Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Emmanuel John Khambay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Primary Question

MHE. EMMANUEL J. KHAMBAY aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga Barabara kilometa 24 kutoka Kona ya Mrara hadi Lango la Hifadhi ya Tarangire kwa upande wa Kijiji cha Mamire kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 1

MHE. EMMANUEL J. KHAMBAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Nina maswali mawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kutambua umuhimu wa machinjio iliyopo ndani ya Halmashauri ya Mji wa Babati, kuna kipande ambacho kinahitaji lami, kipande cha kutoka Junction ya kuelekea Ikulu mpaka Machinjioni na kwenye Machinjio kuelekea kwenye Junction ya Barabara ya Babati - Arusha. Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha kipande hicho cha barabara kwa kiwango cha lami kwa manufaa ya wananchi wa Jimbo la Babati Mjini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, ni lini Serikali itajenga barabara ya kutoka Hangoni mpaka Junction ya kuelekea Ikulu inayopitia Kwere kwa kiwango cha lami?

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nimpongeze sana Mheshimiwa Emmanuel John Khambay, Mbunge wa Jimbo la Babati, amekuwa mfuatiliaji wa mara kwa mara kuhusiana na miundombinu ya barabara katika Jimbo la Babati Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali imeweka mpango mkakati kwenye bajeti zake. Kwanza kuna bajeti za kawaida za TARURA katika Mji wa Babati, na pili, tuna Mradi wa TACTIC ambao pia itakwenda kuboresha barabara za lami na kujenga miundombinu mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu barabara ambayo ameisema Mheshimiwa Mbunge, ya Junction kwenda Ikulu, Junction kwenda Babati. Nimhakikishie tu kwamba, Serikali kwa ujumla wake tumeainisha maeneo yote muhimu ambayo yanahitaji huduma za kijamii na maeneo kama ya kimasoko, stendi, vituo vya huduma, na shule. Maeneo haya yote yanapewa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika mipango yetu ya bajeti tutahakikisha tunatenga fedha kwa ajili ya kujenga barabara hizo kwa kiwango cha lami au changarawe kwa kadiri itakavyowezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nimhakikishie tu kwamba hata hiyo barabara nyingine ambayo ameitaja tutaendelea kuitengea bajeti kwa awamu kuhakikisha kwamba Wananchi wa Jimbo la Babati Mjini wanapata barabara bora kwa shughuli za kiuchumi. (Makofi)

Name

Agnesta Lambert Kaiza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. EMMANUEL J. KHAMBAY aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga Barabara kilometa 24 kutoka Kona ya Mrara hadi Lango la Hifadhi ya Tarangire kwa upande wa Kijiji cha Mamire kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 2

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kuniona. Barabara ya kutokea Tabata - Mwananchi kuelekea Savana – Mawezi, ni barabara ya kimkakati na Serikali imekuwa ikiahidi mara kwa mara kuijenga, lakini hivi hapa ninapoongea hiyo barabara haipitiki na wiki mbili zilizopita tumepoteza mtoto wa Darasa la Saba kutokana na maji kujaa kwenye ile barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu kwa Serikali, ni nini maelekezo ya Serikali ya dharura ya kuweza kusaidia barabara ile iweze kupitika kwa kipindi hiki cha mvua wakati tunasubiri sasa utekelezaji wa ujenzi wa hiyo barabara? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba ziko barabara ambazo zimeathiriwa na mvua nyingi ambazo zinaendelea kunyesha hapa nchini na katika Mkoa wa Dar es Salaam, na bado mvua zinaendelea kunyesha. Kwa hiyo, tunafahamu kwamba barabara hii ya Tabata - Mwananchi - Mawezi ni moja ya barabara ambayo imeharibiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kwanza, kuwapa pole wananchi wa eneo hilo kwa kumpoteza mtoto, na nitumie nafasi hii kutoa wito kwa walezi, wazazi na wananchi kwa ujumla kujaribu kuwa-guide vizuri watoto wetu katika kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha. Madimbwi ya maji yamekuwa mengi, tujaribu kuwa-guide na kuwasimamia kwa karibu ili kuondoa madhara ya aina hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tumeshapokea barabara hii ya Tabata – Mwananchi – Mawezi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, TARURA na tumeshakubaliana na Meneja wa TARURA, Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Wilaya ya Ilala kwamba, mapema iwezekanavyo baada ya mvua kukatika, ijengwe barabara ile ifanyiwe matengenezo iweze kupitika vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa tumekubaliana kwamba maeneo yote ambayo yanaweza kurekebishwa kwa dharura ili kuwezesha wananchi kupita, yaweze kufanyiwa hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninawasisitiza Meneja wa TARURA - Ilala na Dar es Salaam, wafike eneo hilo waone kinachoweza kufanyika kwa dharura ili kuwezesha wananchi kuendelea kupita kwa usalama. (Makofi)

Name

Mashimba Mashauri Ndaki

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Magharibi

Primary Question

MHE. EMMANUEL J. KHAMBAY aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga Barabara kilometa 24 kutoka Kona ya Mrara hadi Lango la Hifadhi ya Tarangire kwa upande wa Kijiji cha Mamire kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 3

MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ni takribani mwaka sasa mkandarasi anayejenga kipande cha barabara kilometa mbili kutoka katikati ya Mji wa Malampaka kwenda Kituo cha Afya cha Malampaka apewe kazi, lakini ameondoka kwenye site kwa sababu hajalipwa fedha zake. Ni lini Serikali itamlipa mkandarasi huyu ili aweze kuendelea na ujenzi kwa kiwango wa lami katika kipande hicho? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mashimba Ndaki, Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki kwamba, tunafahamu kuna mkandarasi ambaye alipewa kujenga barabara katika eneo la Malampaka kuelekea Kituo cha Afya cha Malampaka; na tunafahamu kwamba kutokana na changamoto za kiutendaji, na pia za kifedha, alisimama kwa muda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge na Wananchi wa Maswa Mashariki, kwamba tayari tumeshapokea andiko na maombi kutoka Halmashauri ya Maswa kutoka kwa Meneja wa TARURA na tayari Serikali iko kwenye taratibu zetu za mwisho za kuhakikisha kwamba tunapata fedha hiyo na kumlipa mkandarasi ili arejee, aweze kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo. Kwa hiyo, barabara hiyo itakamilishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali itafanya kazi hiyo mapema iwezekanavyo. (Makofi)