpango mkakati wa miaka mitano ambapo tutaenda kujenga bwawa katika mto. Kuna mto unaitwa Mto Endoro ambapo tutakapojenga lile bwawa, litasaidia kuyachukua yale maji (kuyateka) ili kuzuia mafuriko; pia, tutayatumia kwa ajili ya matumizi ya wananchi wa Mji wa Karatu kwa sababu ni maji mazuri kabisa, lakini pia kwa jiografia yake itatusaidia kuyatumia bila ya kuwa na gharama ya kuweka pump kwa sababu yatakuwa yanashuka kwa gravity.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana.
Name
Ester Amos Bulaya
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DANIEL A. TLEMAI aliuliza: - Je, lini Serikali itatimiza ahadi yake ya shilingi bilioni 4.5 kwa wananchi wa Mji wa Karatu ili waweze kupata huduma ya uhakika ya majisafi?
Supplementary Question 2
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Mcharo kwenye Kijiji cha Kisangwa, Bunge lililopita tulienda kuzindua mradi wa maji. Hivi ninavyozungumza, mradi umesimama kwa sababu bado hamjapeleka fedha zaidi ya shilingi milioni 700, na ule mradi ukikamilika, maji yale yataenda mpaka kwenye Chuo cha Kisangwa, ambapo wanafunzi wanapata adha sana ya shida ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itapeleka fedha ili mradi huo ukamilike, wanachuo wanufaike na maji, na wananchi wangu wa Jimbo la Bunda Mjini kwenye Kata ya Mcharo?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la nyongeza, swali muhimu sana kwa wananchi wa Bunda Mjini, kwa sababu sauti yao imesikika na Serikali inatambua kwamba ni kweli kumekuwepo na changamoto ya ucheleweshwaji wa malipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamtoa hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali baada ya kufanya uhakiki wa madai ya hati ambazo zimewasilishwa, sasa tumeanza kulipa awamu kwa awamu ili kuhakikisha kwamba madeni ambayo wakandarasi wanadai, basi yaweze kuanza kulipwa na kumalizika na wao waweze kumalizia miradi yote nchini, ahsante sana.
Name
Dr. Jasson Samson Rweikiza
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Vijijini
Primary Question
MHE. DANIEL A. TLEMAI aliuliza: - Je, lini Serikali itatimiza ahadi yake ya shilingi bilioni 4.5 kwa wananchi wa Mji wa Karatu ili waweze kupata huduma ya uhakika ya majisafi?
Supplementary Question 3
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Mheshimiwa Waziri, nina Mradi wa Maji wa Kemondo Maruku, leo ni mwaka wa sita tangu umeanza kujengwa, lakini hatujapata maji na kuna shida kubwa sana ya maji Vijiji vya Maruku na Kanyangereko, hasa baadhi ya Vijiji vya Kemondo havina maji mwaka wa sita. Ni nini mpango wa Serikali kuhusu mradi huo?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa tunayo changamoto ya maji katika eneo la Kemondo, ambapo mradi huu mkubwa ulikuwa ni ahadi ya viongozi wa Kitaifa, lakini pamoja na ahadi hiyo, mradi huo tayari ulikuwa umeshaanza na fedha tayari zimeshapelekwa na utekelezaji ukaanza. Tunatambua kwamba mradi haujakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamtoa hofu Mheshimiwa Wakili Msomi Rweikiza kwamba dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba tunakamilisha miradi yote, na huu Mradi wa Maruku tutaupatia kipaumbele kuhakikisha kwamba katika mwaka huu wa fedha unaenda kukamilika, ahsante sana.
Name
Amina Mussa Mkumba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kibiti
Primary Question
MHE. DANIEL A. TLEMAI aliuliza: - Je, lini Serikali itatimiza ahadi yake ya shilingi bilioni 4.5 kwa wananchi wa Mji wa Karatu ili waweze kupata huduma ya uhakika ya majisafi?
Supplementary Question 4
MHE. AMINA M. MKUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa kuna Mradi wa maji Mchungu katika Jimbo la Kibiti, Kata ya Mwambao na Mradi huu unatoa maji yenye chumvi nyingi sana, Serikali ina mpango gani wa kufunga mtambo desalination plant ili watu waweze kupata majisafi na salama? (Makofi)
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia na kubaini changamoto ambayo wananchi wanapitia katika kutumia maji ambayo yana chumvi. Ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba kwa mujibu wa Sera yetu ya Maji ya Mwaka 2002 Toleo la Mwaka 2025, tunatakiwa kuhakikisha watu wanapata huduma ya majisafi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muktadha huo, ninatumia fursa hii kwa niaba ya Waziri wa Maji, kuelekeza wataalamu wetu waende wakafanye tathmini, kwanza, kama inawezekana kuyatibu yale maji na ili yanyweke bila ya kuwa na changamoto ya chumvi, ama kama maji hayo chumvi yake ina concentration kubwa ambapo haiwezekani, basi tutafute chanzo kingine tukachimbe kisima ili kuhakikisha kwamba tunawafikishia wananchi huduma ya maji yaliyo safi na salama, ninakushukuru sana.
Name
Dr. Lazaro Killiani Komba
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Peramiho
Primary Question
MHE. DANIEL A. TLEMAI aliuliza: - Je, lini Serikali itatimiza ahadi yake ya shilingi bilioni 4.5 kwa wananchi wa Mji wa Karatu ili waweze kupata huduma ya uhakika ya majisafi?
Supplementary Question 5
MHE. DKT. LAZARO K. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali dogo la nyongeza katika eneo hili la maji. Kwanza niishukuru Serikali, inafanya kazi kubwa katika sekta hii hasa katika Jimbo la Peramiho, lakini tuna vijiji sita mpaka sasa hakuna huduma ya maji. Je, ni lini Serikali itapeleka huduma hii ya maji katika vijiji hivi sita ambavyo vimebaki?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba tunavyo vijiji takribani 1,575 ambavyo havijapata miundombinu rasmi ya utoaji wa huduma ya majisafi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe hofu, tunao mpango mkakati ndani ya kipindi cha miaka mitano tutahakikisha kwamba na Serikali imejipanga, awamu kwa awamu tutaenda kuhakikisha kwamba vijiji vyote 1,575 vinapata huduma ya majisafi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia bajeti hii katika vijiji hivyo sita, baadhi ya vijiji, ninaomba tukitoka hapa Mheshimiwa Mbunge tukutane ili angalau baadhi ya vijiji tuviingize kwenye bajeti tuanze hatua moja wapo ya kutatua changamoto ya maji katika vijiji hivyo sita vya Mheshimiwa Mbunge na nimpongeze sana kwa kuchaguliwa, ahsante sana.
Name
Festo Richard Sanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makete
Primary Question
MHE. DANIEL A. TLEMAI aliuliza: - Je, lini Serikali itatimiza ahadi yake ya shilingi bilioni 4.5 kwa wananchi wa Mji wa Karatu ili waweze kupata huduma ya uhakika ya majisafi?
Supplementary Question 6
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza nichukue nafasi hii kuishukuru Dayosisi ya Kusini Kati kwa sababu imekuwa iki-support sana miradi ya maji Wilaya ya Makete. Tuna Mradi wa Maji wa Mang’oto, Lupalilo, na Tandala; ni mradi wa maji ambao tuliandika andiko tukaleta Wizarani, hatujapata majibu hadi leo. Ni lini Serikali itawajibu wananchi kuhusu mradi huu mkubwa utakaosaidia Kata ya Mang’oto, Tandala na Lupalilo?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua na tunampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kusimamia na kuandika andiko lenye kutoa uelekeo wa nini kifanyike ndani ya Makete. Nimtoe hofu, kuanzia leo nitafuatilia kuhusu andiko hilo, nijue limefikia hatua gani na tutampa mrejesho Mheshimiwa Mbunge ili kujua wananchi wake wanaweza kutatuliwa changamoto yao kwa uharaka zaidi. Ahsante sana.
Name
Zainab Rashid Kawawa
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DANIEL A. TLEMAI aliuliza: - Je, lini Serikali itatimiza ahadi yake ya shilingi bilioni 4.5 kwa wananchi wa Mji wa Karatu ili waweze kupata huduma ya uhakika ya majisafi?
Supplementary Question 7
MHE. ZAINAB R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Bwawa la Mto Rufiji ni lini Serikali itaanza ujenzi wake kwa kuwa tumesubiri kwa muda mrefu ahadi hiyo mpaka sasa hatujaona utekelezaji wake? Ahsante.
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya vyanzo vya uhakika ambavyo tunavitegemea ni Bonde la Mto Rufiji, kwani litatatua changamoto kwa ukubwa wake katika utoaji wa huduma katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam. Vilevile tunatamani baada ya kuchukua haya maji kuyapeleka Dar es Salaam, tuyachukue pia tuyapeleke mikoa ya Lindi. Lengo ni kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto ya majisafi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, Serikali tayari imeshaanza mchakato wa kumpata mshauri ili aanze kufanya upembuzi yakinifu na baada ya hapo, tuweze kufanya usanifu wa kina, ili kupata gharama ya utekelezaji wa mradi huo. Tukishapata gharama, ndipo sasa Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza kuutekeleza mradi huo. Ninakushukuru sana.