Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Marirta Gido Kivunge

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARIRTA G. KIVUNGE aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa Miradi ya Maji iliyosimama kwenye Halmashauri za Wilaya ya Meru, Longido na Monduli?

Supplementary Question 1

MHE. MARIRTA G. KIVUNGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Serikali imekiri miradi hiyo imesimama. Je, haioni haja ya kutoa fedha za dharura kwa ajili ya kukamilisha miradi hii, ikiwemo Miradi ya Sepeko, Meserani Wilayani Monduli na Miradi ya Maji ya Chai, Kikatiti, Wilayani Arumeru na Mradi wa Maji Tingatinga, Wilayani Longido?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Ni nini mpango wa Serikali, Mkoani Arusha, kuwapatia mipango ya kuchimba visima na mabwawa, hususan kwenye Wilaya kame za Monduli, Longido na Ngorongoro, kwani mtambo mmoja uliotolewa hautoshelezi?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, niruhusu nimpongeze Mheshimiwa Marirta Gido Kivunge, kwa kuendelea kuwasemea wananchi wa Mkoa wa Arusha, hasa akinamama. Pia, ninampongeza sana kwa kushirikiana na Wabunge wa Majimbo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona katika swali lake la nyongeza amegusa karibia majimbo matatu, kwa Mheshimiwa Isack Copriano, kwa Mheshimiwa Nassari pale na naona amegusa kwa Mheshimiwa Dkt. Kiruswa. Maeneo haya yote tumeyaona na kwamba, hata kwenye ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mbunge alisimama na kuonesha umahiri kabisa kuwasemea wanawake wa Mkoa wa Arusha. Kwa hiyo, ninampongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muktadha huo, tunayo mambo matatu, miradi karibia mitatu. Mradi wa Vijiji 13 kutoka Ngaramtoni kwenda Monduli, una gharama ya shilingi bilioni 20.3 ambapo Mheshimiwa Copriano ni shahidi. Serikali tayari tumeingia tripartite kati ya Serikali, Pipe Industry pamoja na mkandarasi, ambaye ni Jandu Plumbers, ambapo sasa tumekubaliana kwamba, waanze kuzalisha mabomba ya chuma. Lengo ni kwamba, mradi usisimame.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge tulimwalika akaenda kukagua mabomba, na yeye tunamwalika, akipata nafasi akashuhudie mabomba ambayo yataenda kulazwa kutoka Ngaramtoni mpaka maeneo ya Monduli. Kwa hiyo, mradi huo umeshafikia asilimia nzuri kabisa ya utekelezaji wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, Mradi wa Kikatiti, kwa Mheshimiwa Nassari pale, wenye gharama ya shilingi bilioni nne, mpaka sasa mradi huu umefikia 40% ya utekelezaji wake na mkandarasi yuko site anaendelea na kazi. Mradi huu unatakiwa kukamilika Disemba, 2026. Kwa hiyo, tunaamini kwamba, tuko ndani ya muda.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ameongelea kuhusu eneo la Tingatinga, kwa Mheshimiwa Kiruswa kule. Eneo hili mradi huu umefikia 56%.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua tunaye Mkandarasi anaitwa Serengeti, kidogo alisuasua japo amelipwa fedha, tumeshamwandikia barua ya onyo ili ahakikishe kwamba anaongeza speed ili mradi huu uweze kukamilika kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, katika maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge amegusia kuhusu Halmashauri kame, tunayo mitambo ya aina mbili. Tunayo mitambo ya kuchimba visima ambayo ni seti 26 ambazo Rais alinunua, na pia tunayo mitambo ya kuchimba mabwawa. Mitambo hiyo imeshaanza kufanya kazi na hata Monduli kuna bwawa ambalo limetumia mitambo ya Rais, ile seti ya kuchimba mabwawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunapokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge, tutaendelea kuhakikisha kwamba kwenye programu ya vijiji 1,575 mitambo hii ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliinunua kwa dhamira ya kumtua mama ndoo kichwani, tunaenda kusimamia utekelezaji wake ili wananchi wa Mkoa wa Arusha ambao yeye amekuwa sauti yao pamoja na Wabunge wote, tutahakikisha tunawapelekea neema ya tabasamu ambayo Rais aliahidi kwa Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)