Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Mjini
Primary Question
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:- Je, Serikali imejipangaje kumaliza tatizo la matundu ya vyoo katika halmashauri nchini?
Supplementary Question 1
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, Mheshimiwa Waziri ameshafanya tathmini ya kujua ukubwa wa tatizo la matundu ya vyoo katika shule za msingi na sekondari kwa nchi nzima na kupanga mkakati wake? Ninataka nijue, ni sahihi katika karne ya sasa Wabunge wa Tanzania, kuendelea kujadili na kuuliza maswali kila mwaka ya matundu ya vyoo, meza na viti na watoto kukaa nchini? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumhakikishia Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara kwamba Serikali inatambua umuhimu wa shule zetu zote kuwa na matundu ya vyoo yanayotosheleza na yenye viwango na ubora unaotakiwa katika kuhakikisha kwamba watoto wetu wanasoma katika mazingira bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kila mwaka tumekuwa tukifanya tathmini ya matundu ya vyoo yaliyopo, upungufu na kuweka mikakati katika kila bajeti kutenga fedha kupitia mapato ya ndani ya halmashauri na pia kupitia Serikali Kuu kwa ajili ya kujenga matundu ya vyoo. Kwa hiyo, tuna tathmini ya kila mwaka, tunajua kiasi gani tunayo, kiasi gani tunahitaji na Serikali imeendelea kutenga fedha na kujenga ili kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, ni dhamira ya Serikali kwamba tuondokane na changamoto ya matundu ya vyoo kabisa na ndiyo maana tumeendelea kutenga fedha kila mwaka. Kwa mujimu wa taarifa za Benki ya Dunia ambayo assessment imefanyika hivi karibuni, tunahitaji kwa ujumla katika shule yenye wanafunzi 400 tunahitaji wastani wa matundu ya vyoo 12 (sita ya watoto wa kike na sita ya watoto wa kiume) na sisi kwa kiasi kikubwa baadhi ya shule tumeshazidi kiwango hicho. Kwa hiyo, tutaendelea kuhakikisha tunaboresha kwenye yale maeneo mengine ambayo yana uhitaji huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kuhakikisha tunajenga matundu ya vyoo, lakini zoezi hili ni endelevu kwa sababu tutaendelea kujenga shule, population ya watoto itaendelea kuongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hakuna siku tutasema tumemaliza, hatujengi vyoo kabisa, kwa sababu population ipo na shule zitaendelea kujengwa na zitahitaji kujenga vyoo. Kwa hiyo, ni zoezi endelevu. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba zile shule ambazo zina upungufu tunaondokana na changamoto hiyo. (Makofi)
Name
Husna Juma Sekiboko
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:- Je, Serikali imejipangaje kumaliza tatizo la matundu ya vyoo katika halmashauri nchini?
Supplementary Question 2
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa maelezo ya Serikali yanaonesha kwamba wana dhamira ya dhati ya kumaliza tatizo la matundu ya vyoo na kwa sababu shule zilizopo vijijini ndio ambazo zina tatizo kubwa la upungufu wa matundu ya vyoo, je, Serikali ipo tayari itakapoanza kumaliza tatizo hili, kuanza na shule za vijijini hasa katika Mkoa wa Tanga, Wilaya ya Kilindi, Korogwe Vijijini na Lushoto? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali iko tayari kuhakikisha kwamba tunatoa kipaumbele kwenye maeneo ambayo yana shule zenye upungufu mkubwa zaidi wa vyoo zikiwemo halmashauri za vijijini hasa Halmashauri ya Lushoto katika Mkoa wa Tanga.
Name
Ester Amos Bulaya
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:- Je, Serikali imejipangaje kumaliza tatizo la matundu ya vyoo katika halmashauri nchini?
Supplementary Question 3
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, ninatambua Serikali yetu ni namna gani ambavyo inajenga shule kwenye maeneo mbalimbali primary schools na sekondari, lakini tunapozungumzia mkakati maalumu wa kujenga matundu ya vyoo ni pamoja na shule zile chakavu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, crisis hii ni kubwa kwenye halmashauri zetu. Waziri alikuja na mpango wa kuhakikisha wanaandika andiko kwa ajili ya maintenance kwenye shule chakavu. Serikali haioni kwamba ni wakati mwafaka sasa hili tatizo la matundu ya choo kukawa kuna mkakati mahususi ili tumalize tatizo hili kwenye nchi yetu? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli, wazo la Mheshimiwa Mbunge ni zuri na tunalipokea. Kama ambavyo iliwasilishwa kwenye bajeti yetu ya Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ule mpango mkakati ambao umewasilishwa Ofisi ya Mipango kupitia Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji ni inclusive na miundombinu yote ambayo inatakiwa kwenye shule. Kwa hiyo, vyoo pia vitakuwa sehemu ya miundombinu ambayo itaboreshwa. Pia suala la kuwa na mpango mkakati ni wazo zuri, tunalichukua kuhakikisha kwamba, tunaboresha vyoo katika nchi yetu.
Name
Yustina Arcadius Rahhi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:- Je, Serikali imejipangaje kumaliza tatizo la matundu ya vyoo katika halmashauri nchini?
Supplementary Question 4
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, Serikali inapojenga vyoo katika shule za msingi na sekondari, ina mpango gani wa kutenga eneo maalum linaloweza kuwapa faragha watoto wa kike, kwa mfano wanapoweza kubadilisha taulo za kike? Ahsante.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, katika michoro yetu ya ujenzi wa miundombinu hiyo ambayo imeendelea kutolewa katika shule zetu, eneo maalum limeendelea kupewa kipaumbele na ziko baadhi ya shule wameanza ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninatumia nafasi hii kuwakumbusha Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini kwamba, pale tunapojenga miundombinu hiyo katika shule ambazo zina watoto wa kike, ni muhimu kuwa na eneo maalum kwa ajili ya huduma hiyo muhimu.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved