Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Saashisha Elinikyo Mafuwe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Primary Question
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza kada ambazo hazipo kwenye orodha ya kada za Sekretarieti ya Ajira kwa kuwa zinafundishwa vyuoni?
Supplementary Question 1
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, niwashukuru sana wananchi wa Hai, ndugu, rafiki na jamaa na ninyi Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa namna ambavyo mlinisindikiza wakati wa msiba wa mama yetu mpendwa. Sifa na utukufu tunamrudishia Mungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali imekubali kwamba wanachelewesha kuweka kozi hizi kwenye Sekretarieti ya Ajira, je, Serikali iko tayari sasa kuunda chombo maalum kitakachohusisha vyuo vikuu ambavyo vinatengeneza hii mitaala na hizi kozi pamoja na Sekretarieti ya Ajira ili waweze kuthamini mahitaji ya hizi kozi na zile ambazo zinahitajika mtaani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali iko tayari sasa kurekebisha sifa za wahadhiri wa vyuo vikuu ambazo zinawataka ili mhadhiri kufundisha kozi fulani lazima awe amebobea kwa umaalum kwenye kozi hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mhadhiri anayefundisha International Relation, anatakiwa awe amesoma degree ya kwanza International Relation, degree ya pili na ya tatu, ilhali aliyesoma Political Science anaweza kufundisha International Relation, jambo linalopelekea vyuo sasa kuanza kufuta kozi. Kwa mfano Chuo cha UDOM kimefuta kozi ya International Relation kwa sababu wahadhiri wenye sifa hiyo Tanzania hawapatikani. Je, Serikali iko tayari kufanya marejeo ili kozi hizi ziendane na sifa halisi zilizopo kwenye vyuo vyetu?
Name
Regina Ndege Qwaray
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza mitaala inayoandaliwa na vyuo vikuu siyo kwa ajili ya ajira za Serikali pekee yake. Mitaala hii inaandaliwa kwa ajili ya ajira za Serikali pamoja na private sector, pamoja na international organizations. Ndiyo maana inaundwa mitaala ambayo inaweza ikakidhi mahitaji ya soko la ajira kwenye Serikali, pia na hizo private sectors.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ombi la Mheshimiwa Mbunge, kwamba kuwe na chombo maalum kwa ajili ya kushiriki katika kuandaa mitaala; ombi lake tunalichukua. Hata hivyo, kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia pamoja na mahitaji ya kisera, Serikali imeendelea kupitia sifa na miongozo ya miundo ya maendeleo ya utumishi katika kada mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuangalia, kwamba kada zile ambazo zinaandaliwa au zinatolewa katika vyuo vikuu zinaendana na soko la ajira. Sekretarieti ya Ajira inatangaza ajira kulingana na uhitaji wenyewe wa soko, kwamba soko la ajira linahitaji nini? Ndiyo maana Sekretarieti inapotangaza ajira inaangalia miundo ya maendeleo ya kiutumishi katika kada mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye kipengele au swali lake la pili kuhusu kurekebisha sifa za lazima kwa wahadhiri wa vyuo vikuu, vyuo vikuu vimekuwa na miongozo na mifumo inayojitegemea ambayo inawalazimu kuandaa sifa ambazo zinatakiwa ili kupata mhadhiri, kwamba lazima awe na sifa hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, swali alilouliza Mheshimiwa Mbunge kuhusu International Relation, kwamba mhadhiri ili aweze kufundisha International Relation awe amesoma undergraduate, amesoma masters na pia amesoma mpaka Ph.D; vyuo vikuu vinafanya hivyo kwa sababu ya kupata wabobezi wanaoweza kufundisha fani hizo katika vyuo vikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba suala lake tutalichukua kama Serikali kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu ili tuweze kuliangalia kwa upana wake na kuona umuhimu wake.
Name
Asha Juma Feruz
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza kada ambazo hazipo kwenye orodha ya kada za Sekretarieti ya Ajira kwa kuwa zinafundishwa vyuoni?
Supplementary Question 2
MHE. ASHA J. FERUZ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kwanza ninampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya. Kutokana na majibu ya swali la msingi, kwamba ni kweli vipo vyuo ambavyo vinatoa kozi ambazo hazipo kwenye kada za Sekretarieti, je, ni upi mkakati wa Serikali sasa kuweza kuwa-accommodate kwa haraka wale wanafunzi ambao tayari wameshamaliza masomo kwenye hizo kozi ambazo hazipo kwenye kada za Sekretarieti, kwa sababu tayari zilisharuhusiwa kufundishwa kutokea Serikalini, zilipewa kibali?
Name
Regina Ndege Qwaray
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza na mimi nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Pia, niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kutoa pole kwa familia ya Mheshimiwa Saashisha Mafuwe kwa msiba mkubwa wa mama yake, Mwenyezi Mungu amhifadhi na aendelee kuwapa faraja familia nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la nyongeza lililoulizwa na Mheshimiwa Mbunge, ukweli ni kwamba Serikali imekuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na vyuo vikuu pale wanapounda kozi au eneo lolote la masomo. Ninataka nitoe mfano ili jibu liwe jepesi. Chuo Kikuu Mzumbe wana kozi inaitwa Maendeleo ya Vijana. Kozi ile inatengeneza maafisa vijana. Kama unavyojua, kwenye Serikali mfumo wetu sisi unazo nafasi kwenye TAMISEMI za maafisa wa vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ile kozi walikuwa hawajaingizwa katika muundo. Tunapozungumza sasa hivi, Serikali imeshakamilisha mawasiliano kwanza ndani ya Serikali, na pia kutengeneza muundo ambao vijana wale ambao wamemaliza kozi ile wote wanakwenda kuwa adopted katika mfumo wa ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunachokifanya ambacho ameeleza Mheshimiwa Naibu Waziri, ninataka nieleze, ni yaleyale, kwamba msingi mkubwa, vyuo vikuu viwasiliane na Wizara husika kwa maana ya Wizara mama kama Wizara ya Elimu ili sisi ambao tunahusika na kutengeneza miundo ya kazi, tuweze kufanya kazi nzuri ya kuhakikisha kwamba watu wote wanaomaliza vyuo vikuu tunawa-adopt katika mfumo wa kazi, waingie katika mfumo wa ajira ili waweze kupata kazi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ninashukuru.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved