Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Enock Zadock Koola
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vunjo
Primary Question
MHE. ENOCK Z. KOOLA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanzisha Kituo cha kukodi vifaa vya kilimo katika Wilaya ya Moshi Vijijini?
Supplementary Question 1
MHE. ENOCK Z. KOOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali na kwa kuwa Halmashauri ya Moshi imeshawekwa kwenye awamu ya kwanza, ningependa kujua kauli ya Serikali kuhusu hivi vituo viko wapi na vitajengwa lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa maeneo ya Jimbo la Vunjo, kuna sehemu kubwa ya tambarare yenye mashamba makubwa ya kilimo cha mpunga; je, Serikali ipo tayari kupeleka matrekta makubwa yanayokidhi mahitaji na kuongeza tija? (Makofi)
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nimthibitishie tu Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Mheshimiwa Enock Koola kwamba moja, ametaka kujua kauli ya Serikali, kuhusu hayo matrekta yako wapi? Wizara ya Kilimo tunapeleka matrekta katika Halmashauri ya Wilaya na wao wanatuainishia maeneo ambayo sisi tunapeleka kile kituo na hususan yale maeneo ambayo vituo hivi vinapaswa kwenda ni yale maeneo ambayo kuna uzalishaji mkubwa, ndiyo maeneo hayo ambapo tumekuwa tukiweka kama ambavyo iko katika eneo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika kipindi hiki cha mwanzo, unakuta mengi yamewekwa katika halmashauri za wilaya katika hatua za mwanzo, wakati huo wakitafuta maeneo ambapo yatakwenda kupelekwa kwa ajili ya kutoa hiyo huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Serikali iko tayari kupeleka matrekta makubwa katika maeneo hayo kwa ajili ya kuwasaidia wananchi. Ahsante sana. (Makofi)
Name
Neema Gerald Mwandabila
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ENOCK Z. KOOLA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanzisha Kituo cha kukodi vifaa vya kilimo katika Wilaya ya Moshi Vijijini?
Supplementary Question 2
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali iliweza kutoa matrekta na hata Halmashauri yangu ya Mji wa Tunduma niliyaona, je, ni upi utaratibu uliowekwa kwa ajili ya matumizi ya matrekta haya kwa watu wetu huko wilayani?
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimemsikia Mheshimiwa Neema, dada yangu. Utaratibu ni kwamba, lengo la Serikali kwanza ni kuanzisha vituo 1,000 nchi nzima ambavyo vitafika katika halmashauri zote nchini. Moja ya lengo letu ni kupeleka karibu takribani trekta 10,000 kusambaza katika hivyo vituo. Lengo kubwa la Serikali ni kumpunguzia mkulima gharama ya uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, matrekta yale yakishakwenda katika yale maeneo, wananchi watakuwa wanakodi kwa bei nafuu, kwa sababu tunaamini kwamba wananchi wengi wanalima chini ya ekari tano. Mtu mwenye ekari tano, ekari moja hahitaji kununua trekta, isipokuwa anahitaji huduma ya trekta, ambayo sasa anaweza kuipata kwa bei nafuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, gharama hii, yaani tunasema mfumo huu ni uendelevu wa mfumo wa ruzuku wa kumsaidia mwananchi kupunguza gharama. Kwa hiyo, hilo ndilo lengo la Serikali na tunaendelea kulifanya hivyo.
Name
Abubakar Damian Asenga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilombero
Primary Question
MHE. ENOCK Z. KOOLA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanzisha Kituo cha kukodi vifaa vya kilimo katika Wilaya ya Moshi Vijijini?
Supplementary Question 3
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika Bunge lililopita Serikali ilikubali ombi letu la kuboresha kituo cha Kilimo cha KATRIN pale Ifakara kwa kuleta pia zana za kilimo ikiwemo matrekta ili wananchi waweze kuyakodi kwa bei nafuu. Je, mpango huu na mkakati huu umefikia wapi?
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Vilevile, ninampongeza kaka yangu Mheshimiwa Asenga kwa kufuatilia jambo hili kwa ajili ya jimbo lake na hususan katika eneo la Ifakara na anajua tumeshalizungumza hili kabla na nimeshampa mpango wa Serikali. Hata hivyo, kwa sababu wananchi wake wanahitaji kusikia hili, ni kwamba hili lipo katika mwaka wa fedha unaokuja kutekelezeka. Tutaongeza hivyo vifaa na wananchi watapata hivyo vifaa na vitawasaidia.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved