Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Yagi Maulid Kiaratu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Singida Mjini
Primary Question
MHE. YAGI M. KIARATU aliuliza: - Je, lini mradi wa maji unaotekelezwa katika mitaa 38 ya Manispaa ya Singida utakamilika ili wananchi wapate huduma ya majisafi na salama?
Supplementary Question 1
MHE. YAGI M. KIARATU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri. Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitaishukuru Serikali kutokana na historia ya upatikanaji wa majisafi na salama kwa Mji wa Singida. Hata hivyo, bado lipo tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mji wa Singida wananchi wanahitaji lita milioni 24 kwa siku ilhali upatikanaji ni lita milioni 11 kwa siku; utaona ni chini ya 50% ya mahitaji ya wananchi. Mradi huu wa miji 28 anaousemea Mheshimiwa Naibu Waziri ni mradi ambao umechelewa sana. Mkataba ulisainiwa Juni, 2022 lakini mradi ukaanza Aprili, 2023.
Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi kuamini mpaka leo bado wanachimba visima, hakuna matanki yaliyojengwa wala mitandao haijatandazwa. Hii inawasababishia wananchi adha ya maji, na hivi ninavyoongea, kuna mgawo mkali wa maji katika mji wa Singida.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili. Viko vijiji 12 na mitaa kumi ambayo haijawahi kupata maji ya bomba tangu vijiji hivyo vimeanzishwa. Vijiji hivyo ni Uhamaka, Mwampafa, Isomia, Mwachichi, Unyamikumbi A, Unyamikumbi B, Ikhade, Ugauga A, Ugauga B, Ikenga, Isasida A, Isasida B, Unyambwa A, Unyambwa B, Mtamaa A, Mtamaa B, Kimai, Mtaa wa Mtisi, Mwinyutuka na vijiji vingine. Wananchi hawa hawajawahi kufungua bomba.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba commitment ya Waziri, na ikibidi, akikubali, basi tutafute muda tuongozane mimi na yeye akaone hali halisi huko ndani. Wananchi wanachangia maji na wanyama katika enzi hizi ambazo Rais ana nia nzuri ya kuwatua wanawake ndoo kichwani…
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa, umeeleweka.
MHE. YAGI M. KIARATU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba majibu ya Serikali.
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Yagi Maulid Kiaratu, Mbunge mahiri kabisa kutoka Jimbo la Singida Mjini na kwa namna ambavyo anafuatilia kwa ukaribu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri kwamba ni kweli tunayo mitaa ambayo bado haina maji, lakini pia tunavyo vijiji kwa sababu jimbo lake lina vijiji na mitaa, katika mitaa 53, mitaa 40 ina maji, mitaa mitatu ina maji ambayo kidogo hayatoshelezi, lakini mitaa 10 ndiyo mitaa ambayo haina maji kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika vijiji 19, tunavyo vijiji saba ambavyo vina maji ya kutosha, pia tuna vijiji takribani vitatu ambavyo maji yake hayatoshi. Vijiji vingine vilivyobaki tunakiri kama Serikali, kwamba bado maji hayajafika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa takwimu hizi, Serikali mpaka sasa imeshafanya kazi kubwa sana kwa sababu hadi sasa Jimbo la Singida Mjini upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama umefikia zaidi ya 76%. Tunatambua kuwa bado kuna kazi kubwa ambayo tunaendelea kuifanya, lakini kwenye suala la mradi huu wa miji 28, dhamira ya Serikali siyo kuchelewesha miradi, bali kukamilisha miradi ili itoe matokeo, na wananchi wapate huduma ya majisafi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la mradi huu wa Singida ni kwamba visima ambavyo vilikuwa vinachimbwa, scenario hii ni sawa na kule Chunya, kwamba wanachimba, lakini visima vinamomonyokea ndani kiasi kwamba wanachimba, lakini bado kunakuwa na changamoto ya kukiendeleza kwa sababu udongo unarudi ndani. Mkandarasi alipata shida sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tumeamua kumtumia mkandarasi aliyechimba Nzunguni, Zuzu, na Nala, sasa tunamhamishia ili aende na vifaa vyake akachimbe katika Mradi wa Miji 28 Singida Mjini ambapo mpaka sasa tumeshachimba visima vitatu. Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali imejidhatiti na iko makini.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kutengeneza mradi ambao hautakuwa na matokeo, na hatuwezi kutengeneza mradi ambao baada ya muda mfupi unakuwa umebaki kama white elephant. Kwa hiyo, tuko makini kufuatilia ili utakapokamilika, utoe matokeo yaliyokusudiwa kwa Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho, niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge katika Jimbo lake la Singida Mjini ili kujionea hali halisi ya maendeleo ya miradi mbalimbali ndani ya jimbo lake.
Name
Nancy Hassan Nyalusi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. YAGI M. KIARATU aliuliza: - Je, lini mradi wa maji unaotekelezwa katika mitaa 38 ya Manispaa ya Singida utakamilika ili wananchi wapate huduma ya majisafi na salama?
Supplementary Question 2
MHE. NANCY H. NYALUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, je, lini Serikali itamalizia mradi wa maji katika Kata ya Wambingetu?
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kujua kata hiyo iko katika jimbo lipi?
MHE. NANCY H. NYALUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Kilolo, Wilaya ya Kilolo.
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana dada yangu Mheshimiwa Nancy, kwa kuendelea kuwasemea akina mama, hasa katika kumtua mama ndoo kichwani; na hiyo ni dhamira ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Tunaendelea kuhakikisha kwamba sera yetu ya maji inahakikisha kwamba watu wapate huduma ya majisafi na salama. Vijiji vyake hasa katika kata ambayo ameitaja katika Jimbo la Kilolo tumeiweka kwenye mpango wa bajeti wa mwaka 2026/2027 ili iende ikatekelezwe.
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Primary Question
MHE. YAGI M. KIARATU aliuliza: - Je, lini mradi wa maji unaotekelezwa katika mitaa 38 ya Manispaa ya Singida utakamilika ili wananchi wapate huduma ya majisafi na salama?
Supplementary Question 3
MHE. DKT. SELEMANI S. JAFO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujua, nini mpango wa Serikali kupeleka fedha za mradi wa maji wa Mafizi ambao sasa hivi umefikia 98%, lakini mkandarasi hajalipwa hata senti tano? Halikadhalika Mradi wa Maji wa Nyani ambao umefikia 75%, lakini miradi hiyo yote wakandarasi hawajalipwa, kwa mfano Nyani wamefanya hadi mobilization ya vifaa; je, Serikali ina mpango gani wa kulipa fedha ili kazi hiyo ikamalike na wananchi wapate maji?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba miradi yote ambayo imefikia katika hatua nzuri za utekelezaji, tunasukuma kwa nguvu kubwa sana upelekaji wa fedha ili miradi hiyo ianze kutoa matokeo. Ni dhamira ya Serikali pia kwamba pale ambapo tutakamaliza miradi ambayo imefikia katika hatua nzuri, tunakuja katika miradi ambayo iko katika hatua za katikati.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba tunayo commitment ya Serikali katika miradi mingi nchini ambapo tutakuwa tunapeleka fedha kwa awamu kwa vipaumbele vya kimkakati. Lengo ni kwamba Watanzania waendelee kupata huduma ya majisafi na salama. Tunatambua kwamba Serikali ina dhamira ya kuikamilisha miradi hii yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimtoe hofu kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Selemani Jafo kwa kuendelea kuwasemea wananchi wake na sisi Wizara ya Maji tutaendelea kushirikiana naye ili kuhakikisha kwamba miradi hiyo inakamilika.
Name
Dr. Wilson Charles Mahera
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Butiama
Primary Question
MHE. YAGI M. KIARATU aliuliza: - Je, lini mradi wa maji unaotekelezwa katika mitaa 38 ya Manispaa ya Singida utakamilika ili wananchi wapate huduma ya majisafi na salama?
Supplementary Question 4
MHE. DKT. WILSON C. MAHERA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ningependa kujua ni lini mradi wa Mugango – Kiabakari – Butiama kwa vijiji kumi ambavyo vinne ni vya Kata ya Biregi, viwili ni vya Kata ya Mtuguri, kimoja Kata ya Isaba, na kimoja Kata ya Busengwe vitaanza kupata maji?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imewekeza fedha zaidi ya shilingi bilioni 70 ndani ya Mugango – Kiabakari – Butiama ambapo tayari mradi huo ulishaanza kutoa huduma ya majisafi na salama. Mimi pia nilifanya ziara na Mheshimiwa Mbunge, tukashirikiana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tukabaini kwamba ni kweli kuna maeneo bado ambayo bado yana changamoto. Sasa, tunachokifanya kupitia mradi huo, tunafanya upanuzi ili uende kwenye kata ambazo Mheshimiwa Mbunge amezisema. Sasa mpango wa Serikali, tumeweka kwenye bajeti ili kuhakikisha sasa tunaenda kufanya extension ya mradi huu ili uweze kufika katika maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyahitaji.