Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Amosy William Maganga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Primary Question

MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA aliuliza: - Je, lini maji ya Ziwa Victoria yataanza kusambazwa katika Kata za Pangale, Mpombwe, Igigwa, Kisanga, Tutuo, Mkolye, Chabutwa na Ipoje?

Supplementary Question 1

MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa hii nafasi na vilevile nimshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini pamoja na majibu hayo ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, kwa vile tanki la maji katika Kijiji cha Tumbili, Kata ya Igigwa tayari limeshajengwa na kwa vile tanki hili tayari limeshajazwa maji takribani miezi miwili iliyopita kwa ajili ya kusambaza maji kwenye kata hizo za Igigwa, Pangale, Ipole, Tutuo pamoja na Mole.

Je, Mheshimiwa Waziri sasa haoni kwamba wakati umefika kwamba hayo maji ambayo tayari yameshajazwa yaanze kusambazwa kwa wananchi hawa ili kuwaondolea adha kubwa ya ukosefu wa maji waliyonayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Kata ya Kilumbi pamoja na Kata ya Kipili wana adha kubwa, wana changamoto kubwa sana ya maji, na suluhu ya kata hizo ni ujenzi wa Bwawa la Kilumbi.

Je, ni lini sasa Serikali itapeleka wataalamu wake ili waweze kufanya tathmini na hatimaye kuanza ujenzi wa bwawa hilo?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Amosy William Maganga, Mbunge wa Sikonge kwa namna ambavyo ameingia na kuhakikisha kwamba anasukuma sana huduma ya maji katika Mji wa Sikonge na kwa namna ambavyo anaendelea kutushirikisha Wizara ya Maji na katika package hii ya Urambo, Kaliua pamoja na Sikonge ni Sikonge pekee ndiyo imekuwa ya kwanza kuhakikisha kwamba maji yanaanza kutoa huduma kwa wananchi kama ambavyo nimesema katika jibu langu la msingi. Hii ni kwa sababu ya msukumo wake ambao anaendelea kutupa ushirikiano sisi Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tanki la Tumbili ni kweli kabisa kwamba tulilijaza maji na Mheshimiwa Waziri alifika Sikonge kwa ajili ya kufanya testing ya yale maji katika lile tanki. Kwa hiyo, ninaamini kabisa kwamba baada ya kufanya test na kukamilika tutaanza sasa kusambaza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa zaidi ni kwamba tuhakikishe ile miundobinu hakuna maji yatakuwa yanavuja ambayo yatasababisha kupoteza maji. Kwa hiyo, ndiyo maana bado tuko katika hatua za mwisho na baada ya hapo tutaanza mara moja kuhakikisha kwamba watu wako wa Sikonge wanasambaziwa maji ikiwemo kilometa 12 katika maeneo ya pembezoni ambayo Mheshimiwa Rais ameelekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la pili Kata ya Kilumbi; hii ni kata ambayo iko kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2025/2030 na hivyo bwawa ndiyo suluhisho. Nimtoe hofu, Serikali hii ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni sikivu sana na kwa sababu amesema na sisi tutatuma timu yetu kwenda kufanya need assessment. Baada ya hapo tufanye feasibility study na baada ya hapo tufanye usanifu wa kina. Baada ya hapo tupate fedha kwa ajili ya kujenga bwawa kwa ajili ya wananchi wake wa Kata ya Kilumbi pamoja na Kata ya Kipili. Ninakushukuru sana.

Name

Agnesta Lambert Kaiza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA aliuliza: - Je, lini maji ya Ziwa Victoria yataanza kusambazwa katika Kata za Pangale, Mpombwe, Igigwa, Kisanga, Tutuo, Mkolye, Chabutwa na Ipoje?

Supplementary Question 2

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Waziri ndani ya Jimbo la Segerea kwa mujibu wa ratiba ya DAWASA tunapata maji kwa mgao na huo mgao kwa sasa ndani ya Jimbo la Segerea umebaki katika makaratasi ya ratiba. Wananchi wa Jimbo la Segerea hawapati maji hata kwa huo mgao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo wananchi ambao mpaka sasa ni miezi 10, ni mwaka mmoja, ni miezi sita, ni mitatu hawapati maji safi na salama ya mgao na Mheshimiwa Waziri alitoa maelekezo kwamba wananchi wa Segerea wapate maji kulingana na ratiba ilivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kufahamu, nini kauli ya Serikali leo kwa jambo hili ambalo wananchi wanaambiwa mnapata maji, lakini maji hawapati. Ninapenda nisikie kauli ya Serikali kwa wananchi wangu wa Jimbo la Segerea. Ahsante sana kwa kunipa nafasi.

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Segerea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu kwamba swali hili aliliuliza wiki iliyopita, lakini ameliuliza kwa namna tofauti kwa leo, lakini mantiki yake iko pale pale kwamba anahitaji wananchi wake wa Segerea wapate maji ya uhakika ambayo pia ratiba ya mgao iweze kutabirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muktadha huo ni katika suala lile lile la kuhakikisha kwamba pampu zetu zinapopata hitilafu ni lazima tufanye replacement ili kuweza kuwa na mnyororo ambao unatambulika, lakini, nitoe maelekezo kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji kwa Mtendaji Mkuu wa DAWASA; suala la Segerea, wananchi wa Segerea hawahitaji ratiba ambazo hazitabiriki. Wananchi wa Segerea wanahitaji kuona kwamba Serikali yao inawajali, wananchi wa Segerea hawahitaji kuona kila siku Mbunge wao anapiga kelele kuhusu Segerea, wananchi wa Segerea tutahakikisha kwamba baada ya kutoa maelekezo haya tunahitaji kuona matokeo na Mkurugenzi wa DAWASA alifanyie kazi kwa ukaribu sana jambo hili ili isiwe kama wimbo wa Taifa katika kutatua changamoto za wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameshatoa maelekezo tusizoee changamoto za wananchi, tuchukue hatua na tuweze kuona matokeo na wananchi wa Segerea wapate huduma ya uhakika na hata kama kuna mgao basi mgao huo uwe na taarifa maalum, lakini pia uweze kutabirika. Ninakushukuru sana.

Name

Christina Solomon Mndeme

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA aliuliza: - Je, lini maji ya Ziwa Victoria yataanza kusambazwa katika Kata za Pangale, Mpombwe, Igigwa, Kisanga, Tutuo, Mkolye, Chabutwa na Ipoje?

Supplementary Question 3

MHE. CHRISTINA S. MNDEME: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa Serikali imekuwa ikitekeleza kwa vitendo Sera ya Maji ikiwemo usambazaji wa maji kutoka Ziwa Victoria na kufikisha maeneo ambayo kuna uhitaji, tunaipongeza Serikali na kuishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita kutuletea mradi wa maji wa Ziwa Victoria, Mkoa wa Tabora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa kuwa bado kuna maeneo mengi Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria bado haujakamilika na hivyo wanawake na wasichana kuendelea kupata shida ya kutafuta maji umbali mrefu.

Je, ni lini Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria utakamilika katika Kata za Kigwa, Goweko, Igalula na Nsololo ili kuwaondolea wananchi adha ya ukosefu wa maji safi na salama katika Wilaya ya Uyui, Mkoa wa Tabora? Ahsante.

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Christina Mndeme, Mbunge Viti Maalum, Mkoa wa Tabora na kwa kumbukumbu yangu inaonesha kwamba katika sekta yetu ya maji leo inawezekana ikawa mara ya tano kuulizia masuala ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kabisa na ni ishara tosha kwamba amedhamiria kuwapambania Wana-Tabora hasa wakina mama ambao wamemtuma kuingia Bungeni na kuwa sauti yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe hofu, Serikali kupitia Wizara ya Maji tutaendelea kukupatia ushirikiano na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alifanya uwekezaji mkubwa wa shilingi bilioni 680 kutoka Ihelele kuja mpaka Tabora na sasa shilingi bilioni 143 kutoka Tabora kwenda Sikonge, Kaliua pamoja na Urambo na huu upande wa Igalula ambapo kuna Goweko, kuna Kigwa na kuna Nsololo. Mradi huo hivi sasa tayari tumeshashusha mabomba ya kutosha ili tuanze usambazaji wa wananchi wa Igalula, Kigwa pamoja na Nsololo. Lengo ni moja tu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kwa vitendo kumtua mama ndio kichwani. Ninakushukuru sana.

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Primary Question

MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA aliuliza: - Je, lini maji ya Ziwa Victoria yataanza kusambazwa katika Kata za Pangale, Mpombwe, Igigwa, Kisanga, Tutuo, Mkolye, Chabutwa na Ipoje?

Supplementary Question 4

MHE. EXAUD S. KIGAHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Mufindi Kaskazini Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupa miradi mingi sana ikiwemo mradi wa maji wa kata tatu: Kata za Ihalimba, Ifwagi na Ikongosi. Mradi huu ni wa kihistoria, lakini umesimama kidogo kwa sababu mkandarasi hajapata fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itampa fedha ili mkandarasi aweze kukamilisha mradi huu wa kihistoria ikiwa ni azma ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kumtua mama ndoo kichwani?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Exaud Silaoneka Kigahe, kama ambavyo amesema kuwa kuna mradi huo mkubwa. Wiki moja iliyopita tulikuwa na ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ndani ya Jimbo la Mheshimiwa Exaud Silaoneka, lakini pia mradi huu ambao ni uwekezaji mkubwa sana una gharama ya shilingi bilioni 41. Gharama hii ni uwekezaji mkubwa sana kuwahi kutokea katika Jimbo la Mufindi Kaskazini ambako Mheshimiwa Mbunge anatoka, lakini pia ni kutokana na ushawishi wake na ufuatiliaji wa karibu sana kuhakikisha kwamba mradi huu unatekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitoa ahadi ya Serikali, ahadi ile ambayo tuliitoa mbele ya Waziri Mkuu iko palepale na utekelezaji wa kuhakikisha kwamba tunasukuma pesa kupeleka upo pale pale. Ninamuomba avute Subira, wakati tunamalizia hatua za mwishoni kum-engage mkandarasi ili aweze kuendelea na mradi huo, ninaamini kwamba ndani ya muda mfupi mkandarasi atarudi na kuendelea na mradi huo. Ninakushukuru sana.

Name

Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA aliuliza: - Je, lini maji ya Ziwa Victoria yataanza kusambazwa katika Kata za Pangale, Mpombwe, Igigwa, Kisanga, Tutuo, Mkolye, Chabutwa na Ipoje?

Supplementary Question 5

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaomba niipongeze Serikali na kukupongeza wewe mwenyewe Waziri, uli-sign Mradi wa Ng'ang'ange na tumepatiwa pesa. Je, ni lini sasa Mradi wa Kihesa Mgagao ambao tayari 85% mkandarasi ameshatekeleza utapatiwa pesa ili wananchi waweze kupata maji safi na salama?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati kwa kutambua na kwa kuleta mrejesho. Alikuwa na anaongelea Ng'ang'ange kila siku akisimama hapa bungeni na Mheshimiwa Rais amepeleka fedha ndani ya mradi ule na tayari Mheshimiwa Kabati amepata matumaini ya kwamba Serikali hii inasema na kutenda na wananchi wasubiri matokeo ya kuona maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimtoe hofu, katika huu mradi ambao umefikia 80% na kitu nimtoe hofu. Kwa staili hiyo hiyo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kusema na kutenda nakuhakikishia hilo nalo tutalifanyia kazi ili kuhakikisha kwamba wananchi wa Kilolo waendelee kufurahia huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana.

Name

Kija Limbu Ntemi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katoro

Primary Question

MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA aliuliza: - Je, lini maji ya Ziwa Victoria yataanza kusambazwa katika Kata za Pangale, Mpombwe, Igigwa, Kisanga, Tutuo, Mkolye, Chabutwa na Ipoje?

Supplementary Question 6

MHE. KIJA L. NTEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mheshimiwa Waziri kwanza nikupongeze kwa majibu mazuri unavyoendelea kutujibu; lakini Mheshimiwa Waziri katika Jimbo la Katoro ni kweli umetuletea maji lakini changamoto maji yanakatika sana, wakati mwingi maji hayapatikani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inapofika wakati wa kusoma mita kwamba tulipe sasa maji ndipo maji yanaweza kutoka siku mbili ili watu waweze kulipa zile bili.

Mheshimiwa Waziri, nini kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba Wananchi wa Katoro wanapata maji wakati wote kwa sababu Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amewekeza fedha nyingi ili wananchi wale waweze kupata maji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate uhakika wa wananchi wa Katoro kuweza kupata maji kila siku au kuna changamoto gani ambayo inasababisha maji yanakatika?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kija Ntemi, Mbunge wa Katoro, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia fursa hii kumshukuru sana, yuko Bungeni, lakini anajua kinachotokea ndani ya jimbo lake, hii ni kuonesha kwamba ametumwa kufanya kazi ya wananchi na wananchi wanaona matokeo ya kumchagua. Nakupongeza sana na hii niitumie kama fursa ya kupata taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge ili sasa Serikali twende tukafanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji namwelekeza Regional Manager wa RUWASA Mkoa wa Geita aende Katoro akafanyie kazi hiyo changamoto. Tujiridhishe changamoto ni nini, kama ni upungufu wa maji ama ni changamoto ya umeme. Baada ya hapo tutajua tunachukua hatua gani ili mradi tu wananchi wa Katoro wawe na uhakika wa kupata huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana. (Makofi)

Name

Dr. Regina Christopher Malima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ENG. AMOSY W. MAGANGA aliuliza: - Je, lini maji ya Ziwa Victoria yataanza kusambazwa katika Kata za Pangale, Mpombwe, Igigwa, Kisanga, Tutuo, Mkolye, Chabutwa na Ipoje?

Supplementary Question 7

MHE. DKT. REGINA C. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi na mimi niulize swali la nyongeza kwa niaba ya vyuo na vyuo vikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti kuna changamoto ya baadhi ya vyuo vilivyoko kando kando ya Ziwa Victoria, lakini pia shule za sekondari especially kwenye Majimbo ya Mwibara na hata Jimbo la Ukerewe.

Je, Serikali iko tayari kufanya uhakiki wa shule hizo na zenyewe kuingia katika mpango wa huu Mradi wa Ziwa Victoria? Ahsante.

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Regina kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni suala la msingi sana ambalo Mheshimiwa Mbunge ameliongelea na kwa sababu Watanzania wote kwa mujibu wa Sera yetu ya Maji ya mwaka 2002 Toleo la mwaka 2025 ni kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma ya maji safi na salama hususan katika maeneo haya ya chuo, tutakaa na wenzetu Wizara ya Sayansi na Elimu ya Juu lakini pia Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, kwa upande wa shule za sekondari na msingi ili tuweke mkakati wa pamoja namna ya kwenda kushughulika na changamoto zilizoko katika vyuo, sekondari pamoja na shule za msingi. Lengo ni kutimiza azma ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anakuwa na access ya maji safi na salama. Nakushukuru sana.