Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Soko la Kisasa la Machinga katika Jimbo la Tabora Mjini?

Supplementary Question 1

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, ninatoa masikitiko yangu kwa majibu ya Serikali kuhusiana na suala zima la Soko la Machinga katika Jimbo la Tabora Mjini. Suala hili siyo la leo na wala siyo la Mkataba wa 2025 - 2030. Suala hili limefuatiliwa na wameona ni namna gani wafanyabiashara wadogo wadogo kwenye Jimbo la Tabora Mjini wanavyofanya biashara kwenye mazingira ambayo siyo rafiki kwao.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Serikali inasema kwamba, ndiyo kwanza wanakwenda kufanya upembuzi yakinifu. Hawawatendei haki wafanyabiashara wadogo wadogo wa Jimbo la Tabora Mjini kwa sababu, tayari Serikali iliahidi humu Bungeni ujenzi wa Soko la Machinga.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka kufahamu hapa, na wananchi wa Tabora wapo kwenye runinga wasikie, ni lini Soko la Machinga, Jimbo la Tabora Mjini, litaanza ujenzi wake? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili. Uchumi wa wananchi wa Tabora unategemea kilimo pamoja na biashara ndogo ndogo. Wafanyabiashara hawa hawana mazingira rafiki kwa biashara zao. Serikali iliahidi katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwamba, watajenga Soko la Machinga haraka iwezekanavyo. Ninataka kufahamu, baada ya uchaguzi, lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa soko na siyo upembuzi yakinifu?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, ninawapongeza Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, kwanza kwa dhamira yao ya kujenga Soko la Machinga. Ikumbukwe kwamba, maandalizi ya design, michoro na eneo la ujenzi ni jukumu la Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, tuliwaelekeza na wameandaa mpango mkakati wa miaka mitano ambao una miradi kadhaa, ikiwemo Soko la Machinga la Manispaa ya Tabora, na tunafuatilia kwa karibu kuona wanakamilisha usanifu na michoro na kuiwasilisha Ofisi ya Waziri Mkuu, ili sisi tuipitie na kuridhia na ujenzi uweze kuanza mapema iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Manispaa ya Tabora, wamepanga kwenye mipango yao kuanza mwaka wa fedha 2027/2028, lakini kwa sababu ya uhitaji wa soko hilo, tutawaelekeza waweze kuanza mapema zaidi mwaka huu wa fedha, ili kuweza kufikisha huduma hizi muhimu kwa wananchi wa Tabora. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mwaifunga, Serikali hii inatambua umuhimu na ndiyo maana tumewaelekeza na wataleta maandiko hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuko tayari hata wakileta leo kufanya tathmini kwa ajili ya kuanza hatua mbalimbali za ujenzi, kwanza, kupitia mapato ya ndani ya manispaa. Pili, halmashauri tayari imetenga, katika mwaka ujao wa fedha, shilingi milioni 150 kwa ajili ya soko hilo. Kwa hiyo, ninamhakikishia tu Mheshimiwa Mbunge, tutasimamia suala hilo na tutahakikisha kwamba soko hilo la Machinga linajengwa. Ahsante.

Name

Bahati Keneth Ndingo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mbarali

Primary Question

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Soko la Kisasa la Machinga katika Jimbo la Tabora Mjini?

Supplementary Question 2

MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Mkakati uliopo kwenye ilani yetu ni kutujengea soko kubwa la Kimataifa la zao la mpunga ndani ya Jimbo la Mbarali. Lini mkakati huo utaanza ili wakulima wa Mbarali waweze kupata soko la uhakika la zao lao la mpunga?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, uko mpango wa Serikali wa kujenga masoko ya kimkakati katika maeneo mbalimbali, ikiwemo katika Jimbo la Mbarali. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, mipango mikakati iko katika hatua mbalimbali; kwanza mingine iko kwenye maandiko ngazi ya halmashauri, mingine iko ngazi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI na mingine iko ngazi ya Wizara ya Fedha. Kwa hiyo, tutahakikisha pia, tunafuatilia hatua za utekelezaji wa soko hilo ili liweze kujengwa katika eneo ambalo limepangwa.

Name

Amosy William Maganga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Primary Question

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Soko la Kisasa la Machinga katika Jimbo la Tabora Mjini?

Supplementary Question 3

MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Mji wa Sikonge ni miongoni mwa miji mikongwe sana katika Taifa letu, lakini umekuwa hauna soko kwa muda wote huu, na kwa vile katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi wameahidi kujengewa soko hilo, je, Serikali ni lini sasa itaanza ujenzi wa soko hilo katika Mji wa Sikonge?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ninatumia nafasi hii kuwakumbusha Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini kwamba, katika mipango yao ya kila mwaka ni muhimu kuainisha vipaumbele ambavyo ni mahitaji ya juu ya jamii katika maeneo yao, yakiwemo masoko.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba, Halmashauri ya Sikonge ni halmashauri kongwe na inahitaji kuwa na soko zuri ambalo litakidhi mahitaji ya wananchi wa Sikonge. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Maganga, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, namwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Sikonge kwanza wafanye tathmini ya gharama zinazohitajika katika ujenzi wa soko hilo, waainishe eneo, na pia, waanze kutenga fedha za mapato ya ndani kwa awamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ikihitajika Serikali Kuu kuunga mkono, tutaunga mkono wakileta andiko hilo. Lengo ni kuhakikisha kwamba, soko hilo linajengwa.

Name

Tinnar Andrew Chenge

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Soko la Kisasa la Machinga katika Jimbo la Tabora Mjini?

Supplementary Question 4

MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Bariadi ni Makao Makuu ya Mkoa wa Simiyu, na kwa kuwa, mji huu unakua kwa haraka sana, je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga soko kwa maana ya Machinga Complex kwa ajili ya wajasiriamali wa Mkoa wa Simiyu?

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, mkipiga makofi kabla Mbunge hajauliza swali, Mheshimiwa Waziri hawezi kusikia. Kwa hiyo, Mheshimiwa Tinnar ninaomba urudie swali lako.

Waheshimiwa Wabunge tuwe wavumilivu. Tupige makofi baada ya majibu.

MHE. TINNAR A. CHENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Bariadi ni Makao Makuu ya Mkoa wa Simiyu, na kwa kuwa mji huu unakua kwa kasi sana; je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga soko, kwa maana ya Machinga Complex, kwa ajili ya wajasiriamali wa Mkoa wa Simiyu?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji wa Bariadi kwanza ni miongoni mwa halmashauri ambazo ziko kwenye Mpango wa TACTIC. Ninafahamu kwamba, soko la pale Mjini Bariadi limeingizwa kwenye Mpango wa TACTIC na hatua zimeanza kutekelezwa. Kwa hiyo, pale litajengwa soko la kisasa sana kwa ajili ya Halmashauri ya Mji wa Bariadi ambapo ni Makao Makuu ya Mkoa wa Simiyu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumepokea ombi la Mheshimiwa Mbunge la kuhitaji kujenga Machinga Complex. Tutafanya tathmini na kuona uwezekano wa kufanya hivyo.

Name

Yahya Ally Mhata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Primary Question

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Soko la Kisasa la Machinga katika Jimbo la Tabora Mjini?

Supplementary Question 5

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Jimbo la Nanyumbu halina soko. Mahali ambapo soko lipo ni viwanja vya watu binafsi. Sasa ninaomba kuuliza, ni lini Serikali itatuletea fedha, ili tujengewe soko la kisasa, kama lilivyoainishwa katika mchoro ambao tumeuleta Wizarani na usanifu na kila kitu kimefanyika?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba, halmashauri zetu, na hususan maeneo ya miji, tunakuwa na masoko yanayokidhi mahitaji. Ninatumia nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali itafuatilia kupitia Halmashauri ya Nanyumbu kuona watafute kwanza eneo kwa sababu, eneo linalotumika, kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, siyo eneo la Serikali. Ni muhimu halmashauri wapate eneo lao na tuweke mipango endelevu ya kujenga soko kwa ajili ya huduma za wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tulifuatilie suala hili. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nanyumbu tunamwelekeza aanze mchakato huo mapema iwezekanavyo ili Serikali iweze kuona namna ya kushirikiana na mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo.

Name

Fagason Aron Nkingwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbogwe

Primary Question

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Soko la Kisasa la Machinga katika Jimbo la Tabora Mjini?

Supplementary Question 6

MHE. FAGASON A. NKINGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niulize swali dogo la nyongeza. Jimbo langu la Mbogwe lina kata 17, lakini zipo kata tatu ambazo hazina masoko ya kisasa nazo ni Kata ya Masumbwe, Nyakafulu na Lulembela. Je, ni lini Serikali ina mpango wa kuja kuweka soko la kisasa katika kata hizi tatu? Ahsante.

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, zipo Kata ambazo zina idadi kubwa ya wananchi na zina uhitaji wa masoko kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Mbogwe amezitaja. Ninaomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tunaendelea kwa awamu na tunafahamu safari ni hatua, kata hizo zinahitaji masoko. Tutaendelea kutenga fedha ili kuhakikisha kwamba tunajenga masoko hayo kwa awamu. (Makofi)