Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Timotheo Paul Mnzava
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Korogwe Vijijini
Primary Question
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga Bwawa la Mayuyu na Skimu ya Umwagiliaji - Korogwe Vijijini?
Supplementary Question 1
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kumekuwa na utaratibu mara nyingi wa kufanya usanifu kwa ajili ya mabwawa, lakini baada ya kukamilika usanifu wa mabwawa ndiyo kazi ya ujenzi wa skimu inafuata na jambo hili huwa linachelewesha kazi hizi. Je, Serikali haioni sasa iko haja ya usanifu wa skimu za umwagiliaji na mabwawa haya uende kwa pamoja?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; pamoja na kazi nzuri ambayo Serikali inafanya, lakini iko ahadi ya muda mrefu ambayo ilitolewa na Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu ya ujenzi wa bwawa kwa ajili ya Skimu ya Mombo pamoja na ujenzi wa eneo la Skimu ya Kwamkumbo. Ni lini ahadi hii ya Serikali itatekelezwa?
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Timotheo Mnzava, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, la kwanza, napenda kumpongeza Mheshimiwa Mnzava ni mfuatiliaji mzuri sana wa miradi ya umwagiliaji kwenye jimbo lake, lakini na kwa nchi nzima. Kwa kweli amethibitisha jinsi ambavyo vijana wakiaminiwa wana uwezo wa kufuatilia mambo makubwa kwenye majimbo na kwenye nchi hii, ili Taifa letu liweze kusonga.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na ushauri wake ambao amesema kwamba kwa nini isiende pamoja mambo yote mawili, kwanza nipende kupokea, lakini pili, kupitia Waziri wa Kilimo, nimwombe Mkurugenzi wa Tume ya Umwagiliaji wapokee ushauri huu, uchakatwe na kama utaonekana pengine unaweza kuwa na tija, tuanze kuufanyia kazi kwa sababu lengo letu wote ni kujenga.
Mheshimiwa Spika, la pili, kuhusiana na kufufua Mto Soni, moja nipende kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imekwisha kamilisha usanifu wa miundombinu ya umwagiliaji kwa maana ya Skimu za Mombo pamoja na bwawa. Kwa kuwa tumeshakamilisha, hatua inayofuata ni kuanza manunuzi kwa ajili ya kumpata mkandarasi huyo.
Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge baada ya kumpata mkandarasi huyu, tutakwenda kuanza utekelezaji ili wananchi wake wa Korogwe ambao kimsingi anawapenda sana, waweze kunufaika na miradi hii. Naomba kuwasilisha.
Name
Yahya Ally Mhata
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyumbu
Primary Question
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga Bwawa la Mayuyu na Skimu ya Umwagiliaji - Korogwe Vijijini?
Supplementary Question 2
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, ahsante, katika Jimbo la Nanyumbu, Kata ya Masuguru, kuna Skimu ya Umwagiliaji katika Bwawa la pale Lukula na Kijiji cha Masuguru. Upembuzi yakinifu umefanyika na umekamilika na usanifu wa kina umekwisha. Ni lini sasa ujenzi wa skimu hii utaanza ili wananchi wa kata ile waweze kunufaika na mradi huu?
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mhata, Mbunge wa Nanyumbu kwa swali lake la nyongeza alilouliza kuhusiana na skimu ya wananchi wake.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali hii imetambua umuhimu mkubwa sana kwa maana ya kuboresha skimu za umwagiliaji nchini na ndiyo maana, siyo tu imeongeza bajeti ya kilimo kutoka shilingi bilioni 294 mpaka shilingi trilioni 1.1, lakini pia imeongeza bajeti nzima ya miradi yote inayotekelezwa nchini kama ambavyo kimsingi Mheshimiwa Waziri alizungumza ambapo miradi zaidi ya 886 nchi nzima ipo kwenye hatua mbalimbali, ikiwemo na ile miradi 146 ambayo naamini na ya kwake ni mmojawapo.
Mheshimiwa Spika, nimwombe Mheshimiwa Mbunge awe na subira. Iko miradi ambayo inatekelezwa na kukamilishwa, ipo mingine ambayo tunategemea kwenda kuanza, na ipo mingine tunakwenda kusaini, wakandarasi wanakwenda kusaini, lakini na mingine tunakwenda kuanza hatua za usanifu. Awe na subira, Serikali itakwenda kufikia miradi yote ikiwepo na wa kwake kulingana na upatikanaji wa fedha za Serikali.
Name
Asia Abdulkarim Halamga
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga Bwawa la Mayuyu na Skimu ya Umwagiliaji - Korogwe Vijijini?
Supplementary Question 3
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Skimu ya maji ya umwagiliaji ya Kata ya Endagaw, ina zaidi ya miaka 15. Imetumia fedha za Serikali shilingi bilioni 1.5 na mara ya mwisho mkandarasi ana miaka miwili toka aondoke.
Je, ni lini Serikali itaenda kukamilisha Skimu ya Miradi ya Maji ya Endagaw, na je, Mheshimiwa Waziri uko tayari twende tukakague fedha hizi nyingi za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambazo ametuletea lakini bado hazijaleta matokeo chanya kwa wananchi?
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asia Halamga ambaye anawapigania wananchi wake kuhakikisha kwamba skimu ya umwagiliaji ambayo Serikali imeshaianza inakamilika.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tunayo miradi takribani 71 ambayo ipo kwenye hatua mbalimbali, kuanzia asilimia moja mpaka 99% kuelekea 100%. Naamini mradi huu ni mmojawapo. Hapa nyuma nchi hii imekuwa na mambo mengi ya kufanya na wewe ni shahidi. Tumekuwa na fedha nyingi tumepeleka kwenye SGR ambayo leo Watanzania wananufaika, tumepeleka kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere. Nina uhakika, baada ya kukamilisha miradi hii mikubwa, kasi ya maendeleo kwenye miradi mbalimbali ikiwemo ya maji, ukiwemo huu wa kwako itakwenda kukamilika. Naomba uwe na subira.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na ombi la kuambatana na mimi Mheshimiwa Mbunge kama Mheshimiwa Waziri wa Kilimo asipokuwa na nafasi, yeye au Naibu wake, akanituma mimi nimwakilishi, sitaweza kukataa maelekezo ya Serikali. (Makofi)
Name
Jasmine Chesco Ng'umbi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga Bwawa la Mayuyu na Skimu ya Umwagiliaji - Korogwe Vijijini?
Supplementary Question 4
MHE. JASMINE C. NG’UMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, swali langu ni kuwa; je, ni nini mpango wa Serikali kuhakikisha skimu za umwagiliaji zinafika katika Mkoa wa Iringa, hususani katika majimbo yote saba, ili kuweza kuwasaidia vijana wa Mkoa wa Iringa kujiajiri, lakini pia kulima kilimo cha kisasa? (Makofi)
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, nampongeza Mbunge wa Vijana, Mheshimiwa Jasmine Ng'umbi kwa jinsi ambavyo anawapigania vijana wa nchi hii. Yeye na Wabunge wenzake ambao wanawakilisha vijana hapa Bungeni wamethibitisha umuhimu wa kuwa na vijana makini wanaofuatilia masuala ya maendeleo ya vijana, kwa maslahi ya Taifa leo na kesho.
Mheshimiwa Spika, kwa swali lake ambalo kimsingi anauliza kwa upande wa Mkoa wa Iringa kwamba ni lini skimu hizi zitakamilika.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa katika mkoa wetu wa Iringa, Wizara ya Kilimo inatekeleza miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na uchimbaji wa visima virefu karibu kwenye majimbo yote saba katika mkoa wetu. Pili, tuna miradi takribani 24 ambayo ipo kwenye hatua mbalimbali ya usanifu, lakini tatu, tunayo miradi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Mradi wa Ruaha Mbuyuni, Mradi wa Mgololo, Mradi wa Mkombozi na Miradi mingine, ambayo kimsingi inatekelezwa. Serikali inampa uhakika Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote ambao wanataka kufahamu kuhusiana na Mkoa wa Iringa na maeneo mengine, itakwenda kuongeza kasi kuhakikisha kwamba maeneo hayo, au wananchi wa Mkoa wa Iringa hususani vijana ambao yeye anawawakilisha, wanakwenda kunufaika ili washiriki kwenye uzalishaji, wapate ajira, wajenge uchumi na waweze kusaidia shughuli mbalimbali katika familia zao.
Name
Emmanuel John Khambay
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Babati Mjini
Primary Question
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga Bwawa la Mayuyu na Skimu ya Umwagiliaji - Korogwe Vijijini?
Supplementary Question 5
MHE. EMMANUEL J. KHAMBAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itakamilisha zoezi la upembuzi yakinifu juu ya ujenzi wa bwawa la umwagiliaji katika Kata ya Bagara, hususani eneo la Kijiji cha Nakwa ili wananchi wa eneo hilo waweze kunufaika na kilimo cha umwagiliaji?
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, napenda kujibu swali la nyongeza kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameweza kuuliza kwamba kama nilivyosema hapo awali, nimtoe mashaka Mheshimiwa Mbunge. Kasi ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kwamba, wananchi wake wananufaika na nchi hii na ameamua kukifanya kilimo kuwa uti wa mgongo.
Mheshimiwa Spika, ili kukamilisha hoja hiyo, eneo la umwagiliaji, ambalo wakati anaingia yeye madarakani lilikuwa ni eneo dogo sana la kumwagilia, takribani eneo la hekta laki sita, wakati Mungu ametupa fursa ya eneo lenye ukubwa zaidi ya hekta milioni 40. Ninakuhakikishia Mheshimiwa Mbunge na ukawaambie na wananchi, Waziri wa Kilimo anawaambia, atakwenda kuwafikia maeneo yote ambayo ni ya kimkakati ili wananchi waweze kuzalisha na tuweze kuuza nje ya nchi na ndani ya nchi chakula pamoja na mazao mbalimbali.