Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Timida Mpoki Fyandomo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. TIMIDA M. FYANDOMO K.n.y. MHE. LUTENGANO G. MWALWIBA aliuliza: - Je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka vivutio maalumu vya kikodi kwa vijana wanaoanza biashara ili kuchochea ajira na kukuza uchumi?

Supplementary Question 1

MHE. TIMIDA M. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali imepitisha vivutio mbalimbali vya kikodi kama Import Duty Exemption, VAT Exemption, Capital Allowance, lakini pia na kuwapa wafanyabiashara na wawekezaji ndani na nje ya nchi the grace period, je, ni kwa nini Serikali inachelewesha kuwaruhusu au kuwapa muda mwafaka wa kutumia zile incentives ambazo wale wafanyabiashara wanakuwa wanataka kuzitumia na wanaruhusiwa kisheria?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Je, Serikali ina takwimu ya watu wanaonufaika na vivutio hivi vya kikodi? Kama haina, Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha kwamba vivutio hivi haviwanufaishi wachache, bali vinawanufaisha watu wengi wakiwemo vijana? Ahsante. (Makofi)

Name

Mshamu Ali Munde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. ENG. MUSHAMU A. MUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa vivutio vya kodi katika kuvutia uwekezaji wa ndani na nje. Ni kweli pia kuwa hapo awali kulikuwepo na changamoto zilizosababisha ucheleweshwaji wa utoaji wa vivutio hivyo. Changamoto hizo zilihusisha urasimu wa kiutendaji, ucheleweshwaji wa maamuzi, ukosefu wa utaratibu wa kutosha kati ya taasisi mbalimbali pamoja na mkanganyiko wa tafsiri za baadhi ya sheria na hatua za kuchukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kubaini hali hiyo, Serikali imechukua hatua mbalimbali madhubuti kupitia taasisi mbalimbali ikiwemo TISEZA. Sasa hivi angalau kuna one stop centre ambapo wawekezaji wanaweza wakaenda kuwasilisha maombi yao kuhusiana na vivutio stahiki kwenye sekta ambayo wanaenda kuifanyia biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kuna ushirikishwaji mkubwa wa taasisi kama TCCIA ambayo pia tunaitumia kwa ajili ya kuwaelekeza wafanyabiashara vivutio stahiki katika maeneo ambayo wanaenda kuwekeza. Jambo hili inaelekea baada ya hatua hizo linaenda kupungua, na hivyo vivutio vitatoka kwa wakati, hasa kwa startups kama vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusiana na takwimu, Serikali kweli inatoa vivutio hivyo, hususan kwa vijana. Hata hivyo, kwa sasa hatuna takwimu zinazoonesha asilimia ambayo inatupa picha ya wale ambao wamefaidika na vivutio hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vivutio hivyo vimekuwa vikitolewa, lakini mtazamo siyo vivutio, tathmini imekuwa ikitolewa kwa kuangalia mtazamo mpana kuliko kuangalia asilimia ya watu ambao wanafaidika. Kwa mfano, kwa kuangalia ajira na shughuli za kiuchumi katika jamii. Kwa sasa tunafikiri Wizara ya Fedha inaweza ikapata takwimu nzuri zaidi pale ambapo sasa tumeanza kutumia mfumo wa IDRAS ambao unachukua takwimu za walipa kodi wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tuko na utaratibu wa kuwaelekeza, na hapa nielekeze kwa dhati kabisa wenzetu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, waweze kuanzisha utaratibu. Ninajua upo utaratibu wa mafunzo kwa wafanyabiashara, hasa vijana ambao wanaanza biashara kwa sasa, hasa kipindi hiki ambacho Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwawezesha vijana hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipokuwa na takwimu na vijana hawa wasipopata mafunzo stahiki kwa ajili ya kutumia zile fedha, zile fedha zitakuwa kama zile ambazo Wabunge tulikuwa tukilalamikia hapa, kwamba, fedha za 10% ya mapato ya ndani ya halmashauri zimekuwa zikienda na maji bila habari kutokana na vijana kuchukua fedha bila kuwa na maarifa stahiki ya kutumia fedha hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi bilioni 200 lazima zilete tija kwa vijana. Kwa hiyo, nawaambia na kuwahimiza Mamlaka ya Mapato Tanzania, pamoja na jitihada wanazofanya za kuwapa mafunzo na kutoa vivutio hivyo ambavyo nimeviongelea, watoe mafunzo stahiki kwa vijana, ili mwisho wa siku shilingi bilioni 200 zilete tija kwao. Pia, kama tunavyosisitiza, wawe ni wajasirimali ambao wanakuja ku-graduate kuwa wafanyabiashara wakubwa watakaoleta tija na kuinufaisha nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)

Name

Kunti Yusuph Majala

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. TIMIDA M. FYANDOMO K.n.y. MHE. LUTENGANO G. MWALWIBA aliuliza: - Je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka vivutio maalumu vya kikodi kwa vijana wanaoanza biashara ili kuchochea ajira na kukuza uchumi?

Supplementary Question 2

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Mapato (TRA) wamekuwa wakikusanya kodi kwa wafanyabiashara wetu kwa kupitia mtaji, kitu ambacho kinawakatisha tamaa wafanyabiashara walio wengi wakiwemo vijana, lakini pia, Serikali kukosa mapato halisi. Je, Serikali iko tayari sasa kukusanya kodi kwenye faida, ili mfanyabiashara aweze kupata moyo na kulichangia Taifa lake kwenye shughuli za maendeleo?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu kwa ufupi.

NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. ENG. MUSHAMU A. MUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, sijapata swali sehemu ya mwanzo, TRA inafanya utaratibu wa kukusanya kodi kupitia nini?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kunti Majala.

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu linasema, TRA mfanyabiashara anapoenda kuchukua leseni, pamoja na TIN, kodi anayokadiriwa ni pamoja na mtaji wake bila kuangalia kwamba, mtaji ule ameupata wapi? Mitaji mingi ya wafanyabiashara wetu wamekopa. Kwa hiyo, TRA inachukua kodi kulingana na mtaji wa mteja alionao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mathalan Kunti ninaenda kuanzisha biashara ya shilingi 4,000,000, kwa hiyo, TRA inapokuja kuni-charge mimi ina-charge kupitia ile shilingi 4,000,000 na siyo faida iliyotokana na shilingi 4,000,000. Kwa hiyo, swali langu, ninataka kujua Serikali mko tayari kuchukua kodi kwenye faida badala ya mtaji wa mteja? (Makofi)

Name

Mshamu Ali Munde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. ENG. MUSHAMU A. MUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu huo haupo, na ndio maana hata tunavyoongelea Corporate Tax tunaongelea kodi kutoka kwenye faida. Hoja hii ninaichukua kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge, kama kweli kuna matukio ya wafanyabiashara kulipishwa kodi kutoka kwenye mtaji, kwa sababu, kodi haitakiwi kufilisi biashara hiyo, ndiyo hasa mustakabali wa kodi halisi. Kodi inatakiwa ichukuliwe kutoka kwenye faida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyoongelea wajasiriamali wadogo, wao wamekuwa exempted kabisa kutolipa kodi, hasa wale ambao wanazalisha fedha chini ya shilingi 4,000,000. Kwa hiyo, hata wale ambao ni zaidi ya shilingi 4,000,000 kitakachotokea ni kwamba, watalipa kodi kwenye faida wanayozalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema wazi pia, tumezungumzia kwamba, wajasiriamali wadogo wana msamaha wa kulipa kodi, lakini pia, uki-graduate kutoka kwenye msamaha, utapata maelekezo wewe kama mfanyabiashara, ni kwa namna gani unakokotoa faida yako ili ihusishwe kwenye kulipia kodi yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)