Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Haji Kombo Mdowe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nungwi
Primary Question
MHE. MDOWE HAJI KOMBO aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga ukuta katika Fukwe za Bahari ya Nungwi Kiungani ili kuzuia bahari kuingia katika makazi ya watu?
Supplementary Question 1
MHE. MDOWE HAJI KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Nungwi wanataka kujua, ni lini tathmini hiyo itakamilika? Kwa sababu kuanzia mwaka wa fedha wa 2023/2024 majibu ya Serikali yalikuja kuhusu tathmini. Ninanukuu; Waziri wa wakati huo alijibu: "Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar imetenga fedha jumla ya shilingi milioni 650..."
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kombo, utakuwa kama unachangia, uliza tu swali.
MHE. MDOWE HAJI KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini sasa tathmini hiyo itakamilika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kadiri siku zinavyokwenda, hali inazidi kuwa mbaya. Sasa tunataka kujua sisi kama wananchi wa Nungwi, ni zipi hatua za dharura ambazo Serikali zitaichukua kukabiliana na hali ile pale? (Makofi)
Name
Kwagilwa Reuben Nhamanilo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Handeni Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, ameshafika ofisini kwetu takribani mara tatu au mara nne kwa ajili ya kufuatilia jambo hili. Hata jana alikuwepo ofisini kwetu. Tayari imeshafanyika tathmini ya awali kwa Zanzibar yote, na tumebaini maeneo karibia 148 ambayo yameathirika zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hayo maeneo 148, maeneo 123 yako Pemba na maeneo 25 yako Unguja. Serikali baada ya kufanya tathmini hiyo imeanza kutekeleza mradi wa mabadiliko ya tabianchi kukabiliana nayo katika ngazi ya jamii. Tayari tumeshaanza kwa awali na halmashauri 11 kule Zanzibar na halmashauri 54 Tanzania Bara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua inayofuata baada ya tathmini hii kukamilika, tunakwenda kufanya tathmini ya kubaini gharama kwa kila eneo ambalo limeathirika yakiwemo maeneo anayotokea Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la pili, ametaka kujua ni hatua za dharura ambazo Serikali inachukua. Kwenye eneo la Mheshimiwa Mbunge Wilaya ya Kati tumebaini maeneo matatu ambayo yameathirika zaidi kuliko maeneo mengine. Maeneo hayo ni Wadi ya Cheju, Wadi ya Chakwa, pamoja na eneo la Wadi ya Ubago.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti hii tunayokwenda kuitekeleza kwenye bajeti ambayo Bunge hili limetupitishia, tumetenga kwa nchi nzima kwa maana ya pande zote mbili kupitia Fungu 31, zaidi ya shilingi bilioni 31 ambazo zitatekeleza miradi hii ya mabadiliko ya tabianchi kwa awamu na awamu itakapofika tutajielekeza kwenye maeneo hayo ya Cheju, Chakwa na Ubago. Ninaomba kuwasilisha.
Name
Moshi Selemani Kakoso
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tanganyika
Primary Question
MHE. MDOWE HAJI KOMBO aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga ukuta katika Fukwe za Bahari ya Nungwi Kiungani ili kuzuia bahari kuingia katika makazi ya watu?
Supplementary Question 2
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko ya tabianchi yamelifanya Ziwa Tanganyika kuwa na mwelekeo tofauti uliosababisha wananchi wa Kata ya Ikola, Isengule, na Karema kukosa makazi baada ya ziwa hilo kuvamia makazi ya wananchi. Je, ni lini Serikali itaenda kujenga tuta kwenye maeneo ya kata hizo tatu?
Name
Kwagilwa Reuben Nhamanilo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Handeni Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kujibu kwenye swali la msingi, Serikali kupitia Mradi huu wa Mabadiliko ya Tabianchi tunatekeleza mradi huu kwa awamu kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali itakapopata fedha, wananchi hao tutakwenda kuwahudumia kwa kujenga kuta kwenye eneo hilo kama ambavyo tumefanya kule Mikindani na kule Sepwese Pemba.
Name
Boniphace Mwita Getere
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Primary Question
MHE. MDOWE HAJI KOMBO aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga ukuta katika Fukwe za Bahari ya Nungwi Kiungani ili kuzuia bahari kuingia katika makazi ya watu?
Supplementary Question 3
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi kama huu wa tabianchi ulifanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, na ulikuja kwenye halmashauri kwenye majimbo mawili ya Bunda na Mwibara. Umetekelezeka Jimbo la Mwibara, ni lini sasa utatekelezeka Jimbo la Bunda? Ninakushukuru. (Makofi)
Name
Kwagilwa Reuben Nhamanilo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Handeni Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kujibu kwenye swali la msingi, kwa upande wa Tanzania Bara, mradi huu tunautekeleza kwenye halmashauri 54 na tunautekeleza kwa awamu kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha, na mradi huu tutautekeleza kwa mwaka huu wa fedha unaoisha na mwaka ujao wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maeneo yote ambayo tumeyaainisha ikiwemo maeneo ya jimbo lake, tutakwenda kutekeleza mradi.
Copyright © Bunge Polis 2026. All Rights Reserved