Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Primary Question

MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza:- Je, lini barabara ya Mlowo – Kamsamba itaanza kujengwa kwa kuwa ni zaidi ya mwaka tangu mkandarasi asaini mkataba?

Supplementary Question 1

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Nimeyasikia majibu ya Mheshimiwa Waziri Mzee wangu, kutoka kule Songwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2025 mwezi wa Tatu, Naibu Waziri kwa kuongozana na wataalam kutoka TANROADS alifika kwenye Jimbo la Momba na Jimbo la Mbozi na kusaini mkataba mbele ya wananchi wa Majimbo hayo mawili, na tukafanya sherehe kubwa sana kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo kilomita tano kama ambavyo amesema Momba na Mbozi.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tena kwenye majibu yake ya msingi Mheshimiwa Waziri, Mzee wangu anasema bado wapo kwenye hatua za kumtafutia mkandarasi fedha. Kwa heshima na unyenyekevu mkubwa, aseme hapa ya matumaini, wananchi wa Momba, Mbozi na Songwe wanamsikia? Ni lini mkandarasi ataanza kutekeleza barabara hii kwa kiwango cha lami, kwa hizo kilomita tano tu ambazo alituahidi? (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge rudia swali, Waziri hajasikia.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, hajasikia?

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge samahani. Waheshimiwa Wabunge, mkipiga makofi ya kutosha, Naibu Waziri hatasikia swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mbunge endelea.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, amesikia au nirudie?

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, umesikia?

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mzee, umesikia au nirudie?

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikia.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naenda swali la pili. Barabara ya Kakozi - Ilonga ambayo inapita kwenye Vijiji vya Chisitu, Chipumpu, Kapele na Mchinga kuelekea Tunduma ambako wananchi wanajipatia mahitaji yao ya msingi, imeharibika sana na inachukua karibu masaa 12 ili waweze kupata huduma hizo, wakati ni kwa mwendo wa masaa manne. Vilevile, barabara ya kutoka Vwawa kupita Isalalu, Msangano mpaka Chitete na yenyewe imeharibika sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni ipi kauli ya Mheshimiwa Waziri kumwelekeza TANROADS wa Mkoa aweze kufanya maboresho ili wananchi wasiendelee kulala njiani kwa barabara ya masaa manne tu kufika mjini? Ahsante.

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tulishasaini mkataba wa kujenga barabara ya Mlowo - Kamsamba kilomita kumi, kuanzia upande wa Mlowo na kuanza upande wa Kamsamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, pia na wananchi wa Jimbo la Momba kwamba, kwa hatua tu hizo kupata Mkandarasi na kusaini ni kuonyesha kwamba Serikali imedhamiria kuijenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami na ndiyo maana tumesema tumeshaanza kwa awamu. Pia, Mheshimiwa Mbunge akumbuke tuna madaraja ambayo yalikuwa na changamoto, na ambayo yalikuwa ni kikwazo kikubwa, tumeendelea kuyajenga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama nilivyosema katika jibu la msingi, bado mkandarasi yupo, na Serikali inajipanga kupata fedha ili tuweze kuanza kujenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami kama ambavyo tulikuwa tumeahidi kwenye mkataba; na kama tulivyokubaliana na mkandarasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili ambalo ametaja barabara kama mbili au tatu, ninadhani hili ni suala tu la utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumwelekeza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Songwe kwamba nina uhakika mvua zimeshaanza kupungua na wakandarasi ambao walikuwa wamepewa kazi ya kuhakikisha kwamba wanakwamua maeneo yote yaliyokwama, basi ahakikishe kwamba wanapelekwa katika barabara hizi na kurekebisha barabara hizo, ambapo tayari msimu wa mavuno umeanza, wasiweze kukwama; aweze kuwaelekeza hao wakandarasi wakakwamue maeneo yote yaliyokwama na wananchi waendelee kupata huduma.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, ahsante sana kwa majibu ya maswali ya Waheshimiwa Wabunge. Tunaendelea na Wizara ya Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Asia Abdulkarim Halamga, Mbunge wa Hanan’g sasa aulize swali lake.