Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Kassimu Amari Mbaraka
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tanga Mjini
Primary Question
MHE. KASSIMU A. MBARAKA aliuliza: - Je, lini ujenzi wa Barabara ya Kiomoni, Pande, Mjesani hadi Muheza inayounganisha Wilaya ya Tanga na Muheza utaanza?
Supplementary Question 1
MHE. KASSIMU A. MBARAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa kuna miradi mikubwa miwili ya shughuli za kiuchumi eneo la Chongoleani pamoja na eneo la Gombero pale ule mradi wa Chuo Kikuu Campus ya Mzumbe, je, ni lini sasa nayo Barabara ya Mabokweni kuelekea mpaka Old Korogwe Kwamndolwa nayo itakamilika kwa kiwango cha lami?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Je, Serikali ina mpango gani wa kibajeti wa kuhakikisha kwamba kilometa 15 za kutoka Tanga mpaka Kirare kwenye Barabara ya Pangani zinaenda kukamilika ndani ya mwaka huu wa 2026?
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Mabokweni kwenda Kwamndolwa inajengwa kwa vipande viwili kuanzia Mabokweni kwenda Bombo Mtoni; tuna kilometa 10 ambayo tutaishia pale Maramba, na pia huku Kwamndolwa tutaanza kilometa 10 na tuko kwenye hatua za mwisho za manunuzi ili wakandarasi waweze kuanza pande zote mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo ni kuijenga barabara yote kwa kiwango cha lami kadiri fedha inavyoendelea, na hata katika bajeti inayokuja tutaendelea kutengea fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya pili kama nimemsikia vizuri, nadhani ni ya Tanga - Pangani sijui kama nimemsikia vizuri ili niweze kumjibu vizuri.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbaraka.
MHE. KASSIMU A. MBARAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani. Ninauliza kuhusiana na barabara ya Tanga - Pangani kuna kilometa 15 za kutoka Tanga Mjini mpaka Kirare pale ambayo inaungana na eneo la Tundaua ambayo tayari kuna lami...
MWENYEKITI: Sasa Mheshimiwa hayo ni maswali karibia matatu.
MHE. KASSIMU A. MBARAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali ni moja tu!
MWENYEKITI: Hebu uliza swali moja Mheshimiwa Naibu Waziri akusikie vizuri.
MHE. KASSIMU A. MBARAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango gani wa kibajeti wa kukamilisha kipande cha barabara kilometa 15 kutoka Tanga mpaka Kirare? (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Barabara ya Tanga - Pangani yenye urefu wa kilometa 50 ipo kwenye utekelezaji na tuko takribani 50%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipande hiki cha Tanga hadi Kirare kwanza kilichelewa kwa sababu hilo eneo lilikuwa lina miundombinu ambayo ilikuwa hatuwezi kuanza, kwa hiyo, tulilazimika kwenda kuanzia Kirare kwenda Pangani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa karibu miundombinu yote imeondolewa, na sasa mkandarasi yupo, tunategemea tutakapokuwa tumemlipa fedha, ataendelea na hiyo kazi ili aweze kuikamilisha ambayo pia Meneja wa Mkoa tumeshamwelekeza, kwa sababu pia barabara hiyo tulipata taarifa kwamba kutokana na hali ya mvua imeharibika sana, kwanza aweze kuhakikisha mkandarasi anaitengeneza, na baada ya hapo, basi aweze kurudi ili kuijenga hiyo barabara yote kwa kiwango cha lami, ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved