Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Yustina Arcadius Rahhi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. YUSTINA A. RAHHI aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua mashamba yaliyokuwa ya ngano nchini ili kuweza kukidhi mahitaji ya ngano nchini?

Supplementary Question 1

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana. Ingawa leo ni mara yangu ya pili nauliza swali kuhusu kufufua mashamba yaliyokuwa yanazalisha ngano, lakini ninaishukuru sana Serikali kwa majibu mazuri. Sasa nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza. Kwa kuwa, ngano inaonekana ni moja ya mazao muhimu ya chakula nchini na tunahitaji takribani tani 1,000,000 kwa mwaka na uzalishaji wetu wa ndani ni chini ya tani 200,000, kwa maana hiyo karibu 90% ya ngano tunaagiza nje kwa fedha za kigeni; sasa pamoja na mikakati mizuri ambayo Serikali imetueleza, haioni sasa umuhimu wa kuifanya ngano kuwa moja ya mazao ya mkakati nchini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Wakati wa ziara ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkoa wa Manyara, Wilayani Hanang’, tarehe 3 Oktoba, 2025 aliwaahidi Wanahanang kupitia upya mikataba ya wawekezaji katika mashamba ya ngano ili kubaini changamoto na wale ambao hawaendelezi wachukuliwe hatua. Je, ni lini ahadi hii ya Rais itatekelezwa? Ahsante sana. (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Yustina Rahhi kwa maswali mazuri ya ngano, bahati nzuri amekuwa ni mfauatiliaji mzuri hata kuanzia katika level ya Kamati.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo moja tu ambalo ninaweza kumweleza yeye na wakulima wa ngano kwamba Serikali imeweka miongoni mwa mazao ya kimkakati ambayo tunakwenda kutekeleza katika mwaka huu wa fedha 2026/2027 ambao ndiyo tunaendelea kuupitisha hapa, ni pamoja na zao la ngano. Kwa hiyo, tayari tumeshaliweka katika bajeti, na yale mazao manne ambayo mwaka 2026 tutayapa msukumo mkubwa, ngano ni miongoni mwake.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wetu wa kwanza ni kweli tutazalisha kama wastani wa tani 110,000, tunataka katika mwaka huu wa kwanza tufikishe walau tani 200,000 na tutaendelea kutoa ikiwemo mbegu za ruzuku bure katika maeneo yale ambayo wanazalisha ngano.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tutaainisha maeneo mapya yakiwemo maeneo ya Njombe, Iringa na tutafanya tafiti katika maeneo ya Tanga na Morogoro ili kuongeza eneo ambalo litafaa kwa ajili ya uzalishaji wa ngano. Kwa hiyo, lipo na tumelipa kipaumbele kikubwa ikiwemo katika bajeti hii ambayo tunakwenda kuipitisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuhusu maelekezo ya Rais, ndiyo maana nimeeleza katika jibu la msingi tunaendelea na tathmini na tukishamaliza tutatoa majibu na tutafikisha vilevile kwa wananchi. Ahsante.

Name

Kenneth Ernest Nollo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Primary Question

MHE. YUSTINA A. RAHHI aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua mashamba yaliyokuwa ya ngano nchini ili kuweza kukidhi mahitaji ya ngano nchini?

Supplementary Question 2

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa mwaka wa 2025 nchi yetu imeagiza ngano kiasi cha shilingi milioni 377 ambayo ni sawa na shilingi bilioni 980. Je, Serikali ina mpango gani wa kuondoa kodi kwenye mashine na increment zote zinazotumika kwenye zao la ngano ili kuweza kuchochea wawekezaji hawa kuweza kulima kwa urahisi? Yaani kufuta kodi zote kwenye mashine ambazo zinatumika kwenye kilimo cha ngano.

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nimshukuru kaka yangu, Mbunge wa Jimbo la Bahi kwa swali lake. Nimwammbie tu jambo moja, moja ya jitihada ya kwanza ya Serikali kwa sasa ni kuongeza tija kwa maana ya uzalishaji, halafu baada ya hapo ndiyo nafikiri hatua inayofuatia itakuwa ni hiyo kusaidia watu ambao wataleta viwanda ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tunaagiza ngano, tunaweza tukasema karibia 95% ya ngano yote inatoka nje kwa sababu uzalishaji ndani ni mdogo sana. Kwa hiyo, kuhusu kupunguzwa kwa kodi maana yake Wizara ya Fedha wanaweza wakalipokea hilo jambo na kuangalia namna bora ambayo itaweza akasaidia katika nyakati zijazo. Ahsante sana.