Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Subira Khamis Mgalu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza utekelezaji wa Mradi wa TACTIC katika Jimbo la Bagamoyo baada ya usanifu kukamilika?
Supplementary Question 1
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza, niishukuru Serikali kwa kuifanya Bagomoyo iwe sehemu ya miji 45, na hata jibu la swali hili kuitamka Bagamoyo kama Halmashauri ya Mji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, wananchi wa Kata za Dunda, Magomeni na Nia Njema walishajiandaa, wakabomoa nyumba zao na maeneo yao ya biashara kwa barabara zinazotaka kujengwa; hata hivyo, hali ni mbaya barabara hazipitiki ikiwemo pia stendi yetu. Ninatambua jibu limesema kuna stendi itajengwa; hii ni ya mkoa, lakini tuna hali mbaya kwenye stendi ya Bagamoyo, kwani iliyopo sasa inajaa maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali haioni kuna haja ya kuja na mpango wa dharura wakati tukisubiria mradi huu mkubwa wa TACTIC?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa tarehe 29 mwezi wa nne nilifanya ziara katika Jimbo la Bagamoyo kwenye maeneo ambayo yameathirika kwa kiwango kikubwa na mvua; kwenye Kata ya Mapinga maeneo ya Kwakibosha, Kimele, Changoyela, Minazi minane, pia maji yameingia kwenye Kata ya Nianjema, je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya TARURA kuja na mpango wa dharura kwa yale maeneo ambayo hayapitiki kabisa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua Serikali inajipanga kuzijenga baada ya mvua kwisha, lakini sasa hivi wananchi wamezungukwa na maji na barabara hazipitiki na wawekezaji wanaojenga viwanda ikiwemo Kiwanda cha Oasis pale Mapinga wanashindwa kufika katika maeneo yao. Je, Serikali iko tayari?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana dada yangu Mheshimiwa Subira Khamis Mgalu, Mbunge wa Bagamoyo. Ni kweli kwamba ziko barabara ambazo zimeathiriwa na maji kutokana na mvua nyingi ambazo zimeendelea kunyesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwanza tulishatoa maelekezo, na maelekezo haya yanaendelea kutekelezwa na Mameneja wa TARURA ngazi ya wilaya na mkoa kote nchini kwamba, maeneo yale ambayo yameathiriwa na mvua na barabara hazipitiki kabisa. Ikiwa kuna uwezekano kitaalamu wa kufanya matengenezo na kuwawezesha wananchi kuendelea angalau kupita kwa kipindi hiki wakati tunasubiri hali ya hewa ikae vizuri na kujenga kwa hali ya kudumu, wafanye hivyo mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kipindi cha miezi mitatu minne iliyopita imepeleka zaidi ya shilingi bilioni 21.4 kwenye halmashauri zetu, kwenye majimbo yetu, kwa ajili ya kurekebisha barabara hizi kwa dharura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitumie nafasi hii nimwelekeze pia Meneja wa TARURA Bagamoyo na Mkoa wa Pwani kuendelea kufuatilia kwa karibu maeneo yote yaliyotajwa na Mheshimiwa Mbunge, ambayo ni Sarunda, Magomeni, Nianjema, Mapinga na maeneo yote ambayo yanaweza kurekebishwa kwa dharura yarekebishwe. Yale ambayo lazima tusubiri hali ya hewa ikae vizuri, kwa sababu hatuwezi kujenga barabara juu ya maji, basi tuwaombe kwamba taratibu za maandalizi yafanyike kwa ajili ya ujenzi huo. (Makofi)
Name
Cornel Lucas Magembe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chato Kaskazini
Primary Question
MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza utekelezaji wa Mradi wa TACTIC katika Jimbo la Bagamoyo baada ya usanifu kukamilika?
Supplementary Question 2
MHE. CORNEL L. MAGEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Serikali imekuwa ikifanya usanifu katika Mji wa Chato katika ujenzi wa soko kuu pale mjini Chato, pamoja na barabara ya kilometa nne za Mji wa Chato ikiwemo soko la samaki pale Kasenda, Kata ya Muganza. Usanifu ule umechukua muda mrefu na kila mwaka tunakuwa tunaahidiwa kwamba mradi ule wa TACTIC unakwenda kuanza kutekelezwa. Sasa ninaomba kupata majibu sahihi, ni lini sasa utekelezaji wa miradi hii mitatu unakwenda kuanza? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Magembe, Mbunge wa Jimbo la Chato Kaskazini, kwamba ni kweli Mji wa Chato ni miongoni mwa miji 45 iliyoko kwenye Mradi wa TACTIC, na mji huu uko kwenye TACTIC Awamu ya Tatu, hii ambayo sasa tumekamilisha usanifu wake. Tunaelekea sasa kuanza taratibu kwa kushirikiana na Benki ya Dunia kwa ajili ya kuanza ujenzi wa miradi hii. Tunafahamu kuna soko, kuna barabara na miundombinu mingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie tu kwamba Serikali iko kwenye hatua nzuri ya kuanza utekelezaji wa mradi huu na wananchi wa Chato na Mheshimiwa Mbunge ninawaomba wawe na amani, Serikali itakwenda kutekeleza mradi huo.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved