Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Martha Nehemia Gwau
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MARTHA N. GWAU aliuliza:- Je, lini Serikali itaweka Sheria ya Ugatuzi wa Madaraka kwa Serikali za Mitaa kama hatua ya kutekeleza Dira ya Taifa ya 2050?
Supplementary Question 1
MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, tunaenda kwenye utekelezaji wa Dira yetu ya mwaka 2050. Je, Serikali za Mitaa zimeanzishwa muda mrefu takribani miaka 44. Sasa kama hauna sera na sheria mpaka sasa uwepo wa mamlaka hizi unatekelezwa kwa utaratibu gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tunatambua kuna mifumo mbalimbali na kuna aina mbalimbali za uendeshaji wa Serikali za Mitaa. Je, sera inayopendekezwa ya mwaka 2016 itakuwa na mfumo upi? Ninashukuru. (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tunazo mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo zinafanya kazi kwa muda mrefu na kwa kweli zimeendelea kufanya kazi kwa ufanisi mzuri kabisa kutoa huduma, kusimamia miradi ya maendeleo na zinaendelea kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetambua kwamba pamoja na kwamba mamlaka hizi zinafanya kazi vizuri kupitia miongozo na sheria mbalimbali, lakini tuna kila sababu ya kuwa na sera mahususi ambayo itakwenda kuzisimamia zaidi shughuli za ugatuzi wa madaraka ili kuzipa nguvu zaidi halmashauri zetu lakini pia na kuweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, pamoja na kwamba kwa sasa tuna miongozo, sheria na taratibu ambazo zinawezesha halmashauri zetu kufanya kazi, kazi zinakwenda vizuri bila changamoto yoyote. Kinachofanyika sasa ni kutunga sera rasmi ili kuwezesha sasa suala la ugatuzi wa madaraka na majukumu ya mamlaka zetu kuwa wazi zaidi, lakini pia kufanyika kwa ufanisi mkubwa zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu sera hii ambayo inatarajiwa kuandaliwa ya mwaka 2026, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge, mara sera itakapokuwa imeandaliwa, tutaleta kwa Waheshimiwa Wabunge kwa namna yoyote ili waweze kuiona content yake ikoje, lakini inapanga kufanya jambo gani ili kuboresha sera hiyo, lakini pia kuhakikisha kwamba inakuwa na tija inayotarajiwa, ahsante. (Makofi)
Name
Boniphace Mwita Getere
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Primary Question
MHE. MARTHA N. GWAU aliuliza:- Je, lini Serikali itaweka Sheria ya Ugatuzi wa Madaraka kwa Serikali za Mitaa kama hatua ya kutekeleza Dira ya Taifa ya 2050?
Supplementary Question 2
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Huko nyuma kulikuwa na miongozo na taratibu mbalimbali za kurudisha mapato ya Serikali za Vijiji kwenye maeneo yao na kwa sheria ya mwaka 1982 Sheria Namba Nane na Namba Saba wanasema kijiji kinapata asilimia tatu, kata inapata asilimia nne na kitongoji 13%, lakini kumekuwepo na maeneo ya minada, kama Mnada wa Mgeta na maeneo mengine Serikali za Mitaa hazirudishi mapato kwenye maeneo hayo. Ni lini Serikali itaweka utaratibu wa mapato hayo yarudishwe kwenye maeneo yao? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iliweka sheria, taratibu, miongozo na nyaraka mbalimbali kuzielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa kurudisha sehemu ya makusanyo ya mapato ya ndani kwenye vijiji ambavyo vimekusanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili linaendelea kutekelezwa, lakini ni kweli kwamba ufanisi wake siyo mkubwa kwa kiwango kinachotakiwa. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kwanza niwasisitize, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri, TAMISEMI, Wakurugenzi wote Mamlaka za Serikali kuhakikisha wanazingatia utekelezaji wa sheria hiyo ambayo inaelekeza sehemu ya mapato ya ndani kurejeshwa kwenye vijiji ili kuweza kusaidia shughuli za maendeleo na za kijamii katika maeneo hayo na sisi Ofisi ya Waziri Mkuu tutasimamia suala hilo kwa karibu ili kuhakikisha kwamba sheria hiyo inazingatiwa ipasavyo. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved