Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
John Francisco Nzilanyingi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyamagana
Primary Question
MHE. JOHN F. NZILANYINGI aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara za pembezoni na mtaani maeneo ya Kushiri, Mahina, Luchelele na Lwanchima?
Supplementary Question 1
MHE. JOHN F. NZILANYINGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali miwili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa majibu ya Serikali swali langu la kwanza hali ya barabara kwenye Jimbo la Nyamagana kutokana na uharibifu ulioletwa na madhara ya mvua ni mkubwa sana, maeneo ya Mahina, maeneo ya Luchelele, maeneo ya Lwanchima maeneo ya Igogo, hali ni mbaya sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nini mpango wa Serikali wa kwenda kufanya kazi kwa haraka ili tuweze kuwanusuru wananchi kwenye maeneo yao ili barabara ziweze kupitika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, barabara ya Mkuyuni Mahina - Mandu kwenda mpaka Nailipichi yenye urefu wa kilometa 10.5, imeshafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Tarehe 19 Disemba ya mwaka 2024 Waziri wa TAMISEMI alikuja kuitembelea barabara ile na akaahidi kutoa fedha ili ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami uweze kuanza mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ...
MWENYEKITI: Uliza swali Mheshimiwa.
MHE. JOHN F. NZILANYINGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, toka Waziri wa TAMISEMI amekuja sasa yapata zaidi ya miaka mitatu. Ni nini kauli ya Serikali juu ya uanzaji wa ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 10.5 ili iweze kuwasaidia wananchi wa Jimbo la Nyamagana? Ahsante. (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza, nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge, nimhakikishie tu kwamba Serikali inatambua kwamba tuna changamoto ya uharibifu mkubwa wa baadhi ya barabara katika Jimbo la Nyamagana zikiwemo barabara za Mahina, Luchelele na nyingine ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie tu kwamba tayari tumeshapokea taarifa rasmi ya tathmini ya gharama zinazohitajika kwa ajili ya mategenezo ya barabara hizo na hivi sasa Serikali inaendelea na hatua za mwisho za kuandaa utaratibu wa fedha ili kupelekwa fedha katika maeneo yote yenye uharibifu wa barabara, zikiwemo barabara za Jimbo la Nyamagana kwa ajili ya matengenezo ya dharura na ya kawaida ili ziweze kupitika vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Nzilanyingi, kwamba tunafahamu na tuko katika hatua za kupeleka fedha ili barabara hizi ziweze kujengwa na kuweza kupitika vizuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la pili kuhusiana na barabara hiyo ya Mbuyuni yenye urefu wa kilometa 10.5 kufanyiwa usanifu, maana yake ni hatua ya mwanzo kuelekea kumpata mkandarasi na baadaye kuendelea na ujenzi wa barabara hiyo. Kwa hiyo, kauli ya Serikali ni kwamba kama ambavyo tumedhamiria na kufanya usanifu tutaendelea kujiandaa kwa maana ya kutafufa fedha na kuhakikisha kwamba barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha lami kama ambavyo ipo kwenye mpango. (Makofi)
Name
William Kafiti Kafiti
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Primary Question
MHE. JOHN F. NZILANYINGI aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara za pembezoni na mtaani maeneo ya Kushiri, Mahina, Luchelele na Lwanchima?
Supplementary Question 2
MHE. KAFITI W. KAFITI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Ilemela, ninaomba kujua, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara ya Pasiansi Lumala – Kiseke, kwa sababu barabara hii ni muhimu kwa wakazi wa Jimbo la Ilemela na imechukua zaidi ya Kata tatu? Ni nini kauli ya Serikali katika hilo? Ahsante. (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Pasiansi katika Jimbo la Ilemela ambayo Mheshimiwa Kafiti ameifuatilia mara kwa mara na tunafahamu kwamba Serikali imeendelea kuweka kipaumbele kuhakikisha kwamba barabara hiyo inajengwa, kwa sababu ni barabara muhimu sana kwa wananchi wa eneo la Ilemela.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ipo kwenye mpango wa Serikali na hatua za utekelezaji wa barabara hizo zitafanyika ili kuhakikisha kwamba inakamilika kwa wakati na inakuwa na ubora unaotakiwa kwa manufaa ya wananchi wa Ilemela. (Makofi)
Name
Ritta Enespher Kabati
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JOHN F. NZILANYINGI aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara za pembezoni na mtaani maeneo ya Kushiri, Mahina, Luchelele na Lwanchima?
Supplementary Question 3
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Boma ya Ng’ombe, Masisiwe ni barabara ya kiuchumi, toka mvua zimeanza kunyesha barabara hii haipitiki magari yamekwama.
Nini mpango wa Serikali tunusuru barabara zote za Kilolo ikiwepo hii barabara ya Masisiwe Boma La Ng’ombe? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Boma Ng’ombe - Masisiwe katika Jimbo la Kilolo ni barabara muhimu sana, na kwa hakika Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati amefuatilia mara kadhaa. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tayari iko kwenye orodha ya barabara zetu za kipaumbele, mara baada ya mvua kukatika na tutaenda na mpango ule wa dharura kwa ajili ya matengenezo kuhakikisha kwamba barabara ile inapitika vizuri na kusaidia shughuli za usafiri katika Jimbo la Kilolo. (Makofi)
Name
Mwita Mwikwabe Waitara
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Primary Question
MHE. JOHN F. NZILANYINGI aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara za pembezoni na mtaani maeneo ya Kushiri, Mahina, Luchelele na Lwanchima?
Supplementary Question 4
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru. Ninapozungumza sasa hivi hapa Kata ya Bumera, Susuni, Nyarero, Ganyange, Pemba, Mbugi hakuna mawasiliano, njia zimekatika. Nini kauli ya Serikali kwa watu wa Tarime Vijijini maeneo ambayo nimeyataja? Ahsante. (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na changamoto ya barabara kote nchini ikiwemo katika Jimbo la Tarime Vijijini kwa Mheshimiwa Waitara, na changamoto hii imetokana na mvua nyingi ambazo zimenyesha na kupelekea uharibifu wa barabara nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba yapo baadhi ya maeneo ambayo mvua bado zinaendelea kunyesha, kinachofanyika sasa ni tathmini ya gharama zinazohitajika kwa ajili ya marekebisho ya barabara hizo, lakini tunasubiri angalau hali ya mvua ipungue kwa sababu kwenda kufanya matengenezo katika kipindi hiki cha mvua nyingi hakutakuwa na faida kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, Serikali inafahamu inawapa pole wananchi wa Jimbo la Tarime lakini imeshaandaa utaratibu wa fedha za dharura kwa ajili ya kwenda kutengeneza mara mvua zikipungua ili barabara hizo zipitike vizuri. (Makofi)
Name
Eng. Ezra John Chiwelesa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Biharamulo Magharibi
Primary Question
MHE. JOHN F. NZILANYINGI aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara za pembezoni na mtaani maeneo ya Kushiri, Mahina, Luchelele na Lwanchima?
Supplementary Question 5
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Barabara za Mtaa wa Ng’ambo Wilaya ya Biharamulo Mjini pale zimeharibika vibaya sana. Tunajua ni msimu wa mvua, lakini technically ziko means za ku-repair barabara ili ziendelee kupitika hata wakati wa mvua. Ni nini kauli ya Serikali kuwasaidia wananchi wa Ng’ambo ili sasa waweze kutoka majumbani na kurejea huku wakilitumikia Taifa lao?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko barabara ambazo zimeharibiwa, lakini zinaweza zikafanyiwa matengenezo ya muda ili kuwezesha shughuli za usafirishaji kuendelea wakati tunajiandaa na matengenezo ya kudumu zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, nimwelekeze Meneja wa TARURA Mkoa wa Kagera na Wilaya ya Biharamulo kwenda kufanya tathmini ya haraka kwenye barabara hiyo na kufanya matengenezo ili barabara angalau iendelee kupitika wakati tunasubiri muda wa kufanya matengenezo ya kudumu. (Makofi)
Name
Edwin Enosy Swalle
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupembe
Primary Question
MHE. JOHN F. NZILANYINGI aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara za pembezoni na mtaani maeneo ya Kushiri, Mahina, Luchelele na Lwanchima?
Supplementary Question 6
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, iko barabara ya Lupembe kwenda Ikondo, na hii barabara inapita nyumbani kwangu pale Kanikelele, yako maeneo matatu yameharibika vibaya sana hata mimi leo siwezi kufika pale kwangu nyumbani Kanikelele. Ni nini maagizo ya Meneja wa Njombe kufanya marekebisho sehemu hizo tatu watu waweze kusafiri kwenye hii barabara?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuwakumbusha Mameneja wa TARURA katika Wilaya zetu zote na katika Mikoa yetu yote kwamba tunafahamu kuna hali ya mvua inaendelea, lakini tuna barabara muhimu sana katika maeneo yetu ambazo ni lazima ziendelee angalau kupitika wakati tunasubiri matengenezo ya kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika Jimbo la Lupembe ninamwelekeza Meneja wa TARURA, Mkoa wa Njombe na Wilaya ya Njombe kwenda kufanya tathmini kwenye barabara hiyo na kuona linaloweza kufanyika angalau matengenezo ya muda yafanyike, barabara iendelee kupitika, wakati tunasubiri hali ya hewa kukaa vizuri kwa ajili ya matengenezo ya kudumu. (Makofi)