Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Primary Question

MHE. ANNE K. MALECELA aliuliza: - Je, lini barabara ya Hedaru - Mamba Vunta yenye Km 42.44 itaboreshwa ili kuokoa uchumi wa Wananchi wa Kata ya Mamba Vunta?

Supplementary Question 1

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alipokuja Same tarehe 30 Septemba, 2025 alisema maneno haya, “kwa kuwa najua barabara za kule mlimani Tarafa ya Mamba mvua zinaponyesha mnashindwa kusafirisha tangawizi, tunakwenda kuzijenga barabara hizo kwa zege na lami.”

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali haioni baada ya Rais kutoa ahadi hii, ni vyema sasa wakati sisi wananchi tunasubiri ujenzi mkubwa wa lami na zege, ikajengwa barabara hii yote kutoka Hedaru – Vunta mpaka Mamba kwa kiwango cha changarawe ili barabara hii iweze kupitika kwa miezi yote 12.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Hapa ninapoongea, niliposimama, barabara ile sehemu ya Kata ya Mpinji haipitiki kabisa. Kwa hiyo, malori mengi yapo pale yanatafuta njia ya kupeleka tangawizi tambarare. Je, Serikali haioni ni vema sasa ikafanya jambo la dharura tu kwenda kutengeneza ile barabara pale Mpinji ili kuboresha uchumi wa wananchi wangu? Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie mama yangu, Mheshimiwa, Anne Kilango Malecela kwamba Serikali inaitambua sana barabara hiyo na ndiyo maana katika kila mwaka wa fedha imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya ujenzi na kuhakikisha kwamba inapitika, kwa sababu ni barabara muhimu ya shughuli za kiuchumi na za kijamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie kwamba maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni kipaumbele namba moja. Tunafahamu Rais ameelekeza, na Serikali tupo kwenye taratibu za kuandaa fedha kwa awamu kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa maelekezo hayo. Kwa hiyo wananchi wa Jimbo la Same Mashariki na Mheshimiwa Mbunge wawe na uhakika kwamba Serikali itatekeleza ahadi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, kumwelekeza Meneja wa TARURA wa Wilaya ya Same, pamoja na Mkoa wa Kilimanjaro, wafike mara moja kwenye hilo eneo ambalo lina changamoto na halipitiki kwa sasa ili tuweze kuona namna ya kulitengeneza kwa dharura ili wananchi waweze kupitisha mizigo yao na kuendelea na shughuli zao za kiuchumi. (Makofi)

Name

Morris Joseph Makoi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Mjini

Primary Question

MHE. ANNE K. MALECELA aliuliza: - Je, lini barabara ya Hedaru - Mamba Vunta yenye Km 42.44 itaboreshwa ili kuokoa uchumi wa Wananchi wa Kata ya Mamba Vunta?

Supplementary Question 2

MHE. MORRIS J. MAKOI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Ninaomba niungane na Mheshimiwa Mbunge wa Same, Mheshimiwa Anne Kilango. Mheshimiwa Rais alipokuja Kilimanjaro alitoa ahadi ya kumalizia ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, barabara ya Rau Madukani - Materuni Shimbwe yenye kilometa 9.7. Ninaomba kauli ya Waziri ni lini Serikali itamalizia sehemu iliyobaki, kwa sababu sehemu hiyo inasaidia sana utalii? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunafahamu hiyo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema. Kama nilivyosema, ninarejea kwamba ahadi za Rais ni kipaumbele namba moja katika utekelezaji wa miradi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kwamba barabara hiyo ya kilometa tisa ipo kwenye mpango hivi sasa, na tutaendelea kuhakikisha tunatafuta fedha mapema iwezekanavyo kwa awamu kuendelea kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili iweze kutoa huduma ambayo inahitajika.

Name

Dr. Christina Christopher Mnzava

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ANNE K. MALECELA aliuliza: - Je, lini barabara ya Hedaru - Mamba Vunta yenye Km 42.44 itaboreshwa ili kuokoa uchumi wa Wananchi wa Kata ya Mamba Vunta?

Supplementary Question 3

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa, TARURA imekuwa ikijenga barabara kwa kiwango cha lami kwa baadhi ya centre, lakini katika Halmashauri ya Shinyanga, Jimbo la Solwa hakuna Kata ambayo ina barabara ya kiwango cha lami, ni lini Serikali itatujengea angalau kwenye Makao Makuu ya Halmashauri barabara kwa kiwango cha lami?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie nafasi hii kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mpango wetu wa barabara za vijijini na mijini tunazo barabara za udongo, barabara za changarawe na barabara za lami, na tumeweka kipaumbele kuendelea kuongeza barabara za lami, hususan maeneo ya miji ili kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie kwamba tunapoendelea na bajeti zetu, tutatoa kipaumbele kwenye eneo la Jimbo hilo la Solwa na hizo barabara za Kata zile ambazo zinawezekana kujengwa kwa awamu, tutaanza ujenzi kwa awamu.

Name

Moshi Selemani Kakoso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tanganyika

Primary Question

MHE. ANNE K. MALECELA aliuliza: - Je, lini barabara ya Hedaru - Mamba Vunta yenye Km 42.44 itaboreshwa ili kuokoa uchumi wa Wananchi wa Kata ya Mamba Vunta?

Supplementary Question 4

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Barabara ya Kapanga - Bujombe - Kalia inayounganisha na Wilaya ya Uvinza Mkoa Kigoma, ina hali mbaya baada ya mvua kunyesha na Serikali iliahidi kutoa fedha za kuiunganisha hiyo barabara kwa shilingi bilioni 1.5. Ni lini Serikali itatoa fedha hizo ili iweze kujenga hiyo barabara?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, zipo barabara ambazo zimeathiriwa sana na mvua ambazo zinaendelea kunyesha kote nchini, ikiwepo barabara ambayo Mheshimiwa Kakoso ameisema.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tumetoa taarifa kadhaa kwa Wabunge, tayari Serikali katika kipindi cha miezi hii miwili iliyopita imepeleka katika Majimbo yetu zaidi ya shilingi bilioni 21.4 kwa ajili ya kufanya shughuli za dharura za kutengeneza barabara ili ziweze kupitika.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa tunaendelea na tathmini za mwisho kwa sababu bado kuna maeneo mvua zinaendelea kunyesha. Kwa hiyo, tunafanya tathmini za mwisho za gharama za fedha zinazohitajika kwa ajili ya kwenda kufanya marekebisho na matengenezo ya barabara hizo, na mpaka wiki mbili zilizopita tulikuwa tuna takribani shilingi bilioni 98 zinahitajika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Kakoso, mara baada ya kukamilisha tathmini hiyo, tutaanza kupeleka fedha za dharura kwa ajili ya kurekebisha barabara hizo na tutahakikisha pia barabara hiyo inapelekewa hiyo shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya matengenezo.