Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Asia Abdulkarim Halamga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza: - Je, lini Serikali itaanzisha kiwanda cha kuchakata mazao katika Jimbo la Hanang?

Supplementary Question 1

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa ni agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba kila wilaya kuanzishwe kongani ya viwanda ili kuweza kukuza thamani ya mazao ya wananchi na pia kupata masoko ya uhakika, na kwa kuwa, wananchi wa Jimbo la Hanan’g tayari Mheshimiwa Waziri katika jibu la msingi anaona namna gani ambavyo wamejikongoja wao wenyewe kuweza kuweka viwanda, je, Serikali haioni haja sasa ya kuanzishwa kwa kongani ya viwanda kwa Jimbo la Hanan’g?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili. Kwa kuwa Wilaya ya Hanan’g, Kata ya Gendabi tunazalisha zaidi ya tani 100,000 ya chumvi, na jambo hili nimeshaliongelea hapa mara kadhaa, pia katika kata nyingine tunazalisha tani 30 mpaka tani 40, je, Serikali haioni haja sasa ya kuweza kutupatia vifaa vya uchimbaji ili tuweze kuchimba kisasa na tuzalishe zaidi ya hizi tani nilizozitaja?

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali haioni haja ya kutuongezea na kututafutia wawekezaji wa uhakika ili rasilimali hii muhimu iweze kutoa ajira kwa wanahanang, na pia kuliingizia Taifa mapato kwa maana ya fedha za ndani na fedha za kigeni?

Name

Dr. Pius Stephen Chaya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Asia Abdulkarim Halamga, Mbunge wa Jimbo la Hanang kwa kuwatetea wananchi wake wa Jimbo la Hanang, hususan kuhusiana na suala la kuanzisha viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Mheshimiwa Rais alituelekeza, na hata alipokuja hapa kuzindua Bunge na katika zile ahadi zake za siku 100 mojawapo ya ahadi ambayo aliitoa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha tunaanzisha kongani za viwanda kila wilaya. Lengo ni kuhakikisha tunasogeza huduma za uzalishaji karibu na wananchi, hususan wakulima wakiwemo wakulima wa Hanang. Sisi kama Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara tumeshaanza huu mchakato kwa kushirikiana na wenzetu wa TAMISEMI.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekwishatoa maelekezo, na sasa hivi tunaandaa mwongozo wa Kitaifa wa usimamizi wa kongani za viwanda. Nina uhakika ifikapo mwaka huu tunapoanza utekelezaji wa Dira 2050 tutahakikisha sasa kila wilaya ikiwemo Wilaya ya Hanan’g inakuwa na kongani ya viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa taarifa yako, tayari Wilaya ya Hanan’g wameshatenga zaidi ya ekari 50 ambazo wametenga kwenye hii bajeti kwa ajili ya kuanzisha kongani za viwanda. Lengo ni kuhakikisha kwamba, tunaweka mazingira rafiki tunapovutia wawekezaji kwenye viwanda mbalimbali vya ngano, dengu na kadhalika, wawe na maeneo ambayo wanaweza kuweka viwanda vyao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali la pili. Ni kweli Hanang ni mojawapo ya maeneo ambayo kuna deposit za chumvi, kuna mashapo ya chumvi. Niseme kwamba tunahitaji kujiridhisha zaidi kabla hatujatangaza kama ni eneo potential kwa ajili ya uwekezaji, kwa sababu tunapotaka kuwavutia wawekezaji wakubwa lazima tufanye utafiti tujue concentration ya ores za salt kwenye yale mashapo ili tujue kwa kiasi gani tunaweza tukawaita wawekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa hivi kwa kupitia Shirika la SIDO tumeendelea kuwasaidia wachimbaji wa Hanang. Mheshimiwa Mbunge ameomba tuendelee kuwasaidia, ninaomba nilipokee hili. Sisi kama Wizara ya Viwanda na Bishara tutahakikisha tunaendelea kuwasaidia wachimbaji wadogo wa chumvi kwa kupitia SIDO ili wakuze kipato chao.