Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Abdallah Dadi Chikota
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyamba
Primary Question
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:- Je, lini Mradi wa Umwagiliaji wa Arusha Chini utaanza kujengwa?
Supplementary Question 1
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina swali moja la nyongeza na ushauri.
Kwa kuwa mkandarasi ameshapatikana na kwa kuwa mkandarasi ameshakabidhiwa eneo la mradi; je, ni lini mkandarasi huyo sasa ataanza kazi ya ujenzi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ushauri, kwa kuwa mradi huu unajengwa pembezoni kabisa mwa Mto Ruvuma na kutokana na mabadiliko ya tabianchi, mkondo wa mto huu sasa unaanza kuhama na kuathiri vijiji vya jirani kama Maembe Chini. Ni ushauri wangu sasa wakati wa utekelezaji wa mradi huu, wataalam wa kilimo washirikiane na wataalam wa mazingira ili kuhakikisha yale maji ambayo yanaathiri wanakijiji yanatumika kwenye mradi na badala yake kwenda kuathiri makazi ya wanavijiji, ninakushukuru.
Name
David Mwakiposa Kihenzile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kusini
Answer
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chikota, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Chikota kwa jinsi ambavyo anafuatilia kwa karibu masuala ya kilimo, sio kwenye jimbo lake tu, na nchi nzima. Kwa sababu tangu uhuru sote tunakubali kwamba kilimo ndiyo uti wa mgongo wa nchi yetu. Kilimo ndiyo kinatoa takribani 100% ya uhakika wa chakula kwenye nchi yetu, kinatuhakikishia usalama, malighafi kwenye viwanda, kinatoa ajira kwa vijana wa nchi yetu na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia ilani CCM maelekezo yake yeye mwenyewe sambamba na Dira yetu ya 2050 amethibitisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye hali ya kilimo nchini ilivyokuwa mwaka 2020 na sasa ameamua kuongeza bajeti ya kilimo kutoka shilingi bilioni 294 mpaka shilingi trilioni 1.1 ili kumnufaisha mkulima wa nchi hii, lakini pia Dkt. Samia kama haitoshi, kwa kutambua umuhimu wa eneo la umwagiliaji, miradi takribani 886 inatekelezwa nchi nzima, ikiwemo na miradi 146 ambayo mmojawapo ni wa kwake Mheshimiwa Chikota huu umeingizwa katika kundi hilo. Ipo miradi 28 ambayo inakaribia kukamilishwa, ipo miradi 71 ambayo ipo kwenye hatua mbalimbali, na ipo miradi 48 ambayo wakandarasi wamekwishapatikana kinachosubiriwa sasa ni kupewa fedha waanze kujenga miradi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Chikota na wananchi wote wananyamba kwa ujumla wawe na Subira, maadam walimchagua Dkt. Samia Suluhu Hassan na maadam Mbunge wao ameshiriki kupitisha bajeti ya kilimo ya mwaka huu, tunawapa uhakika fedha zinatafutwa wanakwenda kulipwa, mjenzi anaanza kujenga mradi huo ili kuweza kuwafaidisha wananchi wa Arusha Chini na maeneo yote ambayo yametajwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ushauri, Serikali imepokea ushauri huo, tutaielekeza kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Tume yetu ya Umwagiliaji wakae na Mheshimiwa Mbunge wapokee ushauri wake, wauingize katika utekelezaji bila kuathiri sheria na kanuni za nchi yetu.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved