Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Primary Question

MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:- Je, lini Serikali itakarabati Shule ya Msingi Mtapenda Kata ya Mtapenda – Nsimbo?

Supplementary Question 1

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na pole kwa usumbufu. Kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri, hii shule imejengwa toka mwaka 1970 mpaka leo haijafanyiwa marekebisho ya aina yoyote. Katika kipindi cha mvua, hasa hii ya mwaka huu, kwa kuwa mabati yote yameoza, watoto wananyeshewa, hawawezi kupata usikivu katika masomo yao. Lini Serikali itachukua dharura ya kurekebisha Shule hii ya Msingi ya Mtapenda ili watoto waweze kukaa kwa amani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kwa kuwa katika Shule ya Msingi ya Mtapenda, hakuna nyumba za Walimu, wananchi wa Kata ya Mtapenda, Kijiji cha Mtapenda, wakaamua kujichangisha ili waweze kujenga hata nyumba mbili za walimu na mimi Mbunge wao nikawachangia kutoka Mfuko wa Jimbo, lakini Serikali mpaka leo haijafanya kitu chochote. Ni lini Serikali itajenga nyumba za walimu katika Kata ya Mtapenda? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba ziko shule kongwe na chakavu kama Shule ya Msingi Mtapenda na Serikali inaandaa mpango mahususi kwa ajili ya ukarabati wa shule zote kongwe kama ambavyo nimejibu kwenye jibu langu la msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa shule hii ni chakavu sana na kwa mujibu wa Mheshimiwa Mbunge kwamba inavuja na wanafunzi hawawezi kusoma vizuri, ni wajibu wa Halmashauri ya Nsimbo na Mkurugenzi kupitia mapato ya ndani angalau kufanya marekebisho ya haraka kwenye shule hii ili wanafunzi waendelee kusoma wakati Serikali Kuu ikiendelea na utaratibu wa kutafuta fedha kwa ajili ya kufanya ukarabati mkubwa wa shule hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI nimwelekeze Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nsimbo, kufanya tathmini ya haraka na kufanya matengenezo ya madarasa yanayovuja ili wanafunzi waendelee kusoma wakati Serikali inaandaa bajeti kubwa kwa ajili ya kwenda kufanya ukarabati mkubwa wa shule hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali lake la pili, tunafahamu kwamba yapo maeneo mbalimbali ya shule zetu ambako kuna upungufu wa nyumba za walimu na Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu katika shule zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa kuna zaidi ya nyumba 650 zinaendelea kujengwa kote nchini. Niwapongeze wananchi wa Nsimbo kwa kuanza ujenzi wa nyumba, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kuchangia nguvu za wananchi. Nimhakikishie kwamba na sisi Serikali Kuu tutafanya utaratibu wa kupata fedha kwenda kuhakikisha nyumba hiyo ya walimu inakamilishwa.